Mafanikio Yanajificha Kwanza Huku!
Umeyasubiri kwa muda mrefu lakini huyaoni kwako kama ukiyaona ni kwa baadi ya watu tena wachache. Unaanza kujiuliza yako wapi haya? Nitayapataje?
Haya ni mafanikio ambayo yamekuwa ni changamoto kwa watu wengi kuyapata. Sizungumzii mafaniko yoyote yale, bali yale unayostahili.
Umeumbwa na upekee ndani yako. Upekee huo ni nguvu ya kufanya mambo makubwa na ya kipekee yenye kuleta matokeo ya kipekee. Haya ni matokeo yanayotoa thamani kubwa sana kwa watu ambayo hawawezi kuipata kutoka sehemu nyingine yoyote ila kwako. Haya ndiyo yanayokupa mafanikio kamili.
Mafanikio kamili yamejificha wapi? Yangekuwa waziwazi kila mtu tungemkuta nayo. Lakini kwa sababu ni wachache tu wanayo basi kuna sehemu yamejificha na unahitaji kujua ili uyafichue na yawe yako.
Leo utaenda kujua wapi mafanikio yako yamejificha na uanze kuayaficha na kukutana nayo waziwazi. Kwa sababu una shauku ya kujua wapi mafanikio yako kamili yalipo ngoja nikuambie ili ujue mapema; mafanikio yako yamejificha kwenye mambo usiyoyafanya.
Unaweza ukawa umeshangaa kwa jibu hilo, ndiyo mafanikio yako kwenye mambo usiyoyafanya! Kwa lugha nyingine yale unayokazana kufanya yana mchango mdogo sana au hayana mchango kabisa kwenye mafanikio yako unayistahili. Ndiyo maana licha ya kuamka kila siku na kwenda kazini lakini umeambulia kiduchu.
Yafutayo ni mambo ambayo yameshikilia mafanikio yako. Ukiyafahamu haya na kuanza kuyafanyia kazi, hakika utaanza kupata matokeo ya tofauti.
Vitu unavyoviogopa. Vitu unavyoviogopa ni vile ambavyo hujazoea kuvifanya. Hivi ni vitu vyenye hatari kubwa na wewe hutaki kuweka jitihada kukabiliana na hatari hizo. Hivyo umeamua kuendelea kufanya vitu ulivyovizoea. Lakini nakukumbusha kuwa hakuna matokeo ya utofauti kwenye ulivyozoea kuvifanya.
Vitu ambavyo hujisikii kuvifanya. Hakuna maajabu kwenye kufanya vitu unavyovipenda tu. Waliofanikiwa wanafanya vitu muhimu vya kuwapa matokeo hata kama hawavipendi. Hujapata unavyotakiwa kuvipata kwani umekuwa ukivifanya vitu unavyojisikia kuvifanya hata kama havina mchango. Kupata mafanikio ni lazima ufanya kilicho sahihi siyo unachojisikia.
Vitu unavyoviahirisha. Unaweka malengo kisha mipango ya kupatia matokeo malengo yako. Lakini muda ukifika hufanyi, unasema kesho. Weka nidhamu ya kufanya kwa muda ulipupanga ili upate matokeo kwa wakati.
Kwenye kazi. Kwa asili ni mvivu. Mwili wako haupendi kufanya kazi au kufanya kidogo. Ni mpaka pale utakapoulazimisha ndipo utaweza kufanya makubwa. Ipende kazi.
Hivyo ndugu, mafanikio yapo na yamekuzunguka lakini yanatanguliwa na vitu ambavyo umekuwa huvifanyi au umekuwa unavifanya kwa kiwango kidogo. Hayo ni baadhi ha mambo ambayo ukianza kuyafanya utapata matokeo mazuri.
Toka nje ya sanduku leo. Fanya vile unavyoviogopa lakini unaona vitakupa matokeo ambayo hujawahi kuyapata. Fanya hata pale ambapo hujisikii. Ipende kazi nayo haitakuangusha kamwe.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz