*Dawa Ya Sita Ya Kutibu Ugonjwa Wako Wa Kushindwa.*
Nikupe hongera kwa kuendelea kupata dawa kwa ajili ya ugonjwa wako wa kushindwa. Kama umefanikiwa kunywa dawa zote tano zilizopita, naamini utakuwa umeshaanza kupona ugonjwa wako.
Kumbuka dawa ya kwanza ilikuwa ya kutibu mtazamo wako, ya pili ilikuwa ya kutibu kufanya vitu kiholela kwa kutoweka malengo. Ya tatu ilikuwa ya kukuwezesha kupenda kazi, na ya nne ilikuwa kujenga nidhamu. Lakini ya tano ilikuwa ya kukupa uvumilivu na ustahimilivu. Leo ikiwa ni siku ya sita, utapata dawa kwa ajili ya tathmini.
Tathmini kama Kliniki ya mtoto, baada ya mama kumlea mtoto kwa muda muda fulani, kumpeleka kliniki ili kujua mwenendo wake. Jambo hili huwa ni muhimu sana kwa maendeleo ya ukuaji na afya ya mtoto. Vivyo hivyo unahitaji kujifanyia tathmini kuja mwenendo wa maisha yako.
Katika maisha yako kuna mambo mengi ambayo uliyapanga kufanya. Uliweka au umeweka mipango kwa ajili ya kuyatimiza. Kama ulipata dawa ya pili ya ugonjwa wako wa kushindwa na umeanza kupona, ina maana tayari utakuwa umeshaweka malengo yako bora kwa ajili ya kupata matokeo. Je umetekelezaje malengo uliyojiwekea?
Watu wengi wamekuwa wakiishi bila kujua kama bado wapo kwenye uelekeo sahihi au la malengo yao. Mwaka ulipokuwa unaanza ulipanga uongeze kipato chako mara mbili, je hilo limefika wapi? Hapo ndipo unapokuja umuhimu wa kufanya tathmini. Kwa sababu ya kutofanya tathmini watu wameshinda hata kujua wahafanyi vizuri ili waweze kufanya marekebisho mapema zile sehemu wanazokosea.
Kwa sababu najali sana mafanikio yako, nakuletea dawa iitwayo tathmini ili uweze kupata mafanikio. Hivi ndivyo unavyoweza kupona ugonjwa huu wa kushindwa kwa kuhakikisha unafanya tathmini na kufanyia marekebisho
1. Weka malengo kwanza. Huwezi kufanya tathmini na kujua wapi uimarishe kama hujui kwa dhati ni kitu gani unatakiwa kufanya. Ndiyo maana dawa ya pili ilikuwa inatibu kwanza kisababishi cha ugonjwa wa kushindwa kiitwacho maisha bila malengo. Ili uweze kujifanyia tathmini sahihi, hakikisha unaweka malengo bora kwanza.
2. Gawa malengo yako. Baada ya kuweka malengo yako bora gawa kwenye vipande vidogo vidogo kiasi cha kuweza kuweza kujua nini unachotakiwa kufanya na kukamilisha kila mwaka, mwezi, juma na siku.
3. Fanyia tathmini kila kipande. Baada ya kujua mpango wa kukamilisha kwenye kila kipande cha muda, hatua inayofuata ni kuanza kufanya tathmini. Fanya tathmini kila siku, juma, mwezi, robo mwaka na mwaka.
4. Fanya marekebisho. Faida kubwa ya kufanya tathmini ni kutambua wapi ambako hufanyi vizuri kisha kufanya marekebisho. Au wapi udhaifu wa mfumo wako upo kisha kufanya marekebisho. Kama hujui wapi inabidi uende ni rahisi sana kupotea.
Inawezekana umeshindwa kwenye mambo mengi uliyoanzisha kwa sababu ya kutofanya tathmini. Kuanzia sasa weka malengo kwenye hatua unayotaka kupiga. Ligawe lengo hilo kiasi cha kujua nini unatakiwa ukifanye kila. Kabla hujalala fanya tathmini kujua ni kwa kiasi gani umetekeleza lengo hilo, changamoto ulizokutana nazo kisha jipange kufanya kwa viwango vizuri zaidi siku inayofuata. Rudia kufanya hivyo kila juma, mwezi na mwaka. Hakika utapona ugonjwa wako wa kushindwa na kupata afya ya mafanikio.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz