Wewe Ni Mbegu, Toa Matunda!
Wewe ni mbegu. Kama mbegu nyingine, unatarajiwa uweze kuzaa matunda yenye mbegu kisha nayo yazalishe matunda mengine.
Sababu mojawapo inayosababisha kutokukua au ukuaji mdogo ni kwa sababu ya kutoitumia mbegu iliyopo ndani yako kuzaa matunda na mbegu nyingine pia.
Mbegu ya mwembe huzaa maembe yenye mbegu kisha mbegu hizo huwa miembe amabayo huzaa maembe mengine. Hivyo mbegu moja ya mwembe inweza kuzalisha msitu wa miembe mingine.
Ndani yako kuna mbegu ya uwezo ambayo inazaa matunda ya thamani. Kama mbegu ya mwembe isivyoweza kutoa machungwa, ndivyo uwezo wako ulivyo wa kipekee wa kuzalisha matundaa ya kipekee.
Swali la kipekee unalotakiwa kujiuliza na mbegu gani uliyonayo? Ukijua mbegu hiyo itakuwa rahisi kujua kama umeshaanza kutoa thamani ambayo ndiyo matunda au la!
Mbegu yako ni kipaji chako. Mbegu yako ni vitu unavyoweza kuvifanya kwa namna ya pekee kabisa kiasi cha mtu mwingine kutoweza kukufikia hata akikuiga. Mbegu yako ni vitu unavyopenda kuvifanya, upo tayari kufanya hata bure mara nyingine.
Je ni sanaa fulani; kuimba, kuigiza, kucheza mpira, uchoraji? Je ni kufundisha, kuandika, uongozi ? Hizi ni baadhi ya mbegu ambazo binadamu anaweza kuwa nazo, wewe una mbegu gani?
Mbegu yako ni utajiri. Uwezo wako utoe thamani. Thamani yako inunuliwe na watu wengine. Thamani moja inatarajiwa itoe thamani nyingine. Kwa mfano unauza bidhaa au huduma. Ukipata faida ya kwanza, hiyo ni mbegu nyingine ambayo unaweza kununua bidhaa nyingine na yenyewe ikatoa faida pia.
Tengeneza msitu kutoka kwenye mbegu yako. Mbegu ya uwezo wako inatarajiwa kukua kila siku na kuleta mafaniko zaidi. Nanasi moja inaweza kuzalisha hekta nyingi tu za minanasi kama mbegu za matunda ya kila mti zitakuwa zinapandwa. Hakikisha kila mafaniko unayoyapata yanakuwa mbegu ya kuzalisha mafaniko mengine. Usiridhike na kile ulichonacho sasa.
Usife na mbegu. Hata kama mbegu ya mbuyu inaweza kuota na kuwa mti mkubwa sana duniani, isipokubali kuzikwa kisha kuota na kuwa mti haiwezi kuwa hata kama mchicha. Usiishi bila kutumia mbegu yako. Kipindi hiki cha uhai wako ndiyo kipindi cha kutumia mbegu yako. Weka malengo na jisukume kuyatimiza nawe utafanikiwa kufa huku mbegu yako ikiwa miti ambayo wengine wataendelea kula matunda yake.
Ndugu! Kaa chini na tafakari, ni mbegu gani unayo ndani yako. Ioteshe hiyo ili izae matunda. Dunia inasubiri matunda hayo maalumu kutoka kwako ili iyafaidi. Utakapofanikiwa kuipa dunia matunda mengi, dunia itakipa nawe utakuwa tajiri.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz