Hiki Ndicho Chenye Nguvu Kubwa Ya Kukutenganisha Na Usingizi Wako Wa Asubuhi.


Categories :

Moja ya kitu kizuri na kitamu katika maisha ya mwanadamu ni usingizi. Miongoni mwa nguvu kubwa ambazo humvuta binadamu ni usingizi. Ndiyo maana imekuwa si rahisi kwa watu wengi kuamka asubuhi na mapema licha umuhimu wake mkubwa kuwa bayana.

Lakini ikitokea mtu anaenda kulala huku akitambua kuwa kesho ana safari muhimu, nzuri na tamu aliyoiota na kuisubiri kwa siku nyingi, usingizi wa siku hiyo huwa anakuwa hauna thamani tena kama siku nyingine. Hata akipata, usingizi wake huwa wa kushituka shituka sana kwani hutamani usiku ule uishe haraka ,kuche na aianze safari yake.

Mbele ya maisha yako lazima kuwe na kitu kikubwa ambacho una shauku nacho kubwa sana ya kukipata bila kujali muda utakaotakiwa kukipata. Hiki ndicho kinatakiwa kuwa na thamani kubwa kuliko usingizi wako. Hiki ndicho kitakachovunja nguvu kubwa ya usingizi inayokuvuta asubuhi kuendelea kulala na hivyo kukufanya uamuke mapema na kwenda kukitafuta kitu hicho. Hii ni ndoto halisi ya maisha yako.

Hii ni tofauti na ndoto unayoiota usiku kisha unaamka asubuhi ukiwa umeshasahau kile ulichokiota usiku. Hii ni ndoto unayoiota kila dakika ya maisha yako. Hiki ni kitu unachotaka ukikamilishe kipindi cha uhai. Hii ni alama kubwa ambayo unataka iendelee kuishi hapa duniani hata kama wewe utakuwa umeondoka.

Ndoto hii inaanzia ndani yako kutokana na kile kitu unachokipenda sana kukifanya. Umuhimu wa ndoto yako kuanzia ndani yako ni kuwa; kwanza itakuwa imeunganishwa na upekee wa uwezo na hivyo itakuwa rahisi kuziamsha nguvu hizo na kukuwezesha kuitimiza ndoto hiyo. Pili ndoto hiyo ikianzia ndani, itakuwa rahisi kuhamasisha na kustahimili kuendelea kupambana pale magumu yatakapokukuta. Hii ni kwa sababu kila wakati moyo wako na akili yako vitaendelea kuamini kuwa unachokipambania utakipata.

Kaa chini kisha tafakari huku ukijiuliza ndani yako, ni kitu gani kipo tayari kuahirisha usingizi wako? Picha gani huwa unaiona ikitokea maishani mwako lakini unaipuuzia kwa kuona hilo ni jambo ambalo haliwezekani kwako? Sauti gani ya ndani huwa inakujia ya kutaka ufanye na kukipata kitu fulani lakini huwa unaipuzia? Huko ndiko kusudi na ndoto yako vinakopatikana.

Ndugu! Kitu kinachokukatisha usingizi wako ili ukiwaze na kisha kuamka na kwenda kukifanya ndicho kilichobeba thamani yako kubwa ya maisha yako hapa duniani. Hiki ndicho kilichobeba utajiri wako. Hiki ndicho kimebeba thamani yako kwa watu wengine. Hichi ndicho kimebeba umaarufu wako.

Wakati umefika sasa wa kuitengeneza ndoto hii kamili ili itawale akili yako na iweze kukuamsha asubuhi na mapema. Ikupe mwelekeo wa maisha yako ili usihangaike na vingine ambavyo vingi vimekuwa siyo vyako. Si hivyo tu lakini pia ikupe hamasa ya kuendelea kustahimili magumu yatakayokupata. Huu ndiyo msingi wa utajiri wako.

Usijipunje kwenye kutengeneza ndoto hii. Ndoto yako lazima iwe kubwa kwani wewe pia ni mkubwa ukiangalia uwezo wako uliopo ndani. Pia ndoto ndogo itakosa nguvu ya kukutenganisha na usingizi wako mtamu. Ndoto yako ni ipi? Itengeneze leo kisha anza kuiishi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *