Fanya Haya Ili Mbegu Yako Ya Uwezo Izae Matunda.
Mkulima akiliona embe huiona mbegu ndani ikiwa mti wenye matunda mengine mengi. Tofauti na mlaji, akiliona embe huona vipande vya embe kwenye sahani akivila huku akifurahia utamu wake.
Hata kama mbegu ya mwembe itakuwa ina uwezo wa kuzaa matunda mengine lakini hupitia hatua mbalimbali ili kuweza kuzaa matunda hayo. Mkukima hutakiwa kuwa mvumilivu kuzifuata na kuipa mbegu hiyo mahitaji yote ili uweze kuzaa matunda yaliyopo ndani yake.
Ndani yako pia kuna mbegu ya uwezo wako wa kuzaa matunda ya mafanikio. Hii ni mbegu ya kipekee ambayo ipo kea kila mtu ikiwa ni pamoja na wewe. Kama mbegu ya mwembe usivyoweza kuzaa nanasi, ndivyo ilivyo kwenye uwezo wa binadamu, usivyoweza kufanya makubwa kama hutatumia uwezo wako wa kipekee.
Hii ni makala maalumu kwako ndugu yangu nikiamini una mbegu tayari ndani yako ya kufanya mambo makubwa ya uwezo. Jifunze kupitia mbegu ya matunda jinsi inavyoweza kuota, kuwa mti na kuzaa matunda ili na wewe uweze kufanya makubwa kwa kutumia mbegu ambayo tayari ipo ndani yako
Tambua kwanza mbegu iliyopo ndani yako. Una uwezo gani wa kipekee ndani yako ili kuweza kuipanda mbegu hiyo na kuzaa matunda? Kuna vitu unavyoweza kufanya kwa viwango vya juu sana mpaka watu wengine wanakushangaa wakati wewe ukifurahia unachokifanya. Huko ndiko mbegu ya uwezo wako iliko, itambue.
Izike mbegu yako. Ili mbegu ya mwembe iweze kuota lazima izikwe kwenye udongo ikae huko kwa muda kisha ianze kuota. Hata wewe unahitaji kujitenga na kelele za dunia zinazokwambia wewe ni wa kawaida. Hata wewe unatakiwa ujizike kwa kutokubali kufanya mambo kwa kuiga watu wengine wanachofanya bali tafuta upekee wako na uuishi huo.
Imwagilie mbegu yako: Mbegu ya mwembe hujitaji maji, hewa na mahitaji mengine ili iweze kumea baada ya kuzikwa. Vivo hivyo na wewe baada ya kujitenga na duniani hakikisha una mahitaji yote yatakayoamsha uwezo wako na kuanza kumea. Maji ya mbegu ya uwezo wako ni kama kusudi la maisha yako, ndoto, maono, mipango nk. Hivyo ndivyo vitaanza kuibua nguvu ya mbegu yako ya uwezo wa kipekee.
Tia mbolea. Baada ya mwembe kuota huendelea kumwagiliwa na kuwekewa mbolea ili uzidi kustawi na kisha kuzaa matunda. Unahitaji mbolea ya hamasa na sababu kubwa ya kwa nini ili uweze kuendelea kustawi. Shukuru kwa matokeo unayoyapata kisha songa mbele.
Subiri: Huwezi kupanda mbegu ya mwembe leo halafu kesho ukavuna matunda. Huchukua miaka kwa mbegu moja ya mwembe kuzaa matunda. Vivo hivyo unahitaji uvumilivu ili mbegu yako iweze kuzaa matunda. Weka mipango na kazi, lakini subiri ili mipango yako izae matunda.
Mbegu huzalisha mbegu. Baada ya mbegu ya mwembe kuota hutarajiwa kuzaa maembe mengine ambayo yatakuwa na mbegu ndani yake ya kuota na kuwa mwembe mwingine ambao utazaa matunda mengine. Uwezo wako kama mbegu ya mti hutarajiwa kuzaa mafanikio na mafanikio hayo kuwa mbegu ya mafanikio mengine bila ya kukoma.
Ndugu! Tayari una mbegu ya uwezo ndani yako. Hii ni ya kukuwezesha kuishi maisha ya mafanikio unayostahili. Kama hujaanza kupata mafanikio basi ni kwa sababu hujachukua hatua ya kuuwekea mazingira mazuri uwezo wako. Tambua kusudi lako, jenga ndoto kubwa, weka malengo na mipango; mbegu yako itaota tu. Kama unahitaji ufafanuzi zaidi, ushauri au vitabu vitakavyowezesha kuota kwa mbegu yako usisite kuwasiliana nami; 0752 206 899. Karibu sana.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz