Mambo mawili ya uhakika kwako. Na moja limeshatimia!


Categories :

Kuna matokeo katika maisha yako unayoweza kuwa huna uhakika kama yatatokea au la! Katika haya inakupasa usubiri muda uamue kujiridhisha kwako.

Katika maisha yako una mambo mawili ambayo una uhakika nayo. Haya huhitaji kujadili na mtu kwa sababu unatambua kabisa yatatokea. Kama hayaji kwenye fikra zako, ni kwa sababu tu huyapi muda wa kuyafikiria. Mambo hayo ni KUZALIWA na KUFA. Katika haya huhitaji kuuliza kwa mtu kwani ukitafakari tu unajua ni suala la muda tu kwayo kutimia.

Kati ya hayo mambo moja limeshakamilika nalo ni kuzaliwa. Kuzaliwa ulikuwa ni mwanzo wa maisha yako hapa dunia. Kwa hiyo kama upo hapa duniani tambua hilo limeshakamikika. Oh ! Kumbe limebaki moja tu kati ya mawili!.

Kumbe unachokisubiri sasa ni kifo. Una uhakika kuwa utakufa hata hivyo kuna fumbo kubwa sana kwenye kifo chako. Hata kama una uhakika kuwa utakufa lakini hujui ni lini. Kumbe hii ni taa ya tahadhari ambayo inabidi iwe inawaka mbele yako kukupa tahadhari.

Kama hujui kitu fulani kitafanyika lini, basi kuna uwezekani wa kutokea hata muda mfupi ujao ikiwa na pamoja na leo na hata sasa. Kumbe jambo la kufa kwako linaweza kutokea hata leo. Hivyo hii taa iwake na kukukumbusha yafutayo;

Fanya kazi uliyoletewa; kila kinachokuja duniani kina sababu maalumu yaani kazi maalumu. Kumbuka hata gari, samani, vyombo vinavyotengenezwa na binadamu vina kazi maalumu. Kadhalika wewe uliyepewa kuvimiliki vitu vyote una kazi maalumu. Hili ni kusudi la maisha yako. Nini kinakusukuma toka ndani mwako ukifanye katika uhai wa maisha yako? Sikiliza moyo wako. Ulizaliwa, na kama bado hujafa una nafasi ya kuishi kusudi lako.

*Tumia muda wako vizuri; Hujafa kwa sababu bado una muda wa kuendelea kuishi. Uhakika wa pili ukitimia huwezi tena kufanya chochote. Muda huu wa kusubiria hakika ya pili ni dhahabu kwako, utumie kufanya mambo yenye umuhimu kwako na mchango kwa jamii ili hata baada ya hakika ya pili kutimia utaendelea kukumbukwa. Tumia muda huu kuishi kusudi lako, ndoto yako; kwa kupanga malengo na kuweka nidhamu ya kuyatimiza.

Tumia nafasi yako vizuri; Nani anatarajia nini kutoka kwako? Je wewe ni kiongozi na watu wana matarajio kwako? Je matarajio hayo watayapata kabla ya hakika ya pili haijatimia? Je wewe ni mzazi na watoto wanatarajia makubwa kutoka kwako? Nini watakikumbuka kutoka kwako baada ya hakika ya pili kutimia? Je wewe ni mfanyabiashara na wateja wana matarajio makubwa ya thamani ya bidhaa au huduma kutoka kwako?

Hakuna cha ziada baa ya hakika ya pili; Muda pekee wa kufanya yote unayotarajiwa hapa duniani upo katikati ya halika hizo mbili yaani kuzaliwa kwako na kufa kwako. Hakikisha unaitumia vizuri kila sekunde kutenda jema na lenye thamani. Hapo ndipo utakuwa umaefanikiwa kubadilisha muda wako kwa dhahabu.

Kama umeweza kusoma makala hii mpaka hapo ni uthibitisho kuwa bado upo hai ukingojea hakika ya pili. Hii ni nafsi ya pekee kuanza kuishi maisha yako badala ya kuiga, kuanza kufanya leo uliyoyapanga siku nyingi badala ya kuendelea kuahirisha. Tanguliza upendo kwenye kila jambo kwani ndiyo njia ya kupeleka thamani kwa watu wengine.

Nakutakia kila kheri katika kuishi kikamilifu unapoisubiri hakika ya pili.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *