Bahari Haijawahi Kuishiwa Samaki Lakini Si Rahisi Kuwaona Samaki Hao Jangwani
Wavuvi wamekuwa wakiwavua samaki miaka nenda rudi huku samaki hao wakiliwa na binadamu kila siku lakini hujawahi kusikia bahari hiyo imeishiwa samaki. Kuna wavuvi wameanza kuvua samaki hao tangu ujanani mpaka sasa ni wazee bila ya kuacha kazi hiyo kwani kila siku wanapata samaki. Kadhalika hata kama shamba litachomwa moto na kila mmea uliokuwepo ndani yake ukateketea, mvua ikinyesha tu shamba huotesha tena majani, vichaka na baadaye msitu kabisa.
Hii ni ishara kubwa sana kwa maisha ya binadamu kwani kuna jambo kubwa sana ambalo ukijifunza kwenye mifano hii litabadili mtazamo wako na kisha maisha yako. Jambo unaloweza kujifunza kwenye mifano hii miwili hapo juu ni kuwa dunia ina utele, yaani huwa haiishiwi kitu. Kila kitu hapa duniani kipo kwa wingi sana kiasi kila mwanadamu anaweza kukipata kwa kiasi kikubwa anachokitaka, akakitumia na baadaye kukiacha baada ya kufa.
Lakini hali imekuwa tofauti kwa watu wengi sana hapa duniani. Watu wamefikiri dunia ina uhaba, wakiamini kuwa kuna watu tayari walishavishikilia vitu na hivyo watu wengine hawawezi kuvipata au wataishia kugawana vichache vilivyobakia. Watu huamini kuwa kama ni fedha basi zipo chache sana na zimeshashikiliwa na watu wachache na wao hawawezi kuzipata tena fedha hizo.
Kwa kuambiwa na kuamini hivyo umeipangia akili yako kuwa inaweza kupata kiasi fulani kidogo tu cha mafanikio. Na kwa sababu chochote ambacho akili yako inakipokea na kukiamini kinakuwa chako, ndiyo maana umeyapata mafanikio hayo madogo. Umeendelea kung’ang’ania kiasi hicho kwa sababu ya kuamini huwezi kuongeza tena kwani vitu ambavyo vingekuletea utajiri ni vichache na tayari vimeshachukuliwa.
Kwa sababu ya akili yako kuamini kwenye uhaba, hujaweza kuoana kama kuna biashara nyingine unayoweza kufanya zaidi ya ile ya jirani yako. Ulipoziona biashara nyingi zinaendelea, akili yako ikajiaminisha kuwa biashara zote zitakuwa zimeshachukuliwa. Kwa kuamini hivyo uliweka mipaka kwenye akili yako ya kuwa huwezi kubuni biashara mpya. Hii ndiyo sababu iliyokufanya kuiga biashara ya jirani na si kubuni ya kwako ambayo ingekupa mafanikio makubwa zaidi.
Ulipoona watu wakifanya vitu vikubwa na vya kipekee, ukaamini kuwa watu kama hao ni wachache duniani, wameshatokea na wewe huwezi kuwa miongoni mwao. Ulipoamini kuwa wewe sio wa pekee ukajipa ukawaida, umefanya vitu vya kawaida na umekuwa wa kawaida kweli. Kwa kujiona wa kawaida hujahangaika kujua upekee wako, kusudi lako maalumu hapa duniani na kipaji cha pekee ulichonacho ndani yako. Licha ya vitu hivi kuwa vya pekee lakini kila mtu anavyo ndani yake, kwa hiyo kama kuna watu wanaviishi, hawajamaliza kwani vyako bado vipo ndani yako.
Ndugu! Ni wakati sasa wa akili yako kuhama kutoka kwenye boksi la uhaba lenye mipaka na kuhamia kwenye boksi la utele lisilo na mipaka na kuona kila kitu unaweza kukipata kwa kiasi chochote ukitakacho. Kuendelea kuiacha akili yako kwenye boksi la uhaba ni sawa na kukazana kutafuata samaki jangwani. Licha ya bahari kuwa na samaki tele, ni vigumu kuwavua jangwani kwani sio eneo sahihi la samaki hao kupatikana. Hivyo ili uweze kunufaika na utele wa dunia hii ni lazima akili yako ibadilike, ikaribishe maji na samaki tele waendelee kuzaliana humo na kukuruhusu wewe kuvua kiasi ukitakacho.
Tafakari sasa ni vitu gani umekuwa ukiamini vina uhaba na kukusababishia kufika hapo ulipo? Je ni fedha au mali? au makusudi na vipaji? Tambua sasa kuna utele hivyo rekebisha mtazamo wako na weka mipango ya kuanza kupata kiasi ukitakacho.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952
Email: alfred@amshauwezo.co.tz