Ulizaliwa na zawadi, je umeshaipa dunia?
Mbegu za matunda zikishamea zinakua na kuwa miti inayotoa matunda na hii inakuwa zawadi kwa dunia. Nyuki walikuja duniani walijua zawadi waliyoibeba wakaanza kutafuta inta za maua na kutengeneza asali ambayo inapendwa sana na watu kwa utamu wake. Kadhalika jua lilipogundua lililochobeba limekuwa likiwaka kila siku kuipa dunia nguvu na mwanga.
Kama ilivyo kwa mbegu, nyuki na jua, kila mwanadamu amekuja hapa duniani akiwa na zawadi ya kipekee ya kuipa dunia. Ni zawadi ambayo mwanadamu anakuwa ameibeba ndani yake tangu kuzaliwa kwake.
Zawadi yako kwa dunia si matunda kama ilivyo kwa mbegu za matunda, asali kwa nyuki au nguvu na mwanga kwa jua. Zawadi uliyoibeba ni thamani ambayo unaweza kutoa kwa watu wengine.
Kitu gani unaweza kuwapa watu wengine maisha yao yakaboreka? Je ni huduma gani ya kipekee ambayo watu wanaweza kuipata kwako tu? Je ni bidhaa gani ambayo dunia imeisubiria siku nyingi na wewe utaigundua? Kitu hicho ni zawadi kwa dunia na inasubiria.
Zawadi uliyozaliwa nayo ni ya kipekee sana kiasi cha kutopatikana kwa mtu mwingine yoyote. Hii inamaanisha kuwa kama hujaanza kuitoa zawadi hiyo dunia inahisi kupungukiwa. Kuna eneo hapa duniani halijaimarika kwa sababu wewe hujaanza kuitoa zawadi hiyo.
Kuna watu wamekosa maarifa sahihi kwa sababu wewe bado hujaiandikia kitabu.
Miti ya matunda huwa haitoki porini kumfuata mlaji, bali mlaji ndiyo hufuata matunda yaliko. Nyuki huwa hawatoi matangazo kuwa sasa asali ipo tayari ili mlinaji aende, bali mlinaji huenda polini kuwatafuta nyuki na asali yake. Kadhalika ndivyo inavyokuwa unapoanza kutoa zawadi uliyonayo kwa dunia, watu watakufuata uliko kwa sababu thamani uliyonayo na uadimu wa zawadi hiyo.
Ndugu! Muda pekee ambao umepewa kuiipa dunia zawadi yako uliyozaliwa nayo ni kipindi cha uhai wako. Huu ni muda wa kuhakikisha dunia inafaidika na zawadi yako. Bahati mbaya huwezi kumridhisha mtu mwingine, hivyo ukifa bila kuitumia utaondoka nayo. Hili litakuwa na janga.
Licha ya wewe kutoitoa zawadi yako kwa dunia, utakuwa unatumia zawadi za watu wengine. Unaona maisha yako yakaboreka ni kwa sababu watu wengine wamefanikiwa kutoa zawadi zao. Ni wakati muafaka na wewe sasa kuitoa zawadi yako.
Masikitiko makubwa ya mtu wakati anakufa yatakuwa kufa anagali zawadi aliyozaliwa nayo hajaitoa. Hatasikitika kwa sababu ya fedha anazoziacha benki au mali anazoziacha kwa sababu atajua hivyo vyote vitaweza kutumiwa na watu wengine wakati zawadi yake ya kipekee akifa nayo.
Kwa sababu bado upo hai, una nafasi ya kuitoa zawadi hiyo kabla hujafa. Umebeba nini ndani yako? Kaa chini na tafakari na usikilize moyo wako utakuambia zawadi uliyozaliwa nayo kisha anza kuipa dunia mara moja kabla hujaondoka.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz