Hivi Ndivyo Namba 6 Yako Inavyoweza Kugeuzwa Namba 9.


Categories :

” Ukiichunguza vizuri namba sita(6) utaona uwezekano wa kuigeuza kuwa namba tisa (9)”
Kuna hali ambazo umekutana nazo na ukaona hapo hakuna unachoweza kukibadili. Yaani umenyoosha mikononi na kukubaliana na matokeo.

Kwenye hali yoyote ile huwezi kupata matokeo ya utofauti kama hutafanya kwa utofauti. Moja ya sababu ambazo huwa zinakufanya ushindwe kubadili matokeo ni kutoichunguza kiundani hali unayoipitia na kuiona njia ya kubadili matokeo. Katika mazingira kama hayo unahitaji muda na umakini kutambua njia ya kujikwamua.

Ukiichunguza vizuri namba 6 utatambua kuwa unaweza kuizungusha kwa nyuzi 180 na ikwa 9 ambayo ina thamani kubwa kuliko 6. Hivyo kabla ya kuchua uamuzi wa kukata tamaa, kuna nafasi ya kuizungusha hali uliyonayo ikakupa unafuu na thamani zaidi.

Zungusha 6 ya hali ngumu ya maisha. Hali ngumu ya maisha umekuwa wimbo wa watu wengi. Mradi tu bado anaishai mtu anaweza kuaanza kuuimba wimbo huu ujanani mwake mpaka uzeeni. Maisha magumu ni namba 6 je unaigeuzaje kuwa 9 inayoweza kulainisha ugumu huo. Tumia ugumu huo kuwa na namba tisa kuwa kujenga hasira ya kutoka kwenye hali ngumu.

Anza kujiuliza kwa nini nateseka na hali hii. Hii itatengeneza KWA NINI kubwa ndani yako kisha kuamsha uwezo wako ndani yako wa kufanya mabadiliko.

Zungusha 6 ya muda unaoupoteza. Matokeo unayoyapata ni kwa sababu ya matumizi yako ya muda. Kila mtu ana masaa 24 katika siku, je wewe unayatumia wapi. Je muda mwingi unatumia kwenye mitandao ya kijamii, kuwaongelea watu wengine, au starehe? Matumizi haya ni 6 ambayo unaweza kuizungusha kuwa 9 kwa kuupangilia muda wako kwenye vitu vyenye mchango makubwa kwenye mafanikio yako kama kupata maarifa sahihi, kusaka wateja, kuboresha utendaji wako wa kazi nk.

Zungusha 6 ya kipato kidogo. Kipato chako ni zao la thamani unayowapa watu wengine. Kama kipato chako cha sasa ni kidogo na hakikuridhishi basi tambua kuwa utatakiwa kuongeza thamani. Unahitji kuigeuza 6 hii na kuwa 9 kwa kuongeza ubora zaidi kwenye kazi au biashara unayoifanya, kuongeza mifereji ya kipato nk

Zungusha 6 ya faida ndogo. Faida ni ndogo kimekuwa kilio cha wafanyabiashara wengi na kuwa chanzo cha biashara nyingi kufa. Ili uweze kukabiliana na hali hii huna budi kuchunguza vizuri ni kwa namna gani unaweza kuibadili 6 ya faida ndogo na kuwa 9 kwa kuongeza faida. Kwanza angalia mauzo yako, yanatosha kukupa faida kubwa? Weka mpango wa kuongeza mauzo zaidi kwa kuwatembelea wateja zaidi
Pili angalia matumizi ya uendeshaji wa biashara yako, je unaweza kutengeneza 9 kwa kupunguza matumizi ysiyo lazima?

Zungusha 6 ya vipaombele vyako. Ni kweli upo busy sana lakini hupigi hatua kubwa, ni wakati sasa wa kugeuza namba ya 6 ya vipaombele vyako. Angalia kila jambo unalolifanya, ni kwa kiasi gani linachangia kwenye matokeo, kama vile kipato uchopata. Baada ya kujua mlinganisho huo, weka nguvu, umakini na muda wako kwenye yale yenye mchango mkubwa huku mengine ukiwaachia watu wengine wafanye kwa niaba yako.

Ndugu! Kwenye kila hali usiyoridhika nayo sasa, kuna uwezekano wa kufanya mabadiliko fulani na kupata matokeo yenye thamani zaidi. Tafakari ni kwa namna gani unaweza kuizungusha 6 hiyo kuwa 9, utapata jibu. Badala ya kulalamika na kukata tamaa wewe zungusha 6 kuwa 9.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *