Je Utaweza Kuruka Kama Tawi Litavunjika?


Categories :

Siku moja nilikuwa nimekaa chini ya mti nikitafakari juu ya maisha ya mwanadamu, ghafla akaja ndege ambaye alinipa funzo kubwa sana.

Ndege huyo alitua kwenye tawi ambalo lilikuwa linakaribia kukatika. Kila alipokuwa anatua, tawi hilo liliendelea kuinana likionyesha kila dalili ya kutaka kukatika. Lakini ndege yule aliendelea kung’ang’ania kusimama kwenye tawi lile.

Tawi lilipokuwa linainama yeye aliruka juu na lilipo tulia alienda tena kusimama kwenye tawi hilo. Baada ya tawi lile kuzidiwa lilikatika kisha ndege yule akaruka na  kuhamia kwenye tawi lililokuwa imara.

Jambo hili lilinifanya nitafakari sana nini maana ya kile kilichokuwa kinatokea kwenye maisha yetu.

Nilijifunza kitu kimoja muhimu sana ambacho nimeamua nikushirikishe na wewe rafiki yangu ili kikusaidie kupiga hatua maishani mwako.

Nilijifunza kuwa “Ndege anaposimama juu ya tawi haweki imani kwenye uimara wa tawi bali kwenye uwezo wake wa kuruka” Irudie kuisoma kauli hii

Ndugu! Kwa jinsi ulivyozaliwa na kukua, umejikuta ukikubwa na mfumo unaokulazimisha ujenge imani kubwa sana kwa watu wengine au kwenye vitu vingine mpaka ukajisahau.

Kama umeshindwa kuonyesha utofauti ambao ungekuwa ndiyo uhalisia wako, basi tambua kuwa umeweka imani nje yako.

Utafanikiwa kuishi kwa mafanikio makubwa kwenye dunia hii iliyojaa ugumu kama kwanza utafanikiwa kujenga imani kubwa sana juu yako.

  1. Amini kuwa wewe ni wa pekee na unaweza kufanya vitu vikubwa na vya kipekee. Hata kama utafanya kilichokuwepo, fanya kwa utofauti.
  2. Usiweke imani kwa watu kabla ya wewe kujenga imani hiyo. Unapowaambia watu inawezekana basi ndani yako usiwe na wasiwasi wowote. Imani ianzie kwako ndipo itoke nje.
  3. Amini kwenye ndoto yako ili hata kama wote waliosema watakusaidia wakirudi nyuma,wewe uweze kuendelea.
  4. Amini kwenye mchakato wa kuvipata vitu ili usiwe mtumwa wa vitu hivyo. Kwa imani hiyo utajiambia kuwa hata kama vyote vitapotea, utaweza kuvipata tena.
  5. Amini kwenye mikakati uliyoweka ya kupata matokeo, ili hata kama matokeo yatachelewa utaendelea kuweka na kufurahia jitihada.

Mafanikio yako makubwa na yenye furaha, yanaanzia ndani yako. Mafanikio hayo yanaanza kwa imani kubwa unayoijenga juu yako.

Upo wewe tu dunia nzima, hakuna mtu mwingine kama wewe. Jiamini; jenga ndoto kubwa kisha zifanyie kazi kwa ujasiri. Hata kama matawi yatakatika yaani utakutana na changamoto, hutashindwa kwani una uwezo wa kuruka kufikia mwisho wako mwema.

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI ni mwongozo kamili wa kukusaidia kujiamini kwa kujua nguvu kubwa iliyolala ndani yako ambayo utakapoiamsha itakusaidia kufanya makubwa katika dunia hii yenye matawi yanayoweza kukatika.

Wasiliana nasi kupitia 0752 206 899 kukipata kitabu hiki kwenye mfumo wa nakala ngumu,  tete na sauti.

Karibu sana.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *