Unataka Picha Ya Maisha Yako? Bonyeza Kitufe Hiki!
Mbona siioni hata picha moja?! Mungu wangu inamaana tukio zima hatujafanikiwa kupata hata picha moja! Umeniumbua leo!
Haya yalikuwa ni maneno ya Bwana mmoja aliyekuwa ametoka kukamilisha zoezi la kufunga harusi. Baada ya kuipamba vizuri shughuli ya harusi yake alikuwa na shauku kubwa ya kuyaona matokeo yaliyotokea.
Lakini furaha na shauku vilizima ghafla baada ya kukuta kamera aliyotegemea iwe na picha kutokuwa na picha hata moja.
Hili lilikuwa ni tulio lililomuumiza sana Bwana huyu baada ya kujua hana picha hata moja ya tukio muhimu la harusi yake ambalo lisingeweza kujirudia.
Baada ya mabishano mengi na kutafuta sababu za kwa nini mpiga picha hakufanikiwa kupiga hata picha moja, sababu ilikuwa ni hii; licha mipiga picha kuwaona watu aliyokuwa anawalenga wakiwa wamejaa vizuri kwenye kioo cha kamera lakini alikuwa habonyezi kitufe cha kuruhusu picha inaswe na kuhifadhiwa kwenye kamera.
Hiki ndicho kinachotokea kwenye maisha yako. Umekuwa ukiviona vitu vingi sana unavyotakiwa uwe navyo lakini huna. Umekuwa ukiziona njia za kukufikisha unakotakiwa kufika lakini hata safari hizo hujazianza. Umekuwa ukikitamani chakula fulani maishani mwako, lakini kinachowekwa mezani ni tofauti kabisa.
Sababu kubwa ya haya yote ni kutokubonyeza kitufe kama yule bwana kamera huyu. Maisha yako ni tukio moja tu katika historia ya hapa duniani. Je siku yako ya kutoweka hapa duniani hutaanza kushangaa kama yule bwana harusi?
Bonyeza kitufe cha ndoto yako. Kuna picha ya maisha unayotakiwa uyapate kwenye uhai yako, lakini kila ikikujia unaipuuzia kwa kutoanza kuiishi badala yake unaishi maisha ya kawaida. Ikija ibonyeze.
Bonyeza kitufe cha mipango yako. Tayari unafahamu nini unatakiwa kufanya ili upate matokeo unayotarajia, lakini muda wa kutekeleza ukifika unajipa udhuru. Muda unaenda na huna matokeo. Bonyeza mipango yako.
Bonyeza kitufe cha maarifa. Kuna maarifa ambayo umetambua kuwa unatakiwa uwe nayo maishani lakini huyajengi. Umenunua vitabu lakini huvisomi. Umesoma lakini huweki kwenye matendo. Semina zimetangazwa lakini umepuuzia. Bonyeza maarifa hayo yazame akilini mwako.
Bonyeza kitufe uamke kitandani.* Unafahamu umuhimu wa kuamka mapema ili kuipangilia siku yako vizuri, kupata muda wa kusoma vitabu, kufanya mazoezi nk. Lakini alamu ikikuamsha unaizima haraka na kuendelea kulala. Ni wakati sasa wa kubonyeza kitufe cha kukuata usingizi.
Ndugu! Usishangae kwa nini hupatia kile unachokita maishani licha ya kuwa na uelewa, ni kwa sababu hubonyezi kitufe. Badili matokeo leo kwa kuanza kubonyeza kitufe cha matokeo. Kitufe hicho ni kazi unayotakiwa uiweke mara moja kabla nafsi hiyo haijapita. Chochote kinachotakiwa kutekelezwa, bonyeza kazi hiyo mara moja.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz