| | 0 Comment| 7:53 pm

Categories :

Pale mtu anapolia machozi ni rahisi sana mtu mwingine kuyaona machozi hayo yakitiririka kutoka machoni kwenda mashavuni hata mpaka kwenye kidevu.

Kama kuna mtu amekuwa akikusubiri upate shida afurahi ni rahisi sana kutambua kuwa muda wake umefika wa yeye kufurahi.

Kadhalika kama kuna mtu alikuwa anakutegemea wewe kama shujaa wake, ataanza kuogopa kama wewe shujaa wake unalia itakuwa vipi kwake?

Kama kuna mtu alikuambia kuwa kuna jambo huwezi kufanya na kukuonya kuwa unajisumbua na kuumia bure, utakuwa ni muda mzuri kwake kutoa ushuhuda kuwa alijua tu.

Kumbe njia nzuri ya mtu kutokutambua kuwa unalia machozi ni kulilia kwenye mvua. Unapolia ingali mvua inanyesha machozi hayo yatakuwa yanasafishwa na matone ya mvua au hata kama yatabaki machoni atakayeyaona atajua ni matone ya mvua.

Ukiweka malengo na mipango na kuanza kufanyia kazi kisha ukaanza kupata changamoto, usimwambie kila mtu kuhusu changamoto zako. Ukifanya hivyo;
[ ] Wale walikuwa wanasubiri ushindwe ndiyo watapigilia msumari kwenye kidonda
[ ] Wale walijaribu na kushindwa watakuwa na nguvu kubwa kukupa ushuhuda wa kushindwa kwao

Hivyo ukikutana na changamoto kubwa ya kukukatisha tamaa si muda wa kujitenga na malengo yako bali baki huko huko.

Kuendelea kuweka jitihada licha ya changamoto unazokutana nazo inakupa nafasi ya kutokata au katishwa tamaa.

Kuendelea kuweka jitihada licha ya changamoto inatoa ukinzani kwenye vikwazo vilivyo mbele yako. Unashuriwa kuendelea kushusha nyundo juu ya jiwe hata kama unaona halitikisiki. Muda utafika litapasuka tu.

Hii ndiyo dhana ya kutembea kwenye mvua pale unapolia machozi. Unapokutana na changamoto, usiipe nafasi changamoto hiyo ikukutishe tamaa, endelea kula nayo sahani moja mpaka inyoshe mikono.

Kila la kheri katika mapambano ya changamoto inayoikabili sasa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *