Hii Ndiyo Njia Pekee Ya Kufaidi Maumivu Unayoyapitia.


Categories :

“Licha ya mzizi wa mti kubanwa na mawe, huacha kusikilizia maumivu na badala yake huhangaika na kupenya kwenye mawe hayo ili kukua kuyafikia maji na chakula”

Kuna kitu kimoja ambacho ni cha uhakika ukiwepo hapa duniani, nacho ni maumivu. Duniani kuna miba, milima, mabonde, jua, mvua ambavyo utakutananavyo kwenye safari yako ya maisha. Bahati mbaya ni kuwa hata pale unaposema huhitaji mafanikio, bado utaendelea kufikiwa na maumivu hayo.

Kwa mfano unaposema wewe hutaki kujitesa kupata utajiri, bado kuna maumivu utayapata kwa kukosa fedha za kutosha za kukuweka huru. Hata pale utakaposema utaishi ndoto ndogo ili kuwa huru, bado utakutana na changamoto za kutosha zenye maumivu wakati wa kutimiza ndoto zako ndogo.

Huwezi kukwepa maumivu kwani ni sehemu ya maisha. Njia pekee ya kufaidi maumivu hayo si kuasikilizia bali kujifunza na kukua. Unapopitia changamoto na kukupa maumivu usibakie unalia na kulalamika, bali ona cha kujifunza kisha, songa mbele.

Mbona ukikanyaga mwiba huwa huendelei kuuacha mguu hapo hapo, lakini badala yake hunyanyua mguu kisha kuutoa mguu wako kwenye mwiba! Je umeshawahi kumuona mtu akikanyaga mwiba anauacha mguu hapohapo kisha kuanza kuulizia au kutafuta nani aliyeweka miba kwenye njia hiyo ili amulaumu? Haya huwa hayatokei, bali mtu akishatoa mguu kwenye mwiba hujitahidi kutokupita hapo anaporudi au huuondoa mwiba huo na kutupa nje ya barabara. Hivi ndivyo unavyoweza kufaidi maumivu katika maisha yako;

Usiridhike na hali yoyote mbaya. Je ni mara ngapi umejikuta kwenye hali mbaya ya kiuchumi, mahusiano, afya nk lakini ukaamua kuendelea kuyavumilia maisha hayo? Kuna njia ya kutokea kwenye kila hali bila kujali ukubwa wake. Usitende kosa la kuridhika na hali mbaya inayokukuta. Ukiamini kwanza kuwa kuna njia ya kutoka hapo utakuwa na nia ya kutafuta njia hiyo. Itakuwa ni ngumu kutafuta njia yoyote kama utaridhika na hali yako mbaya inayokukumba.

Ukishindwa jifunze kisha nenda mbele. Kushindwa siyo kosa bali kosa ni kutojifunza kutokana na kosa hilo na kuendelea kubaki hapohapo unapokosea kila siku. Usiridhike na maumivu ya kushindwa bali yafaidi kwa kujifunza na kuwa bora zaidi baada ya kurudi. Kuna nafasi ya kujifunza kwenye kila kushindwa ,tumia fursa hiyo.

Ukidharauliwa ishi upekee wako. Kudharauliwa ni moja ya jambo linalowatesa watu wengi sana. Haya ni maumivu ambayo mtu huyapata baada ya kuambiwa au kuoneshwa kuwa hana thamani. Lakini naomba nikukumbushe kuwa ukiona tusi au dharau yoyote inakuuma badi wewe ndiyo uliyeiruhusu. Waswahili husema tusi haliwezi kuwa tusi mpaka mtukanwa akubali kutukanwa. Huwezi kuwa dhaifu mpaka wewe unayeambiwa umeamini kuwa ni dhaifu. Una nguvu kubwa na ya kipekee ndani yako inayokufanya uwe mtu wa kipekee, usikubali kudharauliwa, bali amsha upekee huo kwa kufanya makubwa ili wakose namna ya kukudharau.

Vumilia. Hata kama upo kwenye njia sahihi bado kuna magumu utakutana nayo. Dunia humpima mtu kama ana nia ya kweli ya kukipata hicho anachokitaka. Hivyo njia pekee ya kufaidi kutoka kwenye maumivu haya ya kutopata kitu hata kama upo kwenye njia sahihi, huwa ni kuvumilia. Wapo watu waliokosa vitu angali walikuwa wanakaribia kuvipata baada ya kukosa uvumilivu kisha kukata tamaa. Ukijiridhisha kuwa mpango ulionao ni sahihi, endelea kuweka nguvu mpaka upate matokeo huku ukijiboresha kila siku.

Usilalamike. Kulalamika huhalalisha matokeo uliyoyapata. Unapolalamika unahisi kuna mtu wa kubeba yale mabaya uliyoyapata na kuwa hakuna haja ya kuchukua hatua kuboresha hayo. Unawajibika kwenye kila linaloltokea maishani mwako. Utafaidi maumivu kwa kuchukua jukumu la kuboresha kila unachofanya badala ya kujikita kulaumu watu.

Njia pekee ya kuyafaidi maumivu si kuyasikilizia, bali kujifunza na kukua. Upepo wa changamoto unavyozidi kuvuma kwako endelea kuimarisha mizizi ya imani na maarifa. Kila wakati angalia kama upo kwenye njia sahihi, kama ndiyo endelea kuweka kuweka nguvu, utapata unachokitaka.

Mhimuli huu wa changamoto na ung’ang’anizi ni mmoja kati ya mihimili kumi na mbili iliyoelezewa kwa kina kwenye kitabu cha DONDOO 366 ZA MAISHA YA MAFANIKIO. Nina imani wewe ni miongoni mwa watu wanaotaka kujenga mafanikio makubwa na ya kudumu, hivyo nakushauri usikose kupata nakala ya kitabu hiki ili upate mwongozo sahihi wa kuwafikia mafanikio hayo.

Gharama ya kitabu hiki ni Sh 20,000/ lakini kwa sababu najali mafanikio yako, sasa utakipata kwa sh 15,000/ tu. Wahi kabla ya ofa hii kuisha. Wasiliana nami kupitia namba 0752 206 899(Alfred Mwanyika).

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *