Itatokeo Na Kwako Lakini Inahitaji Hiki Kutoka Kwako……
Licha ya hamu kubwa ya kupata mtoto anayoweza kuwa nayo mama majamzito, lakini hulazimika kusubiri takribani miezi tisa ili hamu yake kutimizwa. Muda wa mama kusubiri humpa nafasi kukua kiasi cha kuweza kuhimili mazingira pindi atakapotoa nje ya mwili wa mama yake.
Licha ya mbegu ya muhindi kuwa na uwezo wa kuzalisha punje nyingine nyingu lakini mkulima hulazimika kusubiri mpaka mbegu hiyo ipandwe, imee,ikue kisha kuzaa. Katika kipindi cha kuisubiri mbegu izae matunda, mkulima hulazimika kuendelea kuihudumia vizuri mbegu hiyo hata kama hayaoni matunda.
Mifano hii miwili in somo zuri sana kuhusu ndoto na malengo uliyonayo. Una ndoto inayotawala kichwa chako usiku na mchana. Una malengo kwenye maisha yako unayotamani kuyatimiza. Hivi vyote vina matokeo na kuna vitu vingi vinavyosimama katikati ya kile unachokitaka kama vile kazi, nidhamu, changamoto, kushindwa nk. Lakini ili uweze kupata matokeo licha ya haya yote, huna budi kuvipa muda ili vikupe matokeo. Utafanikiwa kuvipa muda kisha kufanikiwa kama utakuwa na kitu hiki muhimu katika mafanikio, nacho ni uvumilivu.
Kuna watu wengi sana ambao hawana matokeo ya mafaniko, si kwa sababu hawana ndoto, au hawana malengo bali kwa sababu ya kukosa uvumilivu. Walikuwa na ndoto wakaweka malengo na mipango mizuri tu, lakini pale matokeo yalipochelewa, waliacha kuweka jitihada na kisha kushindwa.
Inawezekana na wewe ni miongoni mwa watu wanaopitia au waliopitia kipindi kama hiki. Kama unachokifanya ni sahihi na kazi unaiweka lakini matokeo hujapata, hii inamaanisha kuwa muda bado haujatimia. Katika mazingira kama haya, unahitaji uvumilivu tu .
Mama mjamzito hawezi kulazimisha kuzaa mtoto wa miezi mitano kwa sababu ya changamoto za usumbufu anazozipata; huona njia sahihi ya kufika mwisho ni kuvumilia, ndivyo ilivyo kwako, endelea kuweka kazi kwenye mpango sahihi, muda utafika utapata mafaniko.
Wanaofanikiwa ni wale wasioacha kuweka kazi kwenye mipango sahihi licha ya jasho jingi walilokwisha kuvuja. Na wewe ungana na walifanikiwa kwa kuendelea kuweka juhudu kwenye mipango yako licha ya vikwanzo na maumivu unayopitia.
Usiwe miongoni mwa wale walioacha kuweka juhudi baada ya kuona hawapati matokeo, kumbe walikuwa karibu sana na kupata matokeo.
Leo kaa chini kisha tafakari mipango uliyoianza kisha ukaishia njiani. Ifufue mipango hiyo, jiapie kuweka kazi na uvumilivu mpaka upate matokeo.
Matokeo ambayo unayoana kwa watu wengine na wewe utayapata kwa sababu unafanya kamaa wao lakini ulikuwa umepungukiwa uvumilivu tu.
Baada ya mama mjamzito kuvumilia kwa miezi tisa kisha hupata mtoto.
Baada ya mpishi kuvumilia hupakua chakula kilichouva.
Baada ya mponda jiwe kuendelea kushusha nyundo kwenye jiwe, jiwe kubwa hugawanyika.
Hata wewe baada ya kuvumilia kwa muda mrefu kwa kazi na jasho kwenye uelekeo sahihi. Utapata matokeo.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz