Siri Ya Kuwa Mtu Mwenye Makali.
Kisu kinachosifika kuwa na makali ni kile kilichukubali kupunguza unene wake kisha kubakia na ncha ndogo sana.
Msumari hufanikiwa kupenyeza kwenye mbao na hata zege kwa sababu licha ya ugumu wake lakini hukubali kupunguza nyama zake kisha kuchongoka kwenye ncha mojawapo.
Kadhalika mwiba ni mkali sana kwa sababu ya baadhi ya majani kukua na kuwa imara huku yakipunguza nyama zake na kuwa na ncha kali.
Katika dunia iliyojaa changamoto nyingi, ni watu wenye makali ndiyo wanaoweza kuzikata changamoto hizi kisha kufanikiwa. Kuwa butu kutakufanya ushindwe kuzikata changamoto zitakazosimama mbele yako na hivyo kuwa kikwazo katika kupiga hatua.
Ndugu kama kila changamoto imekuwa kikwazo kwako basi huna budi sasa kuanza kuchukua hatua za kujinoa ili kuwa na makali. Yafuatayo ni mambo unayotakiwa kuyanoa ili uweze kuwa na makali.
1. Msimamo.
Kwenye maisha yako lazima uwe na vitu unavyovisimamia ili usiyumbishwe. Kuna matukio mengi yatatokeo mbele yako na jamii itapendekeza namna ya kuyachukulia, je msimamo wako utakuwa upi?
Msimamo ni upi duniani inapokuambia huna haja ya kujitesa ili ufanikiwe wakati kuna njia za mkato?
Ili kuwa na msimamo punguza kukubali kila unachoambiwa.
2. Fikra.
Tunakuwa kile tunachokifikiri kwa muda mrefu. Tunatenda kulingana na maamuzi. Ili uweze kufanya maamuzi kwa haraka tena sahihi huna budi kunao akili yako na kuwa kali sana.
Unaweza kunoa akili yako kwa kufanya mazoezi ya kutafuta majawabu ya changamoto hata zile ngumu badala ya kuzikimbia.
Punguza kufikiri vitu vingi kwa wakati mmoja.
3. Tabia.
Matokeo unayoyapata maishani mwako ni kwa sababu ya tabia ulizozijenga kwa muda mrefu. Ukijenga tabia za mafanikio utapata mafanikio ukijenga tabia za kushindwa utashindwa.
Ili kuwa na makali jenga tabia ya kujiamini, kuwajibika, nidhamu,….punguza tabia za kushindwa kama kujidharau, kulalalmika,kutowajibika..
4. Kazi.
Kazi ni makali ambayo kila anayetaka kufanikiwa anatakiwa awe nayo. Utakuwa na makali ya kupata mafaniko kama utaipenda kazi na kutouonea huruma mwili wako kufanya kazi.
Punguza uvivu bakia na ncha ya kazi.
5. Kuchukua hatua.
Hata uwe na mipango mizuri, lakini kama huchukui hatua ni bure. Utafanikiwa kuwa na makali haya ya kupata matokeo na kufanikiwa sana kama utaacha kuahirisha mambo.
Baada ya kuja kitu gani ni sahihi, basi jisukume kuchukua hatua ili kupata mafanikio.
Acha kuahirisha bakia na hatua.
Anza kujinoa sasa kwa kutumia vinoleo vya mambo haya matano. Utakuwa na makali ya kusambaratisha changamoto zitakazokuwa zinasimama mbele yako kisha kuyafikia mafanikio yako.
Kitabu cha JENGA NIDHAMU KALI ni mwongozo muhimu sana kwako kuweza kujinoa kisha kukabiliana na changamoto au sababu yoyote ya kukuzuia usipate matokeo ya malengo yako.
Wasiliana kupitia 0752 206 899 ili kujipatia nakala chache za ofa zilizobaki.
Karibu sana.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz