Hiki Ndicho Kitakachokupandisha Kileleni Mwa Mafanikio Yako Kwa Haraka.
Kitakachomfanya mtoto awahi kutembea ni kasi ile ya kujaribu kutembea licha ya maumivu anayoyapata kila anapoanguka.
Kitakachomfanya mtu ajue haraka kuendesha baiskeli ni kujaribu kuning’iniza miguu juu ya baiskeli licha ya kujua kuna nfasi ya kuanguka na kuchubuka.
Kuna kitu kimoja ambacho huwezi ukakiepuka kama unataka kujua kitu, nacho ni kuthubutu au kujaribu. Huwezi kupata matokeo bila ya kuanza kufanya hata kama hujawahi kufanya. Huwezi kuwa mzoefu bila ya kupitia kujaribu kwanza. Huwezi kufanya makubwa bila kujaribu.
Kuthubutu au kujaribu ni kuchukua hatari ikiwa ina maana unafanya kitu ambacho huna uhakika nacho. Unapofanya kitu ambacho huna uhakika nacho unakuwa huna uhakika wa kupata matokeo mazuri. Hiki ndicho kinachowafanya watu wasijaribu kwani wengi wanapenda vitu ambavyo wana uhakika karikubia 100% wa kupata matokeo.
Licha ya kukukosesha matokeo chanya, kujaribu huweza kukupa matokeo hasi kama vile kupata hasara, maumivu ya hisia, kukosolewa nk. Licha ya maumivu ambayo kujaribu kunaweza kusababisha, lakini ndicho kitu pekee kinachoweza kumpandisha mtu juu zaidi ikiwaacha watu wengi chini wanaoteseka kufanya vitu ambavyo tayari wana uhakikia navyo.
Ndugu! umekuwa hupigi hatua au unapiga hatua ndogo kwa sababu ya kutokuwa tayari kujaribu. Hii ndiyo hofu iliyokukwamisha kufanya mambo makubwa licha ya kuwa na uwezo huo wa kufanya miujiza ndani yako. Umekuwa ukiweka mipango mingi mikubwa lakini muda wa utekelezaji ukifika, unasita kwa ajili ya hofu ya kujaribu.
Una haki ya kutengeneza ndoto kubwa lakini kwa sababu ya hofu, umekuwa ukitengeneza ndoto ndogo ambazo unaona hazina usumbufu wa kuzikamilisha. Hii ndiyo sababu ya wewe kuwa mtu wa kawaida.
Mpira wenye upepo utabakia tu ardhini mpaka pale utakapokubali kudundishwa, ndipo utakaporuka juu kadri ya kiasi cha kudundishwa utakachokubali. Kiasi cha mafanikio utakayoyapata kitategemea sana kiasi cha hatari utachokuwa tayari kuchukua kwa kujaribu.
Watu waliofanikiwa kufanya mambo makubwa hapa duniani, walikuwa tayari kuchukua hatari kubwa ambazo wengi walizikwepa. Walikubali kuanzisha biashara ambazo wengi waliona kuna hatari ya kupoteza fedha nyingi. Walichukua hatari ya kwenda ambako hakuna aliyewahi kufika.
Ni kwa kuchukua hatari ndipo unapoweza kupanda juu sana ambako hakuna watu au wapo wachache na kupunguza ushindani. Ni kwa kuchukua hatari ndipo unapoweza kufika mbali sana ambako kuna utajiri usio na ushindani mkubwa.
Umekuwa ukipata matokeo hayohayo kila siku ambayo hayakuridhishi kwa sababu ya kutojaribu vitu vingine vikubwa zaidi. Ni wakati sasa wa kuweka malengo makubwa kuliko ambayo umekuwa ukiyaweka na kuwa huru kuyapata. Chukua hatari sasa ya kuanzisha biashara ya ndoto yako hata kwa kuanza kidogo kidogo. Kumbuka, ni kwa njia ya kuchukua hatari hizi ndipo unapoweza kwenda kileleni.
Siri kuu ya kufika kilele kwa haraka cha mafanikio yako ni kujaribu na kujifunza kwa haraka. Kumbuka hakuna mafanikio makubwa yasiyokutana na kushindwa kwa sababu tofauti tofauti. Hivyo kama unataka kupata mafanikio haraka huna budi kuweka malengo yako makubwa, chukua hatari, kukosea, kujifunze na kusonga mbele kwa haraka.
Kuendelea kuendelea kuogopa kujaribu na kuchukua hatari kubwa ni kuchelewesha mafanikio yako makubwa ya kukupandisha kileleni. Kumbuka leo, ni jambo gani kubwa umekuwa ukilitamani kulifanya lakini kila ukilifikiri hofu ya hatari iliyopo inakuogofya? Wakati umefika sasa wa kuvaa ujasiri na kulifanya, utaanguka lakini kuna nafasi ya kuinuka. Utakutana na maumivu lakini una uwezo wa kuvumilia na yataisha.
Inuka sasa, chukua hatari kubwa, kosea, jifunze kisha paa kileleni.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz