Hivi Ndiyo Vichocheo Vya Kukusukuma Kufanya Magumu Yenye Matokeo Makubwa.
_ “Vifaranga hushuhudia upendo wa kweli kutoka kwa mama yao pale atakapokuwa anahangaika na kupigana na mwewe kuokoa maisha yao”
Mafanikio hasa makubwa ni safari ndefu na ngumu, yenye maumivu makali ya kutokwa machozi na damu. Hii imekuwa miongoni mwa sababu kuu za kwa nini mtu anaamua kuchagua njia rahisi na kuwa mtu wa kawaida.
Kwa nini nijitese kiasi hicho? Si nitaishi tu hata kama kipato cha kawaida? Maisha siyo magumu hivyo! Haya ni maswali na kauli ambazo unaweza kujiambia, ukajiuliza na kujijibu na kujifariji kisha ukaishi. Lakini pia maswali kama haya na mtazamo huo huja baada ya ile njia yako sahihi ya kupita kufikia mafanikio makubwa kuonekana ngumu na ndefu hivyo kuamua kujitoroka mwenyewe.
Mara nyingi njia sahihi za kupita hufahamika kwa watu wengi, na wengine hujaribu kabisa. Lakini baada ya kuonja au kuona maumivu anayotakiwa kuyapitia huacha njia hiyo na kutafuta mbadala ulio rahisi.
Mtu anapofikia hatua kama hii anakuwa amekosa KWA NINI kubwa ndani yake lakini na kiungo muhimu sana cha kuiishi kwa nini hiyo; ambacho NI UPENDO.
Sababu ya KWA NINI ufanye hayo yote magumu na yanayochukua muda mrefu lazima iwe kubwa na yenye imani ya mvuto kuliko sababu ya kutojitesa. Ni vigumu sana kufikiria kujitesa kuongeza kipato kama umeridhika na kile unachokipata. Ni vigumu sana kujitesa kuongeza maarifa kwa kusoma vitabu kama mtazamo wako na matokeo unayoyapata havikuudhi. Kwa nini ujitese?
Lakini kwa nini pekeyake haiwezi kufanya kazi bila kuunganisha na kiungo kingine muhimu. Kuku kuishia kufikiri tu kwa nini vifaranga vyake vipotee kwa sababu yeye yupo inaweza isimshawishi kuchukua hatua za maumivu za kukabiliana na mwewe asipokuwa na upendo kwa wanawe. Kwa nini yako lazima iambatane na UPENDO kwako na dunia yaani jamii inayokuzunguka. Bila kuwa na upendo hutaona sababu ya kujitesa wakati unaweza kuwa wa kawaida na kuishi kawaida.
Kuku kukubali kupigana na mwewe hata kujeruhiwa ni kwa sababu ya kwa nini kubwa aliyonayo ndani yake. Hujiuliza kwa nini watoto wake waangamie wakati yeye yupo kwa ajili yao. Hii ni kutambua kusudi lake. Lakini pia huviangalia vifaranga vyake na kuwaonea huruma kwa udogo wao na kuamua kupata maumivu kwa ajili yao. Huu no upendo.
Kitu gani unakiona dunia inateseka ingali wewe una uwezo wa kukifanya na kuondoa maumivu hayo? Huduma gani unaweza ukaifanya hata kama kwa ugumu lakini watu wakanufaika? Je uongozi gani upo tayari kuuchukua hata kama una hatari ili kuwafikisha watu kwenye mwanga na wakaona njia wa kwendea? Ipi ni kwa nini yako inayoweza kuushinda ugumu na hatari zake?
Tazama kundi kubwa linaloweza kunufaika na kuifanya KWA NINI YAKO, waonee huruma, wathamini na wapende. Piga picha ya matokeo ya mateso yako. Matokeo hayo yatakupa ridhiko la moyo wako kwa thamani utakayokuwa umeitoa kwa wengine. Huku ni kujipenda mwenyewe. Lakini pata picha ya watu wengi watakaonufaika na mateso na ugumu ulioamua kuubeba. Zaidi ya hayo hapo ndipo watu hao watakapokuwa tayari kukulipa kwa sababu ya thamani uliyowapa na hii ndiyo njia ya kujipatia utajiri.
Tafakari kitu ambacho upo tayari kukifanya kwa ukuu wake bila ya kujali maumivu na hatari zake Kifanye hicho maishani yako yote. Hapo ndipo utakuwa umefanikiwa kuipa dunia thamani kubwa sana na yenyewe kukurejeshea utajiri na ridhiko la moyo wako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz