Siri Ya Kubadili Maisha Yako Imejificha Hapa.
Kuna maisha unayoyataka hayo unayoyaishi sasa siyo yenyewe. Kuna vitu unavyotamani uwe navyo, ulivyo navyo siyo vyenyewe au ni vichache. Una kipato unachotamani uwe nacho, ulichonacho hakikutoshi.
Nawezaje kuishi maisha yangu ninayoyapenda? Nawezaje kupata kipato kinachonipa uhuru? Nawezaje kuwa mtu ninayetaka? Naanzia wapi?
Huwa inaonekana kuwa kama kuna siri iliyojificha ambayo watu wengi hawaijui kiasi cha kushindwa kuishi maisha wanayoyataka! Licha ya kundi kubwa la watu kutokuwa na maisha wanayoyataka, lakini wapo wachache waliofanikiwa kupata vitu wanavyovitaka na kustahili.
Kuna siri za wewe kupata unachokitaka maishani. Leo nitakuambia siri moja muhimu na kisha uanze kuitumia mara moja. Siri hiyo ni KUBADILI MTAZAMO.
Hatua ambazo umekuwa ukizichukua na zilizosababisha hali uliyonayo sasa ni kwa sababu ya mtazamo wako. Kipato ulichonacho ukizingatia umri ulionao ni kwa sababu ya mtazamo wako. MTAZAMO ni jinsi unavyoyaona mambo. Hii ni miwani ya kuona mambo kisha kuyatafsiri na kuchukua uamuzi.
Kuna aina mbili za mitazamo; hasi na chanya. Miongoni mwa mitazamo hasi iliyowagharimu wengi na kutopata wanvyostahili ni; Kuna mtu wa kuwajibika na maisha yangu, kuna watu wachache wenye bahati, utajiri ni dhambi, kuna uhaba duniani, mimi sina kipaji, kuna watu wachache wanayostahili mafanikio, biashara ni za makabila fulani nk.
Lakini watu waliofanikiwa wana mitazamo chanya tofauti na walioshindwa. Waliofanikiwa wanaamini kuwa wanawajibika kwa 100% kutengeneza wanachokitaka. Wanajiamini na wanaamini kuwa dunia ina utele na wanaweza kupata utajiri wa kila kitu. Imani hiyo inawafanya waendelee kuweka jitihada hata pale matokeo yanapochelewa.
Norman Vicent Peale alisema “Change your thoughts, and you change your world” ikiwa na tafsiri kuwa badili mawazo na utabadili dunia yako. Kulingana na jinsi unavyofikiri, unakuwa na dunia yako. Hivyo kama dunia uliyopo sasa huifurahii, basi namna pekee ya kuibadili ni kubadili namna unavyofikiri yaani mtazamo wa kifikira.
Je unataka kuibadili dunia unayoiona sasa? Inawezekana kabisa kuijenga dunia unayoitaka wewe kwa kuwa unayemtaka wewe. Badili mtazamo wako.
[ ] Fikiri na jione kuwa unaweza kuwa mtu yoyote unayetaka
[ ] Amini kuwa unaweza kupata chochote unachokitaka
[ ] Amini kuwa dunia ina utele
[ ] Ona kuwa una wajibika kwa 100% kutengeneza maisha yako
Acha kujiona mnyonge. Una nguvu kubwa ndani yako ya kuwa unayetaka kuwa. Acha kujidharau. Jipe thamani unayostahili.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz