Hiki Ndiyo Kitu Kidogo Lakini Chenye Matokeo Makubwa.


Categories :

“Ni mpaka pale akili itakapokubali kugeuka na kurudi nyumbani ndipo nayo miguu iliyosahau kiatu nyumbani inavyoweza kurudi kufuata viatu hivyo”

Nimejaribu mambo mengi lakini sipati ninachotarajia! Kwa hatua niliyofikia naona giza tu sijui nianzie wapi? Inafika hatua naona kama dunia inanisaliti! Sijui nifanye nini?

Hizi ni kauli na hali ambazo watu wamekuwa wakizipitia. Inawezekana na huwa unapitia hali hizo na hujui ufanyaje na hivyo unaishia kukata tamaa. Je ni wapi inabidi uanzie katika mazingira kama hayo?

Baada ya mambo kuwa magumu kuna watu ambao wamewatafuta watu wa kuwalaumu wakiamini hao ndiyo waliowasababishia hali hizo . Wapo wengine walioamua kuacha safari waliyoianzisha kama vile biashara na kianzisha nyingine. Wapo wanao kata tamaa na kuona hawawezi tena kuendelea.

Ukitoka nyumba kisha ukafika sehemu ukagundua umesahau kuvaa kiatu kimoja, ni mpaka akili ikubali kurudi nyumbani ndipo na miguu itakapoweza kurudi kufuata kiatu kilichosahaulika.

Ndugu! Kituo kikuu cha mageuzi ya maisha yako kipo akilini mwako. Ni mpaka mtazamo wako ubadilike ndipo unapoweza kubadili vitendo na matokeo yako.

Ni mpaka ubadili fikra kuwa jukumu la kutengeneza maisha yako ya mafanikio ni lako, ndipo unapoweza kuweka kazi kupata matokeo badala ya kumlalamikia mtu kwa kushindwa kwako. Ni mpaka uamini kuwa na wewe unaweza kuwa tajiri, ndipo unapoweza kuweka malengo makubwa ya kukufikisha kwenye utajiri.

Mpaka pale utakapokubali kufanya mabadiliko kwenye vitu visivyoonekana(akili) ndipo unapoweza kuyaona mabadiliko ya viti vinavyonekana.

Winston Churchill “Attitude is a little thing that makes a big difference” ikiwa na tafsiri kuwa mtazamo ni kitu kidogo kinacholeta matokeo makubwa. Kumbe unaweza kuwa hupati matokeo kwa sababu ya kitu kidogo tu kinachoitwa mtazamo.

Mitazamo hujengeka kulingana na mazingira ambayo mtu anakuwa amezungukwa nayo kwa muda mrefu. Unachokisikia, kuona,kuhisi,soma ndivyo vinavyotengeneza mtazamo wako. Kwa mfano kama umezungukwa na watu ambao wao kila siku wanailalamikia serikali kama ndiyo sababu ya maisha yao magumu, ni rahisi sana na wewe kuwa na mtazamo huo.

Lakini unapotambua kuwa matokeo mabaya au madogo unayoyapata ni kwa sababu ya mtazamo ulionaoa na kisha kubadilika, ndipo unapoweza kushudia matokeo makubwa sana. Kwa mfano kama una tabia ya kutumia kila fedha unayoipata bila ya kuweka akiba na baadaye ukaona kufanya hivyo si kufaidi fedha yako bali kuhatarisha maisha yako ya kifedha ya baadaye, kuna faida kubwa sana utaanza kuipata. Baada ya kubadili tu mtazamo huo, utaanza kukusanya fedha ambazo baadaye unaweza kuziwekeza na zikazalisha zaidi.

Njia kuu ya kubadili mtazamo ni kupata maarifa mapya. Moja ya sehemu ambayo unaweza kupata maarifa ya maana ni vitabu. Kusoma vitabu kutakusaidia sana kuchuja mtazamo wako. Vitabu vitakupa ni kipi watu wengine walikiwaza wakapa matokeo ambayo hata kwako ni bora pia.

Chukua hatua; Tafakari jambo ulilokwama na huoni mweleke mbele yake. Je ni kipato? Mahusiano? Ajira? Sehemu pekee ya kubadili uelekeo wa jambo hili ni akilini, badili kwanza mtazamo ndipo na mambo mengine yatakapobadilika.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *