Hiki Ndicho Kinachokufanya Ubweteke, Kimepoteza Wengi!


Categories :

Mimi sina shida! Kwa nini nijitese! Nitafanya kesho! Nisome vitabu ili iweje? Nitakachopata ni hicho hicho.

Haya ni maneno ambayo umeshawahi kuyasema au umesikia wengine wakiyasema. Haya ni maneno yenye ishara ya kuridhika.

Huku ni kuridhika hata kama hujapata matokeo yale uliyostahili. Ni kuridhika kwa kujidanganya huhitaji kitu hicho, ingali una haja nacho.

Kuridhika huku ni kiburi cha kuona bado una muda wa kufanya unayopanga kufanya. Lakini pia unaenda mbali zaidi ukifikiri huna ukomo kwenye muda. Hivyo umeamua kubweteka. Kila hali inayokuhitaji ujitoe zaidi, unaikwepa au kuipuzia kwani unaona kama bado una muda kufanya ambacho unaweza kukipuuzia au kukiahirisha.

Kujiona kama bado una muda kunakufanya ubweteke. Hii imekuwa sababu kubwa ya wengi kushindwa au kuwa wa kawaida kwani wakishaamini kuwa bado wana muda mwingi wakufanya mambo waliyopanga, hujiona hakuna sababu ya kujisukuma zaidi ya hapo.

Kujiona bado una muda kumekupa ujasiri wa kuahirisha mambo ukiamini hata kama usipofanya leo, utafanya kesho.

Kuna mipango ambayo ulipanga uikamilishe mwaka huu,lakini baada ya kukutana na ugumu umeahirisha na kusema utafanya mwakani. Kuna mipango ulipanga uifanye leo, lakini ulipoona hujisikii kufanya ukaacha kwa sababu unajiamini kuwa utafanya kesho.

Umekuwa na wazo la kuanzisha biashara, ni miaka mingi imepita sasa na kila siku unasema bado hujawa tayari. Unasema bado hujawa na maarifa ya kutosha au mtaji wa kutosha. Unajibweteka kiasi hiki kwa sababu bado unaamini una muda wa kutosha.

Ndugu! Maisha yako ni muda wako. Kuna fumbo kubwa sana kwenye maisha yako ambalo ungelikumbuka hili mara kwa mara ungeacha kubweteka kwa kujifariji kuwa unaweza kuahirisha leo kisha ukafanya kesho. Fumbo hili ni kuwa unajua ulizaliwa lini, una umri gani sasa lakini hujui maisha yako yatakoma lini.

Hiki ni kitu kilichopoteza wengi. Walipoteza muda waliopewa wakisema watafanya kesho. Waliahirisha mambo muhimu waliyopanga wakisema watafanya kesho. Lakini ambacho walijisahulisha ni kuwa walikuwa hawana uhakiki na mwaka kesho wa siku ya kesho.

Walikuja kushituka mwishoni kuwa inabidi waondoke hapa duniani. Ndipo waliaanza kufikiri mambo mazuri waliyotamani kuyafanya lakini hawakufanya kwa muda muafaka wakiamini bado wana muda.

Una kitu gani unatamani ukifanye katika maisha yako? Una mipango gani umeiweka mwaka huu ili uikamilishe? Unatamani uwe nani? Leo umepanga ukamilishe nini?

Muda mzuri na uhakika wa kufanya haya yote ni leo tena sasa. Usiingie kwenye kundi la wale waliopotezwa kwa kubweteka wakiamini bado wana muda. Huna uhakika na kesho, hivyo ukipewa leo, itumie vizuri kupanga kufanya mambo yale yaliyo kipaombele kwako kisha kuweka nidhamu ya hali ya juu kuyafanya.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *