Dawa Ya Tano Ya Kutibu Ugonjwa Wako Wa Kushindwa.
Lazima upone tu ! Hiki ndicho kinachokwenda kutokea kwenye maisha yako kama kweli utakubali kunywa dawa hizi kwa ajili ya ugonjwa wako wa kushindwa.
Mpaka sasa umeshapokea dawa nne kwa ajili ya ugonjwa wako wa kushindwa; kutibu mtazamo wako, kuishi kwa malengo, kupenda kazi na nidhamu. Hizi ni dawa ambazo inabidi uendelee kunywa kila siku ili uweze kupona. Leo tunaona dawa ya tano ya kutibu ugonjwa huo wa kushindwa ambayo ni ung’ang’anizi na ustahimilivu.
Ung’ang’anizi ni kitendo cha kuendelea kukaa kwenye jambo ulilopanga kulifanya mpaka upate matokeo. Hata kama matokeo yanachelewa lakini wewe unaendelea kuweka kazi. Hata kama mambo ni magumu lakini wewe unaendelea kuweka kazi. Kama kupe anavyong’ang’ania kwenye ngozi ya ng’ombe kwa kwenda naye popote ndivyo ung’ang’anizi unavyohitajika kujengwa kwenye maisha yako ili uupate ushindi.
Utafanikiwa kuwa na ung’ang’anizi kama utakuwa mstahimilivu. Kustahimili ni kuvumilia mateso au vikwazo. Safari ya mafanikio makubwa haijawahi kuwa rahisi hata kidogo, imejaa mabonde, milima ,kona nk. Pia inakuhitaji kujitoa kweli kweli. Mara nyingine inakuhitaji kutoa jasho na damu ili kuweza kupata matokeo makubwa.
Kwa sababu ya ugumu huu, wengi wameishia njiani. Wameanza kwa kuweka nguvu, muda na umakini lakini mambo yalipoanza kuwa magumu wakaacha. Kukosa ustahimilivu imekuwa sababu mojawapo kubwa ya kuugua ugonjwa huu wa kushindwa. Ushindi unahitaji ung’ang’anizi.
Kwa nini ung’ang’anizi?
1. Kutumia rasilimali vizuri. Una rasilimali adhimu kwa ajili ya kujenga mafanikio yako. Miongoni mwa rasilimali hizo ni kama muda, fedha, nguvu, umakini. Kwa sababu ya matokeo kuchelewa wengi wameishia njiani bila matokeo huku wakikubali kupoteza rasilimali hizo ambazo walishaziwekeza. Ili kuepuka kupoteza rasilimali hizi huna budi kunywa dawa hii ya ung’ang’anizi. Kwa kuwa na tabia hii, hutakubali kirahisi kupoteza nguvu zako bila kupata matokeo.
2. Ukaribu na matokeo: Inasemekana kuwa pale unapofikiria kukata tamaa ndipo unapokaribia kupata matokeo ushindi. Kumbe watu wengi waliacha kufanya walivyokuwa wanafanya bila kujua kuwa walikuwa wanakaribia kupata matokeo. Kunywa dawa hii ya ung’ang’anizi na hakikisha huachi mpaka umepata matokeo.
3. Njia ya kuamsha uwezo wako. Kuna nguvu kubwa ambayo bado unayo ndani mwako. Nguvu hii inasubiri kuamshwa ili uweze kupata matokeo. Ukifikia hatua unahisi ukomo kumbuka kuwa bado unanguvu ya kuendelea kufanya jambo hilo na kupata mafanikio. Kunywa dawa hii ya ung’ang’anizi na endelea kuweka kwenye mipango yako. Itakulipa tu.
Kadri kifaranga kinavyoendelea kung’ang’ania kutoka nje ya ganda licha ya kutoona mlango ndivyo ganda linapopasuka kisha kifaranga kutoka nje.
Kadri nyundo inavyoendelea kung’ang’ania kushuka juu ya jiwe licha ya kutoona ufa wowote ndipo jiwe linavyopoteza msimamo kisha kusambaratika.
Kadri matone ya mvua yanavyoendelea kung’ang’ania kuingia kwenye pia licha ya kutokuonekana dalili zozote zile za pipa kujaa, ndipo ung’ang’anizi huu unapofanikiwa kujaza pipa hilo.
Ndugu! Najua kuna mambo mazuri ambayo umekuwa ukipanga kufanya lakini hujapata matokeo ya kueleweka mpaka leo. Pale ulipokutana na ugumu ukaamua kuacha na kufanya kitu kingine ambacho nacho kina ugumu wake. Pia baada ya matokeo kukawia ulikata tamaa na kuamua kutafuta njia fupi lakini nazo hazijasaidia. Nakushauri unywe dawa hii kukomesha tatizo hili; baada ya kuwa na mpango sahihi usiuache kwa sababu yoyote ile mpaka ukupe matokeo.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz