Ni Hiki Tu Kinachosubiriwa Kutoka Kwako Ili Uwe Maarufu.


Categories :

Moja ya mahitaji au tamaa ya bindamu kuwepo hapa duniani ni kuwa maarufu. Kuwa maarufu ni kupewa utambulisho wa kipekee kwa jambo la pekee ambalo lina matokeo ya upekee.

Kwa sababu ya huu umaarufu kutopatikana kirahisi, wapo walioamua kufanya vitu vya hovyo kama kutembea uchi, ubakaji, kufanya usanii uliotofauti na tamaduni nk. Lakini maarufu huu huwa haudumu.

Lakini upo umaarufu mzuri ambao hudumu na hupokewa chanya na jamii lakini pia kukupa ridhiko moyoni mwako. Umaarufu huu ni wa kuwa na mchango wa pekee kwenye jamii. Huu ndiyo nitaenda kuuongelea hapa ili uujenge.

Umaarufu huu chanya huhitaji muda mrefu sana kuujenga na kutambulika. Huu ni umaarufu utakaotokana na kujenga himaya yaani kuwa mbobezi kwa kufanya vitu kwa kiwango vikubwa sana. Utakapofanya vitu kwa kiwango kikubwa sana tofauti na wengine wanaofanya kitu hichohicho, ndipo macho ya wengi yatakapokuona wewe tu. Kitu pekee kinachosubiriwa kwa ajili ya wewe kuwa maarufu wako ni kuanza.

Watu wengi wanatamani kuwa maarufu bila ya kuujenga umaarufu kwanza. Huwezi ukaanzia kileleni kuupanda mlima wowote ule. Unahitaji kuanzia kwenye msingi wa mlima huo. Licha kutamani kuwa maarufu kwa siku nyingi lakini hujaanza kuutengeneza umaarufuu huo.

Tumeona hakuna umaarufu chanya bila ya kuwa na thamani ya pekee. Hivyo kitu cha kwanza unachotakiwa kuanza nacho ni kujenga thamani ya pekee. Thamani ya pekee utaijenga kwa kuishi upekee wako. Umezaliwa na upekee ndani yako, yaani nguvu za kipekee za kufanya kitu kwa viwango vya juu sana ambavyo hata kama kuna mtu mwingine akiamua kufanya hawezi kukufikia.

Huwezi kuweka taa iliyowashwa juu ya kilima halafu usiangaze. Huwezi kufunika moshi wa wa mto unaoendelea kuwaka halafu usifuke. Fikiria tena mifano hii miwili; Unapotambua na kuuishi upekee wako kwa ukamilifu utafananishwa na taa iliyowashwa na kuendelea kuwaka kisha kuwekwa kwenye kilele cha mlima. Kila mtu ataweza kuiona tu; huu ndiyo umaarufu wako.

Anza kwa kujiuliza unaona nini ndani yako umachoweza kukifanya kwa uwezo mkubwa sana na kupata matokeo ya tofauti sana na watu wengine. Kutambua upekee, mara nyingine inakulazimu kujaribu vitu vingi mwanzoni. Jaribu vitu vingi huku ukiusikiliza moyo wako na kuangalia matokea unayoyapata.

Ukishajua upekee wako ndipo safari ya kuujenga inapoanzia. Umaarufu wako utaanza kujengwa kwa kutengeneza ndoto yako kubwa, narudia tena, ndoto kubwa. Hakuna umaarufu wa kudumu unaojengwa kwa ndoto ndogo. Watu wengi wamefanikiwa kuishi ndoto ndogo na ndiyo maana hawajaweza kuwa maarufu.

Ndoto kubwa ni ile ambayo inaanza kukushitua hata wewe mwenyewe. Lakini kwa kuendelea kuangalia ile nguvu kubwa uliyonayo unajenga imani kuwa utaitimiza. Ndoto yako kubwa huzidi kuleta taharuki pale inapotoka nje. Ndoto yako kubwa itawashitua watu wengi na wengine kukuona umechanganyikiwa. Ukiona kila mtu anakubali kuwa unaweza kuitimiza ndoto yako, rudi kajipange tena. Hiyo ni ndoto ndogo; rudi chumbani katengeneze nyingine.

Ndugu! Umeshajua umaarufu wako unakoanzia kutengenezwa. Lakini pia una mtaji wa kwanza ndani yako wa kutengeneza umaarufu wako wa kipekee; huu ni uwezo wako wa kipekee. Umaarufu wako upo mbele yako, itengeneze ndoto yako na kuanza kuishi kwa viwango vya juu. Hii itakuwa sawa na kuweka kuweka taa juu ya mlima na kuzidi kuongeza mwanga wake kila wakati. Utaongeza mwanga kwa kuongeza thamani ya pekee unayowapa watu kila siku.

Una uwezo wa kuwa maarufu huku ukiwapa watu thamani kubwa kwa kuitengeneza ndoto yako kubwa na kuiishi kikamilifu. Unachosubiriwa ni kuanza, na siku nzuri ya kuanza ni leo. Nakutakia kila la kheri.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *