Ya kwanza ni ya kuzaliwa; lakini ya pili ni fumbo kwa wengi. Ukiitambua na kuiishi hii ya pili, basi mafanikio kamili yapo mikononi mwako
Watu wengi wakiulizwa wataje siku mbili muhimu katika maisha yao, wengi watakutajia siku ya kuzaliwa. Siku ya pili imekuwa ikitofautiana kati ya mtu na mtu. Wapo watakaosema ni siku ya kuoa au kuolewa; siku ya kufa; siku ya kupata kazi ya uhakika; siku ya kufanikiwa; siku ya kupanda ndege; siku ya kuwa na biashara n.k. Hii ni kutokana na matukio na matamanio ya mtu.
Siku ya pili imekuwa changamoto kwa watu wengi kutajwa kwa usahihi. Hii ni ishara kuwa wengi hawajaweza kuifikia siku hiyo kwani wangefanikiwa kuifikia siku hiyo bila shaka kila kiungo cha maisha yako kingeshuhudia kuwa hii kweli ni siku muhimu sana maishani.
Kusudi la Makala hii ni kuhakikisha umeifahamu siku hiyo na pia kukusaidia kuishi kwa usahihi kile utakachokipata siku hiyo.
Mwandishi nguli wa Kimarekani,Mark Twain, aliwahi kusema, “The two most important days in your life are the day you are born and the day your find out why.” ikiwa na tafsiri kuwa,“Siku mbili muhimu zaidi katika maisha yako ni siku ambayo ulizaliwa na siku ambayo utagundua kwa nini ulizaliwa.”
Kumbe, baada ya siku ya kuzaliwa(Birthday), siku nyingine muhimu katika maisha yako ni siku ya kujua kwanini ulizaliwa. Siku nyingine ambazo umekuwa ukizitaja zinaweza kuwa muhimu lakini hazifikii umuhimu wa kujua kwanini uliruhusiwa kuwa sehemu ya dunia hii.
★★★
Siku ya kuzaliwa: Kila mtu anaamini kuwa siku ya kuzaliwa ni muhimu sana katika maisha yake. Ndiyo maana kuna watu wengi ambao wameendelea kusherekea siku hizo mpaka ukubwani. Wanaamini bila kuzaliwa basi wasingepata nafasi ya kuwepo hapa duniani. Siku ya kuzaliwa kwako ndiyo ulikuwa mwanzo wa kutambulishwa hapa duniani.
Ulipokuwa unazaliwa dunia ilitambua kuwa kuna mtu anakuja kwa ajili ya kutatua changamoto ambayo ipo. Huu ulikuwa ni utambulisho kuwa kuna mtu mwenye sababu maalumu amezaliwa na kuna changamoto inaenda kutatuliwa. Si hivyo tu, bali, ilikuwa ni utambulisho kuwa kuna mtu wa kipekee, mwenye uwezo wa kipekee na mtenda miujiza amezaliwa.
Hii inapaswa kuwa tafakari kuu kwenye siku unapoadhimisha siku ya kuzaliwa kwako. Kwenye siku hiyo jiulize ni kwa sababu gani nilizaliwa na nina nguvu gani ya kipekee ndani yangu. Hayo ndiyo yatakuwa maadhimisho bora kabisa ya siku yako ya kuzaliwa.
★★★
Siku ya kutambua kwanini ulizaliwa:
Mtu huzaliwa angali yeye mwenyewe na watu wengine hawajui kwanini amezaliwa. Lakini hii siri huwa ndani ya mtu na Yule aliyemuumba, yaani, Mungu. Licha ya mtu kuwa na nafasi ya kutambua kusudi lake lakini imekuwa siyo kazi rahisi kama unavyofikiri, hivyo, kuna watu wengi wanaoendelea kuishi maisha tofauti na makusudi yao. Wapo pia ambao wamekufa bila ya kutambua na kuyaishi makusudi yao.
Ugumu huu wa kutambua kusudi la maisha yako ndiyo linaloleta umuhimu mkubwa wa siku hii ya kutambua sababu ya wewe kuzaliwa. Kumbuka pale unapofanikiwa kulitambua kusudi lako ndipo unapoweza kusema,“Nimejipata baada ya kujitafuata kwa siku nyingi.”
Kuna sababu nyingi zinazosababisha watu wengi kutotambua makusudi yao, lakini, kubwa zaidi ni kutoelewa kuwa kuna sababu maalumu ya wao kuzaliwa pamoja na kusikiliza kelele za dunia. Maoni ya watu juu yako yamekuwa kelele zinakufanya usisikilize sauti ya ndani yako inayokutambulisha wewe ni nani na kwanini upo hapa duniani.
Sauti pekee ya ukweli itakayokuambia kwa nini wewe upo hapa ni ile kutoka ndani yako. Kumbuka wewe wa ndani ndiye aliyeunganishwa na Muumba ambaye anakujua vizuri sana wewe na anajua siri zako.
Lakini umeshindwa kuisikia sauti hii kwa sababu ya kelele za jamii zinazosema wewe wa kawaida, wewe huna maana, wewe huna akili, wewe ni maskini, n.k.
Rafiki itakuwa ni hasara kubwa kama utaendelea kuishi hapa duniani bila kufanya kile ulichokusudiwa kufanya. Kadhalika itakuwa ni hasara kubwa sana kama utakufa bila ya dunia kufaidi kile ‘spesho” ulichokibeba wakati unazaliwa.
Utajisikiaje kama leo nitakuambia kuna mwongozo wa kukusaidia kuifikia siku hii muhimu ya pili ya maisha yako?…….naamini utajisikia vizuri. Habari njema ni kuwa nikiwa naadhimisha siku yangu ya kuzaliwa ningali tayari nimeshaitambua siku yangu ya pili (kutambua kusudi la maisha yangu) nakupa zawadi ya kitabu ambacho nawe kitakusaidia kuitambua siku hii muhimu.
Kitabu hiki ni NGUVU YA KUSUDI. Hiki kitakuwezesha kutambua na kuishi kusudi la maisha yako ili uweze kupata mafanikio kamili ungali hapa duniani.
Kitabu hiki kinaenda kukusaidia kuzishinda kelele za dunia ili uifikie siku muhimu ya kujua kwanini ulizaliwa. Siku hii itakuwa ni mwanzo mpya wa maisha yako; si hivyo tu, bali utaanza kuona umuhimu wako wa kuwepo hapa duniani.
Kuipata zawadi hii muhimu sana siku hii ya leo, tafadhali wasiliana nami kupitia 0752 206 899. Wasiliana nami leo, usiiache leo ikapita.
*“Kabla hujafa, tambua kuna siku mbili muhimu sana katika maisha yako: siku ya kuzaliwa na siku ya kutambua kusudi la maisha yako.”
Karibu sana;
Alfred Mwanyika
Scientist, Author & Trainer (Uwezo & Mafanikio)
AMSHA UWEZO
0752 206 899
www.amshauwezo.co.tz