Kwani Wewe Mwenyewe Unasemaje ?
Ganda la yai huwa halipasuki kwa kuona muda wa kifaranga kutoka nje umefika, bali ni baada ya kifaranga kuamua kutaka kutoka nje ya ganda.
Ganda huendelea kubaki pale likimuuliza kwani kifaranga mwenyewe unasemaje? Muda wa kutoka nje ukifika kifaranga husema nataka kutoka nje hata kama siuoni mlango wa kutokea. Kadri kifaranga kinavyoendelea kusisistiza huku kikiweka msukumo kwenye ganda kuonyesha mlango, ndipo ganda huanza kupasuka ili kutengeneza malango kifaranga kutoka.
Hakuna jambo muhimu na kubwa utakalopanga usikutane na ukinzani, vikwazo au changamoto zozote. Huwezi ukaweka mipango ya kupata mafanikio kisha usikutane na changamoto. Ndiyo maana changamoto zimekuwa sehemu ya mafanikio pale unapozikabili. Una mpango wa kuyafikia mafanikio, lakini vikwazo vimesimama mbele, imebaki kwako tu ; KWANI WEWE MWENYEWE UNASEMAJE?
Una ndoto yako lakini unaambiwa utakuwa umechanganyikiwa kwani kitu unachofikiria kukifanya hakiwezekani; kwani wewe mwenyewe unasemaje? Ni kweli umechanganyikiwa? Je wewe huoni mwisho ulio na mafanikio kama kweli ukijitoa? Wewe mwenyewe ukikubali kuwa inawezekana na kuamua kutokumsikiliza mtu mwingine, hakuna wa kukuzuia kuitimiza ndoto yako.
Umeweka mipango ya siku kwa shauku kubwa lakini baada ya muda mfupi unaanza kujisikia uvivu na sauti ya kuahirisha inakujia ikikuambia ngoja kwanza ushangae shangae kwenye mitandao ya kijamii kisha utaendelea na kazi. Kisha unakumbuka kuwa hali hiyo ilikutokea na jana na baada ya kuahirisha hukurudi tena kuendelea na kazi uliyokuwa unafanya. Sawa kwani wewe unasemaje? Ukikubali na leo kuacha itakuwa sawa na jana.
Kuna tabia ambayo imekuwa ikikukwamisha wewe kupiga hatua kwa mfano kuweka akiba kwenye kipato unachokipata. Lakini ulijiapia kuwa sasa utaanza kuweka akiba ili kupata mtaji wa biashara. Umefanya hivyo kwa mwezi uliopita lakini sasa kuna sauti inakujia kuwa mbona huna fedha ya kula starehe kama nitaweka akiba? Jiulize kwani wewe mwenyewe unasemaje, mbona ulikubali kuwa utajikaza katika hilo, kwa nini sasa unataka kulegeza msimamo? Sema hapana, lazima niweke akiba.
Umetambua umuhimu wa kuamka mapema ili kuweza kuiandaa siku yako vizuri kwa kuipangilia na kufanya mambo mengine muhimu kwa utulivu zaidi. Kufanikisha hilo umeweka na alamu ili ikutaarifu muda wa kuamka ukifika. Alamu sasa inalia, je wewe unasemaje? Unaendelea kulala kwa nini? Sema hapana kwenye usingizi amka kajenge maisha yako ya mafanikio.
Kuna maisha fulani umekuwa ukiyatamani kuishi lakini kila ukifikiria unaona kama muda bado au kama yapo mbali sana au eneo fulani yamejificha. Ivi ni kweli muda wa kuanza kuishi haujafika? Au unajidanganya? Hivi kweli maisha hayo yapo mbali sana, au unajidanganya? Kwani wewe mwenyewe unasemaje? Sema hapana kwenye mawazo hayo. Maisha unayoyatamani yapo ndani yako na unaweza kuanza kuyaishi sasa.
Ndugu! Chochote kinachotokea maishani mwako hatima yake ipo mikononi mwako. Utakachokubali wewe ndicho kitakachotokea. Kwani wewe mwenyewe unasemaje? Sema kila unachotaka kitokee. Hivyo kikwazo chochote kikitokeo kwenye mbio za kufika mafanikio yako, jiulize kwa mimi mwenye nakubali hiki kinikwamishe? Hakika utapata nguvu ya kusonga mbele.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz