Kifanye Hiki Ili Usije Kujuta Baadaye.
Majuto ni mjukuu. Ukiona mtu anajuta basi tambua kuna kitu hakukifanya. Bahati mbaya majuto huja baada ya muda kupita. Hivyo inakuwa bahati kwako kutambua kitu ambacho usipofanya utajuta kisha ukajisukuma kukifanya ili usijute mbeleni.
Leo nakushirikisha kitu muhimu sana cha wewe kukifanya ambacho watu wengi wamekuwa hawakifanyi na kimeleta majuto makubwa sana kwao. Kitu hicho ni KUJARIBU.
Katika kujenga mafanikio makubwa katika maisha yako, kuna hatua hujawahi kufanya utatakiwa ufanye ili upate matokeo ya utofauti. Njia pekee ya kuvuka hapo huwa ni kujaribu kisha kujifunza kutoka kwenye matokeo unayopata.
Kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa kupata matokeo watu wengi hawapendi kujaribu vitu vipya. Hivyo huendelea kung’ang’ania kufanya vitu kwa namna ile ile wakifikiri watapata matokeo ya utofauti.
Albert Einstein alisema ” Insanity is doing the same thing over and over again and expecting different results.” Ikiwa na tafsiri kuwa ukichaa ni kufanya kitu kile kile mara kwa mara huku ukitarajia kupata matokeo ya utofauti.
Haya ni maneno magumu lakini ndiyo ukweli. Itakuwa ni hasara kama unachokifanya sasa hakikupatii matokeo yanayokuridhisha lakini wewe unaendelea kufanya hicho hicho bila kujaribu mbinu mpya. Einstein anasema huu ni ukichaa.
- Njia unazotumia sasa hazikupatii kipato cha kutosha, kwa nini usijaribu biashara?
- Unapata dharura ukiwa huna fedha hivyo unalazimika kukopa kwa riba kubwa, kwa nini usijaribu kuweka akiba kwenye kila kipato unachokipata?
- Umeanzisha biashara lakini wateja hawaji dukani, kwa nini usijaribu kuwatembelea au kuwapigia simu?
- Umefanya maamuzi kwa kutumia maarifa uliyonayo sasa lakini hayakupi matokeo mazuri, kwa nini usijaribu kusoma vitabu kuhusu kitu unachokifanya?
- Mbinu unayotumia sasa haikupi majibu kwa nini usjaribu mbinu nyingine?
Ndugu! Njia pekee ya kukua ni kujaribu vitu vipya. Njia ya kupata matokeo makubwa basi ni kujaribu mambo makubwa. Usiogope kujaribu kwani kujaribu kufungua milango tofauti ndipo unaukuta wa kukufikisha kwenye ukamilifu wako.
Kitu gani umekuwa ukitamani kukifanya lakini unakiogopa kufanya? Nenda ukakijaribu leo.
Majuto hayapo kwenye kujaribu na kushindwa bali kwenye kutokujaribu.
Nakusihi ujaribu kukipata kitabu cha UWEZO WA KUANZISHA NA KUKUZA BIASHARA kisha ukisome uone kama hakitakuwezesha kuanzisha biashara ya ndoto yako au kukuza mauzo(biashara) ya biashara yako ya sasa. Wasiliana kupitia 0752 206 899 kukipata kitabu hiki. Jaribu kukinunua sasa ili usiendelee na mazoea ya kuahirisha.
Karibu sana.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz