Usikatishe Safari Kwa Sababu Umepitwa….


Categories :

Kama utakuwa kwenye gari la abiria halafu ghafla dreva akasimama na kusema tunaahirisha safari kwa sababu kuna gari linelipita(overtake) gari lake na yeye hapendi hilo, ungemshangaa sana.

Kama ungemuona mwanariadha ameacha mashindano kwa sababu tu kuna mtu amempita na yeye hakupenda hilo, ungemshangaa sana. Inawezekana ungemuuliza kama kweli alidhamiria mashindano hayo au la!

Lakini kumbe ni zamu yetu sisi kukushangaa wewe hivyo hivyo kama wewe ambavyo ungeweza kuwashangaa hao?

Naamini utakuwa unajiuliza kuwa ni lini wewe umeendesha gari na kukatisha safari kwa sababu ya kupitwa na gari jingine au ni lini wewe umeshiriki mashindano ya riadha?

Maisha ni safari za kila siku na mipango unayoweka ni mashindano ya kila siku. Umeweka malengo na mipango ambayo unahitaji kuvitimiza. Lakini katika kuyatimiza haya unahitaji kukabiliana na kuzishinda changamoto.

Uliweka malengo na mipango, lakini kabla hujapata matokeo, changamoto zikatokeo(zikakupita). Kama umekata tamaa ya kuendelea kumbuka umekatisha safari baada ya kupitwa na gari.

Una maono makubwa na umeanza utekelezaji sahihi. Lakini baada ya kuona matokeo yanachelewa, umeacha kuweka jitihada. Nakukumbusha kuwa umeacha kukimbia mbio zako kwa sababu mwanariadha mwingine amekupita.

Una malengo makubwa lakini kwa sasa unapata matokeo madogo. Baada ya kuona wengine wanapata matokeo makubwa, umekata tamaa; je kwani ulikuwa unashindana nao?!

Rafiki! Mafanikio makubwa na ya kudumu yapo kwa watu ambao wameondoa msamiati HAIWEZEKANI kwenye akili zao. Hivyo wanaendelea kuweka jitihada mpaka wakutane na INAWEZEKANA.

Usiache kufanya kilichosahihi kwa sababu tu matokeo kuchelewa kwani wengi wameshindwa baada ya kukata tamaa ikiwa ulibakia mstari mwembamba sana kati ya jitihada zao na matokeo.

Chukua hatua;

Tafakari ni lengo gani sahihi uliliacha baada ya kukutana na changamoto? Endelea ulipoishia na weka jitihada mpaka uyapate matokeo.

“Hakuna kitu kitakachokuzuia kupata matokeo kama utaendelea kufanya kitu sahihi bila kuacha”

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *