Huu Ndiyo Wakati Wa Kuonyesha Imani Yako!


Categories :

Mambo mengi kama siyo yote ya msingi utakayokuwa unafanya maishani mwako hayatakuwa na majibu ya papo kwa papo. Hivyo unanitaji kusubiri ndipo uone matokeo.

Kuna matokeo yatachukua muda mfupi kutokea, wakati mengine yakichukua muda mrefu. Kwa sababu ya matokeo kuchelewa, kuna watu wamekosa uvumilivu kisha kukata tamaa.

Lakini kwa sababu ya matokeo kuchelewa , mara nyingine imekuwa ni vigumu kufanya vitu ambavyo ni mara ya kwanza, na hujawahi kupata matokeo hayo wala jamii kuyashuhudia. Ndipo jamii inapokuja na kukuona wewe ni wa ajabu ikiamini unafanya jambo ambalo halipo kabisa.

Mambo uliyoyopanga yanapokuwa magumu kiasi cha kutotoa matokeo mpema au unapokuwa na ndoto yako kiasi cha watu kutoamini kuwa una maanisha unachofanya, hapo ndipo unapotakiwa kuonyesha na kuishi kitu kimoja kinachoitwa IMANI KUBWA ndani yako.

Imani ni kuwa na uhakika kuwa jambo unalolifanya au tarajia litatokea. Hata pale mazingira ya sasa yanapokuwa hayaonyeshi dalili hizo, imani huona matokeo.

Ni kwa njia ya imani mtu huendelea kuweka jitihada kwenye kile anachokifanya hata kama hayaoni matokeo.

Ni kwa njia ya imani ndipo wewe utaendelea kusimamia na kuendelea kufanya kile ambacho wengine wanasema huwezi kukifanya.

Ni kwa njia ya imani ndipo unapoweza kuendelea kuvumilia maumivu makali ya hatua unazochukua ukitambua hayo ni mpito ya kuelekea kwenye matokeo mnayotarajiwa.

Ni kwa njia ya imani ndipo unapoweza kufurahia mchakato wa kupata matokeo badala ya kusubiri furaha ya muda mfupi ya matokeo.

Ndugu, litafute jambo moja linalopiga kelele sana moyoni na akilini mwako. Linapiga kelele kwa nini usifanye hivi, ni sauti ambayo imekuwa ikijirudia mara kwa mara lakini umekuwa ukiipuzia.

Kwenye jambo hilo ndiko unakoweza kujenga imani kubwa ya kuhakikisha unakipata unachokitaka.

Ukijenga imani kwenye jambo hilo hakuna kitu kitakachokuzuia kupata unachokitaka labda kifo. Calvin Coolidge  aliwahi kusema “Nothing in the world can take the place of persistence” akimaanisha kuwa hakuna kitu cha kuchukua nafasi ya ustahimilivu duniani. Aliendelea kusema sio kipaji, akili nyingi wala elimu.

Lakini kumbuka kitu pekee kinachokufanya uvumilie kwenye kutafuta kitu ni imani. Yaani matumaini ya kuona tayari unacho hata kama huna hicho kitu mkononi.

Ili ufanikiwe kupata matokeo makubwa maishani mwako huna budi kuwa na angalau kitu kimoja ambacho ni kikubwa na umekijengea imani kubwa ya kukipata. Lije jua au ije mvua, wewe utapambana na kila hali mpaka ukipate.

Je imani hiyo umeijenga kwenye jambo gani? Je ni uhuru wa kifedha kupitia biashara unayoifanya? Au ni ndoto kubwa uliyonayo ya kutatua tatizo kubwa la umasikini kwenye jamii?

Imani yako tutaiona kwenye jambo gani? Tafakari na amua leo kipi kitakufikisha kwenye ridhiko la maisha yako na na imani nacho; CHAGUA NA ANZA KUKIFANYA LEO.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *