Je Ungetamani Upendelewe Kufanikiwa? Inawezekana, Siri Ipo Hapa…
Kama itatokea kuna nafasi ya kupendelewa kufanikiwa kila mtu angetamani aipate nafasi hiyo.
Kuna watu ambao mmekuwa pamoja kwa muda mrefu hata umri ukiendana, lakini wamepiga hatua kubwa za mafanikio mpaka unahisi wamependelewa.
Najua unatamani sana kupata mafanikio makubwa kwenye kila eneo la maisha yako. Inawezekana muda unaenda lakini huoni dalili ya kufanikiwa katika maisha yako.
Vipi kama leo nitakuibia siri ya kupendelewa kufanikiwa? Utajisikiaje…….naamini utajisikia vizuri!
Siri ya kupendelewa kufanikiwa ipo kwenye matumizi sahihi ya masaa 24 unayopewa kila siku.
Kama kuna watu unawafahamu na unaona wamependelewa kupiga hatua kubwa maishani mwao, basi tambua kuwa wamekuzidi kwenye kutumia vizuri masaa 24 ya kila siku.
Dunia haina upendeleo kwani inatoa muda sawa kila siku kwa kila mtu; saa 24. Baada ya hapo mtu huamua ajipendelee au ajipunje.
Maisha yako yatabadilika sana utakapoanza kuitumia siri hii.
Je huwa unafanya nini na masaa 24 unayopewa kila siku? Je umekuwa ukiupoteza tu muda? Je umekuwa ukifanya hata vitu visivyo na mchango wa kufanikiwa kwenye muda huu mzuri?
Kumbuka ulichonacho maishani mwako sasa ni matokeo ya vile ulivyokuwa unavifanya kwenye saa 24 za kila siku. Kama huridhiki na matokeo, basi sehemu pekee ya kuanza kuibadili ni kwenye matumizi ya saa 24 za siku.
Anza kujipendelea kufanikiwa kwa kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali hii muhimu ya maisha yako.
[ ] Ianze siku yako mapema(alfajiri). Kuna muda mzuri wa utulivu ambapo wengi wamelala, utumie muda huo kujianda; kusoma, kuandika maono, malengo na mipango yako, kusali…
[ ] Pangilia vizuri masaa 24 uliyopewa. Usilale zaidi ya saa 8. Muda mwingi tumia kufanya kazi.
[ ] Usifanye chochote bali kile chenye mchango mkubwa kwenye mafanikio yako.
[ ] Usiahirishe kufanya uliyopanga. Epuka saratani hii ya matokeo.
[ ] Kwenye saa 24 za leo, jitahidi kuwa bora kuliko saa 24 zilizopita.
[ ] Epuka usumbufu unapofanya kazi. Kama ni simu ni usumbufu basi iweke mbali na wewe.
[ ] Kumbuka unachofanya leo ndicho kitaamua nini ukipate kesho, mwezi ujao, mwakakesho au maiaka 10 ijayo.
Saa 24 zipo mbele yako, uamuzi ni wako kujipendelea au kujipunja. Chagua kujipendelea kwa kuchukua hatua za matumizi sahihi ya saa 24 hapo juu.
Nakutakia kila la kheri kwenye upendeleo huu.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwl. & Kocha (Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;Simu 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz