Hamasa Inaweza Kuzima Njiani, Lakini Huyu Ataendelea Kuwaka Mpaka Mwisho……..


Categories :

Je unakumbuka siku ulipopata hamasa kubwa ya kufanya kitu? Labda baada ya mtu aliyefanikiwa kukusimulia jinsi inavyowezekana kupata unachokitaka, ulijisikiaje? Naamini ulikuwa u unajisikia mwenye nguvu kubwa ya wewe pia kwenda kufanya kazi.

Je unakumbuka mwaka mpya ulipokuwa unaanza na kuwasikia watu wengi wakisema mwaka mpya na mambo mpya. Ulikuwa na hamasa kubwa sana ya kuona mwaka huo mpya unaenda kufanya makubwa, miezi mitatu imepita sasa, je ile hamasa bado ipo?

Hamasa pekeyake haitoshi kukusaidia wewe kupiga hatua kubwa. Ni kama moto tu wa kuni, haijalishi umekolea kiasi gani, kama hutaendelea kuuchochea utaisha tu. Kuna kitu kinachotakiwa kiitangulie au kwenda sambamba na hamasa, nacho ni NIDHAMU.

Hamasa pekeyake haiwezi kukubeba

Safari ya mafanikio makubwa ni ngumu; utakosa matokeo kwa muda, utapata hasara, vitu havitaenda kama ulivyopanga. Hii itakufanya usijisikie kufanya unachotakiwa, unahitaji zaidi ya hamasa ambayo ni nidhamu.

Nidhamu ni kitendo cha kufanya unachotakiwa kukifanya bila kujali unajisikia au laa. Ni kupitia nidhamu ndipo watu wanafanikiwa kupata matokeo hata kwenye njia ngumu.

[ ] Hutajisikia raha kuacha usingizi mtamu wa asubuhi kisha kuamka mpema. Hata kama huna hamasa lakini kumbuka ndiyo kitu sahihi unachotakiwa kufanya hata kama hujisikii.

[ ] Hutajisikia raha kutonunua kitu kizuri ambacho hakikuwa kwenye bajeti ili ufanikiwe kuweka akiba. Hata kama huna hamasa kumbuka kuweka akiba ndiyo njia sahihi ya kujenga utajiri.

[ ] Hutajisikia raha kukimbia au kufanya mazoezi huku misuli ikikuuma. Hata kama huna hamasa fanya hivyo kwa sababu ndiyo njia ya kuboresha afya ya mwili wako.

[ ] Hutajisikia raha kuwapigia simu wateja ungali unafahamu kuwa wanaweza kukujibu vibaya. Unahitaji kujenga nidhamu ya kufanya kwa kutambua ndiyo njia pekee ya kupata wateja wazuri.

Ndugu hamasa hupungua na kuisha lakini ukijenga nidhamu inakuwa ni sehemu ya maisha yako. Kwa kujenga nidhamu utakuwa na mtazamo kuwa ili ufanikiwe unahitaji kutoa MATOKEO na sio SABABU. Kwa kuwa na mtazamo huu utafanya unachotakiwa kufanya bila kujali visingizio.

Ili kujenga nidhamu huna budi kujua sababu ya kwa nini ujitese au kujilazimisha kufanya unachotakiwa kufanya. Tengeneza KWA NINI KUBWA kwenye kila nidhamu unayotaka kuijenga.

Je kwa nini ujitese kufanya mazoezi. Je ni kwa sababu ya kuboresha afya dhaifu uliyonayo?

Je kwa nini ujitese kuweka akiba angali kuna vitu vizuri unatamani kununua? Je ni kwa sababu unataka kukusanya mtaji wa biashara?

Chagua kitu kimoja leo utakachokifanya kila siku kwa huu wote. Tafuta KWA NINI KUBWA ya kufanya kitu hicho kisha kifanye kila siku.

Jiunge na wenzako wanaoendelea kujenga nidhamu kali kwa kufanya jambo moja kila siku bila kuacha. Hii ni kupitia programu ya JENGA NIDHAMU 2023 chini ya AMSHA UWEZO.

Kujiunga na programu hii ambayo ni bureee kabisa bonyeza kiunganishi hiki hapa chini https://t.me/+uftysBbpBl4zODE0

Karibu sana.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *