Anza Kuvunjika Ndani……Tengeneza Maisha!
Kuna namna mbili za kuvunjika kwa yai ambako kuleta maana mbili tofauti.
Kama yai litavunjika kutoka nje, hili ni kiashiria kuwa uhai wa yai lile ndiyo umeishia hapo. Hata kama litakuwa limevunjwa kwa ajili ya kupikwa, lakini hapo hakuna maisha tena ya yai hilo. Kuvunjika kutoka nje ni MWANZO WA KIFO.
Lakini kuna kuvunjika ambako hutokea kutoka ndani, namna hii ina maana sana. Kuvunjika kutoka ndani hutokeo pale yai linapokuwa limeatamiwa kwenye mazingira sahihi na hivyo kuruhusu kiiini chache kukua.
Kuvunjika kutoka ndani huwa ni MWANZO WA MAISHA. Hii ni hatua ya kifaranga kuwa na maisha kwani bila kuvunjika vile na kifaranga kutoka hakuna maisha.
“Vitu vikubwa huanzia ndani”
Kama unataka kufanya mapinduzi katika maisha yako na kupata matokeo chanya ambayo hujawahi kupata hapa awali, huna budi kuanza kuvunja vitu kuanzia ndani yako
- Vunja mtazamo wa kujiona wewe huwezi. Wewe ni wa pekee, upo pekeyako hapa duniani. Una uwezo wa kipekee ambao dunia inasubiri matunda yako.
- Vunja mtazamo wa uhaba. Dunia ina utele, usiache kuweka juhudi kwa kufikiri utajiri wote umeshachukuliwa. Toa thamani kwa kutumia upekee ulionao. Utalipwa na kuwa tajiri kwa thamani unayotoa.
- Vunja mazoezi. Mazoea ni sumu ya kupiga hatua kubwa. Fanya kwa ubora zaidi ya jana ili upate matokeo ya utofauti kila siku
- Vunja uvivu wa mwili wako. Mwili wako hautaki usumbufu, ni mvivu kwa asili. Usiusikilize, upe kazi upate mafanikio. Mafanikio na kazi ni mapacha.
- Vunja woga ndani yako. Vitu vikubwa hufanywa na watu jasiri. Simamia ndoto yako kubwa bila kuyumbishwa na mtu yoyote. Ni wewe pekee ndiye unayeona mwisho wa kile unachokiota.
Ndugu! Usiyumbishwe na mabadiliko ya nje. Acha hali za nje ziendelee kuvunjika zenyewe. Usijihusishe navyo. Wewe jikite kuvunja mitazamo inayokudidimiza usichukue hatua. Leo unaanza kuvunja mtazamo gani kati ya hiyo hapo juu?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz