Ulishalia Wakati Wa Kuzaliwa, Usilie Tena Wakati Wa Kufa.
“Ulipokuwa unazaliwa ni wewe pekee uliyekuwa unalia huku wengine wakicheka na kushangilia. Haya yalikuwa ni maandalizi ya wewe kufa ukitabasamu angali wengine wakilia“
Moja ya kitu kimoja ambacho mtoto hufanya wakati wa kuzaliwa ni kulia. Hata pale anashindwa kufanya hivyo kwa hiari hulazimishwa na wakunga kufanya hivyo hata kwa kumsababishia maumivu ili mradi tu alie.
Kuna sababu za kisayansi ambazo unaweza kuwa unazifahamu za kwa nini mtoto anatakiwa alie wakati wa kuzaliwa, moja ikiwa ni kumsaidia kufungua mapafu ili aanze kutumia mfumo wake wa upumuaji. Lakini kitendo hiki kina maana kubwa sana katika maisha ya mwanadamu.
Na wewe unayesoma hapa ulilia wakati unazaliwa huku mama yako, wakunga na watu wengine waliokuwa wamezunguka wakitabasamu. Kucheka na tabasamu la watu waliokuwa wamekuzunguka ilikuwa ni ishara ya kufurahi kwa wewe kuzaliwa kuja duniani kuleta thamani kubwa ambayo dunia imekuwa ikiisubiria.
Kila mwanadamu anayeruhusiwa kuzaliwa hapa duniani amebeba thamani kubwa sana ndani yake. Kama ilivyo kwenye vitu, hakuna kitu kilichopo hapa duniani kisicho na kusudi yaani kazi maalumu, ndivyo ilivyo kwa binadamu; hakuna mwanadamu anayezaliwa bila kuwa na kusudi maalumu hapa duniani.
Tarajio la binadamu ni kuzaliwa na kuishi hapa duniani kwa mafanikio makubwa kisha kufa. Samaki ataishi kwa mafanikio kama atakuwa anaogelea kipindi chote cha uhai wake. Basi litakuwa limeishi kwa mafanikio kama litaweza kubeba na kufikisha abiria katika kipindi chake chote.
Kumbe ili uweze kuishi kwa mafanikio ni lazima utambue na kuliishi kusudi lako kikamilifu.
kulitambua kusudi na kuliishi kikamilifu imekuwa changamoto kubwa kwa watu wengi. Hii imepelekea watu kuishi maisha yoyote. Yaani ni sawa na samaki angeamua kuruka hewani akimuiga ndege, hata kama angejaribu basi ni kwa kiasi kidogo sana. Maisha yake yasingekuwa ya mafanikio kwani uwezo wake wa kuogelea asingekuwa ameutumia vizuri.
Ridhiko kubwa la maisha ya binadamu lipo kwenye kufanikiwa kuliishi kusudi lake kikamilifu. Hapo ni pale anapotumia uwezo wake mkubwa wa kipekee kwa ukubwa wake. Kwa kufanya hivyo anatoa thamani kubwa sana kwa watu wengine. Naomba nikuambie leo siri ya wapi furaha na ridhiko la maisha yako vimejificha. Furaha na ridhiko vimejificha kwenye thamani yako inayowafikia watu wengine.
Fahari yako ya hapa duniani si kulimbikiza utajiri wako benki, si kuwa na mali nyingi ulizolimbikiza bali ni kiasi kile ambacho unawafanya watu wengine wawe na fahari. Unapofanikiwa kufikia hatua hii ndipo ridhiko na furaha vinapoingia katika maisha yako. Ni katika hatua kama hii ndipo unapofanikiwa kufa huku ukitabasamu au ukicheka. Ulizaliwa ukilia kwa sababu ya kazi kubwa uliyokuwa unaiona mbele yako ya kupita milima na mabonde kuhakikisha unaipa dunia thamani inayotegemea kutoka kwako.
Kwa kipindi unachokuwa hapa duniani hakikisha unatumia muda wako vizuri kuipa dunia thamani inayotarajia. Uzuri ni kuwa una nyenzo ndani yako ya uwezo wa kukuwezesha kufanya hivyo. Ndugu kumbuka kuwa dunia haina uchoyo ile thamani unayoipa inakurudishia mara dufu, Tumia vipaji vyako na matamanio mkubwa yanayopiga kelele ndani yako kila wakati kutoa thamani kwa watu wengine.
Hii ndiyo siri ya wewe kutabasamu wakati wa kufa na sio kulia; ishi kusudi lako kikamilifu; wape watu thamani kwa kutumia uwezo wako. Bila ya kufanya hivyo utalia wakati wa kuzaliwa na pia wakati wa kufa.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu (Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz