Mtu Mwenyewe Ni Wewe Na Muda Wenyewe Ni Leo.


Categories :

Tangu utotoni kuna maisha fulani hivi umekuwa ukiyatamani kuishi. Kuna wakati umepata picha kamili ya maisha hayo, kuna muda umishia kusema maisha fulani mazuri.

Mchakato ulianza wa kuanza kutafuta maisha hayo; ulipoingia shule ya misingi ukafikiri maisha hayo yataonekana ukishamaliza shule ya msingi na kwenda labda sekondari. Inawezekana uliendelea na kutafuta elimu kwa muda mrefu mpaka elimu za juu na kuona maisha yako mazuri yapo sehemu fulani.

Inawezekana pia uliishia hatua fulani ya elimu na ukaendelea kuyafikiria maisha yako mazuri unayostahili yapo eneo fulani.

Hizi zimekuwa ni fikra za watu wengi kuona maisha fulani anayostahili yapo sehemu fulani yatakuja muda fulani, na yameshikiliwa na mtu fulani. Fikra hizi zimewafanya watu kuendelea kusubiri na kuona ngoja waendelee kuishi yamkini watakutana na maisha hayo huko mbeleni.

Kwa kufikiri hivyo watu wameendelea kusubiri huku umri ukizidi kwenda. Baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila matokeo wamesihia kulaamu watu wengine kuwa wameshindwa kuwatengenezea maisha wanayostahili. Pia wapo walioona kuwa dunia hii ina upendeleo, kuna watu wana bahati zao wengine hawana.

Je na wewe ni miongoni mwa watu watu hao wanaoendelea kusubiri maisha hayo yawafikie? Je unaamini kuna mtu ameshikiria mustakabali wa maisha yako? Je umekuwa ukiamini kuwa kuna watu wachache wenye haki ya kuwa na mafanikio lakini sio wewe?

Ndugu! Mafanikio ni haki yako ya kuzaliwa. Kama ulifanikiwa kuja hapa duniani basi una kitu cha pekee sana ambacho hakuna mtu mwingine aliyenacho. Kitu hicho ni uwezo wa kipekee na ndiyo unaoweza kukupa mafanikio ya kipekee.

Mafanikio ambayo umekuwa ukifikiria na kuyatamani, mara nyingine ukifikiri yapo mbali sana, si kweli kuwa yapo mbali bali karibu sana yaani ndani yako. Uwezo wako umekamilika kukupa chochote unachotaka kama utafanimiwa kuuamsha. Mafanikio yoyote yanaanza kama mawazo kisha kuwekwa kama vitendo. Moyo na akili yako vina wazo zuri la mafanikio yako, visikilize kwa umakini.

Hakuna mtu mwingine anayeweza kukupa maisha unayostahili isipokuwa wewe mwenyewe. Usiendelee kusubiri mtu huyo, kwani hayupo. Chukua wajibu wa asilimia mia moja kutengeneza mafanikio yako. Tambua kilicho sahihi kufanya kisha anza kufanya.

Umekuwa ukisubiri sana kuwa kuna muda maalumu wa kuanza kutengeneza mafanikio yako. Kila ulipofikiri kufanya kitu fulani ukaona kama muda bado na umeendelea kuahirisha mpaka leo. Hii ndiyo sababu iliyokufanya kutokuwa na matokeo mpaka leo.

Maisha ya mafanikio yako yameshikiliwa kwenye muda. Hakuna unachoweza kufanya kama huna muda. Lakini kama ungali hai unaweza pia kufanya na kurekebisha makosa ambayo umekuwa unafanya. Leo naomba uanze kwa kurekebisha makosa haya mawili.

La kwanza; Usiendelee kusubiri mtu aje akutengenezee mafanikio, bali tambua mtu huyo ni WEWE MWENYEWE na jiweke tayari.

La pili: usiendelee kuona kuwa muda bado. Hakuna siku nyingine ambayo utaambiwa kuwa ndiyo maalumu kwa wewe kufanya ile mipango mizuri uliyonayo bali ni LEO tena sasa.

Anza leo kwa kurekebisha makosa hayo mawili. Fufua mipango yako uliyokuwa unaiahirisha kila siku. Na muda wa kufanya hayo yote ni leo tena sasa; usiahirishe tena.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *