Simu Unayoitafuta Ndiyo Hiyo Unayomulikia


Categories :

Kuna jamaa mmoja alikuwa na simu janja nzuri aliyoipenda sana. Kila wakati alitamani alipo na yenyewe iwepo hapo. Alifanya hivyo kwa siku nyingi huku akiomba na kutamani asiipoteze simu yake.

Siku moja usiku umeme ulikatika na hivyo ndani ya nyumba kukuwa giza. Giza hilo halikumtisha kwani alikumbuka simu yake ina tochi hivyo angeweza kuiwashana kupata mwanga. Aliiwasha na kuiweka juu ya meza ili iendelee kutoa mwanga chumbani. Baada ya muda kupita bila kuwa na simu mkononi mwake akahisi kuna kitu amepungukiwa na hivyo kuamua kuanza kutafuta simu yake. Kwa sababu kulikuwagiza, ilimulazimu kuchukua ile tochi iliyokuwa inamulika kile chumba ili kutafutia simu yake.

Aliitafuata simu yake kwa muda mrefu bila mafanikio na ndipo allipoamua kumuita ndugu yake aliyekuwa chumba ili aje kumsaidia kutafuta. Lakini muda huo tayari alikuwa kwenye masikitiko, malalamiko, kukata tamaa kwa kujua ameshaipoteza simu yake. Ndugu yake alipofika chumbani hapo, yule jamaa akamueleza yaliyotokea na kuwa amepoteza simu yake na ameitafuta kwa muda mrefu bila mafanikio. Ndipo rafiki yake alipo mshangaa sana huku akimuambia kuwa mbona simu unayoitafuta ndiyo hiyo uliyoishika mkononi na unaitumia kama tochi?

Haya ndiyo maisha ambayo watu wengi wamekuwa wakiishi. Umekuwa ‘busy’ sana ukitafuta vitu unavyovitamani ukihisi vipo mbali mno na wewe. Umejiambia kuwa wewe watu fulani ndiyo wenye uwezo wa kuwa na mafanikio lakini sio wewe.

Uwezo upo ndani yako. Mimi siwezi kufanya hilo, hayo mambo ni ya watu fulani!. Kwa nini unajidharau kwa kuona wewe huna uwezo wa kufanya mambo makubwa na kuwapa kipaombele watu wengine kuwa wao ndiyo waliopendelewa uwezo wa kufanya makubwa.

Ndugu! Una uwezo mkubwa na wa kipekee nadani yako. Nguvu za pekee unazozithibitisha kwa watu wengine zipo ndani yako pia.

Wazo la biashara lipo ndani yako. Nina mtaji sijua biashara gani niifanye? Biashara gani inalipa sana kwa sasa? Mbona kila biashara inayoanzishwa inakufa? Hii ni ishara kuwa umekuwa unafikiria wazo la biashara linaanza nje yako. Au umeamini kuwa kuna watu fulani ndiyo wa kufanya biashara.

Lakini kila mtu ana uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara ya mafanikio hata bila ya kuiga nini mtu mwingine anakifanya. Wazo bora la biashara linaanzia ndani yako kwa kutafakari kitu gani unakipenda sana kukifanya, yaani upo tayari kukifanya hata kama hulipwi! Kisha kuunganisha kitu hicho na matataizo au chagamoto zilizopo kwenye jamii. Wazo bora la biashara lipo ndani yako, usimulike kwingine.

Mtaji wa kuanzi unao. Je umekuwa ukisingizia kuwa huanzi biashara kwa sababu huna mtaji? Kama umekuwa unapata kipato hata kama kidogo huko ndiko kwenye chanzo cha mataji wako. Anza leo kuweka asilimia hata kumi kwenye kila kipato unachokipata, baada ya muda fulani akiba hiyo itaongezeka na kuwa fedha kubwa ya kuanzisha biashara hata kama ni kidogo.

Je una vitu vingapi nyumbani kwako ambavyo huvitumii ulivyonunua kwa tamaa tu baada ya kuonana na muuzaji au baada ya kuona jirani anachao? Uza vitu hivyo na pata mtaji. Unaona ndugu! Unatafuta vitu ambavyo tayari unavyo.

Wateja unao tayari. Biashara ni ngumu sana, wateja hamna, siku hizi wateja wamekimbilia sehemu fulani nk. Je ni kweli huna wateja wa biashara yako? Hiyo si kweli, je majirani zako wote wanajua biashara uliyonayo? Je watu wote ambao umewahifadhi kwenye simu kwa namba zao za simu umeshawataarifu na kuwashawishi wanunue biashara yako. Wateja unao karibu yako acha kumulika mbali.

Ndugu! Vitu vingi ambavyo umekuwa ukivitafuta tayari vipo ndani yako au karibu na wewe kama tulivyoona kwenye mifano michache hapo juu. Kwa hiyo kuanzia sasa usiseme siwezi kufanya hiki kwa sababu sina hiki, au siwezi kuendeleza kitu fulani kwa sababu sina kitu fulani. Vyote vipo mikononi mwako, chunguza vizuri.

Tafakari, leo utaanza nini ulichoahirisha siku nyingi kwa kujua huna kitu fulani!

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo na mafanikio,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *