Haya Ndiyo Maumivu Yenye Faida Ya Kuyapokea.


Categories :

“Maumivu ya magurudumu ya gari hufanya gari lisogee. Maumivu ya kuni huivisha chakula. Kadhalika maumivu ya nyundo hutengeneza samani”

Magurudumu ya magari ndiyo yanayogusana na ardhi na kisha kupata msuguano na barabara pale yanapozunguka. Maumivu hayo ya magurudumu ndiyo yanayowezesha gari kusogea na kufika safari yake. Ili kuni ziweze kuivisha chakula ni lazima zikubali maumivu ya kuungua na kutoa joto litakalofanya chakula kiive, kiwe salama na kitamu. Hayo ndiyo maumivu yenye faida.

Kadhalika ili msumari uweze kugongelewa kwenye mbao na kutengeneza samani kama meza kabati, sofa na mapambo mazuri, hauna budi kuvumilia maumivu ya nyungo ambayo inashuka juu yake ili kuweze kuushindilia ndani.

Maisha ya binadamu yametawaliwa na maumivu. Fikiria tu unapofanya mazoezi ili kuimarisha misuli unakabiliwa na maumivu na unahitaji kuyavumilia maumivu hayo ili uweze kuweza kuimarisha afya yako. Pia unapofanya kazi ili kupata matokeo fulani utakabiliwa na maumivu. Hivyo hakuna namna utakayozuia maumivu halafu ukapata matokeo yenye maana kwenye maisha yako.

Kumbe kuzuia maumivu ni kama kuyakimbia mafanikio.  Waulize waliofanikwa, watakuambia ni kwa kiasi gani wanakutana na maumivu lakini wanayavumilia ili kupata wanachokitaka? Watu wengi wamekuwa wakiyaona  na kuyatamani mafanikio ambayo watu wengine yamekwisha kuyapata, lakini wanapoambiwa njia ngumu ya kupita ilivyo ngumu, wamekuwa wakirudi nyuma.

Imekuwa kawaida ya mwanadamu kutafuta mafanikio yasiyo na maumivu. Ndiyo maana kila siku watu wanatafuta njia za mkato za kufikia mafanikio. Kwa nini watu wengi wamekuwa wakihangaika na michezo ya bahati nasibu, ni kwa sababu yakutaka kupata kipato kisicho na maumivu.  Lakini wakati wakikwepa hivyo, wameshituka wakipata maumivu njiani. Kwa mfano kwa mtu yoyote ambaye anakwepa kazi kwa sababu ya maumivu, hataweza kupata mafanikio anayostahili kwa sababu hakuna mbadala wa kupata mafanikio yoyote ya kudumu bila kazi. Hii ndiyo sababu kubwa ya watu kuishi maisha ya maumivu wasiyostahili.

Kwa sababu hakuna namna ya kuyakwepa maumivu kabisa, basi ni vizuri kupata maumivu yenye faida. Magurudumu yanapopata maumivu gari linasogea na kufika safari yake. Hakikisha na wewe unapopata maumivu basi safari yako ya mafanikio inasogea na kisha kufika.

Katika maisha yako weka malengo ambayo ndiyo yatakuwa safari yako unayotakiwa ufike. Safari hiyo iwe na matunda ambayo unayaona kwenye fikra zako kisha weka jitihada za kupata matokeo hayo. Hata kama utakuwa unapata maumivu hayo lakini yatakuwa na faida kukupa kile unachokitaka.

Kwenye kila unachokitaka maishani mwako, kumbuka kuwa huwezi kupata kwa kuyakwepa maumivu.  Kwenye kila kitu kizuri unachotaka kuna gharama zake za kulipa, hayo ndiyo maumivu.

Kuwa tayari kufikiri kwa kina nini unaweza kukifanya kwa upekee na kupata matokeo ya pekee. Kuwa tayari kujibana kwa kutotumia fedha zako kwenye anasa ili upate mtaji. Kuwa tayari kuacha au kupunguza starehe ili upate muda wa kutosha wa kujenga biashara yako. Kuwa  tayari kuvumilia pale matokeo yanapochelewa au yanapokuja tofauti na ulivyotarajia. Haya ni baadhi ya maumivu ya faida katika kuelekea kwenye safari yako ya mafanikio.

Je unataka nini maishani mwako? Tathmini gharama au maumivu ambayo utatakiwa kuyakabili kisha vumilia maumivu hayo mpaka upate matokeo. Hakuna njia ya mkato.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu (Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),

Mawasiliano;

Simu; 0752206899/0714301952

Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *