Kaa Juu za Mizani Hizi Kujua Kama Unakua au Unakufa.


Categories :

Kuna kauli inasema kama hukui basi unakufa. Ni kauli muhimu sana ya kupima jinsi unavyoenenda katika maisha yako. Pia ni kiashiria kuwa kumbe ili uweze kufanikiwa unahitaji kukua, la sivyo utakuwa unakufa.

Je kwa jinsi unavyofanya mambo yako unakua au unakufa? Mtoto akipelekwa kliniki ili kujua kuwa unakua au la moja ya kipimo anachopimwa ni uzito kwa kutumia mzani. Ili kujua mtoto huyo anakua basi uzito wake wa mwezi huu unatarajiwa kuwa mkubwa kuliko wa mwezi uliopita.

Kuna mizani unazoweza kutumia kujua kama kweli unakua maishani mwako au laa. Mizani hizo zitapima ukuaji wako wa ndani kwanza kabla ya nje. Tutajikita kwenye ukuaji huu kwa sababu mtu hawezi kukua nje kabla ya ndani.

Je unaumizwa na matokeo au unajifunza kutokanayo? Maisha yako yamejaa matukio, yanayofurahisha na yanayoumiza. Watu wamepata shida kubwa kutokana na matukio yanayoumiza. Wapo waliokata tamaa, wapo waliougua magonjwa nk. Kukua ni kutoumizwa na matukio ali kujifunza kutokana nayo. Je mtu akikufanyia ubaya unaumia au unajifunza na kupuuzia. Kujifunza na kutoumizwa ni ishara ya kuwa unakua.

Je unaweza kutoa nje ya eneo huru? Moja ya changamoto kubwa inayosababisha usipige hatua ni kuendelea kung’ang’ania eneo lenye uhuru ambalo hutaki hata kujinyoosha. Yaani kwa lugha rahisi ni kufanya kwa mazoea. Kukua ni kujisukua kutoka nje ya mduara. Amaka mapema zaidi, jifunze zaidi, fanya kwa ubora zaidi, weka malengo makubwa zaidi nk

Je unafanya kilicho sahihi au unachojisikia? Kuna muda huwa unafika unajua kabisa kilichosahihi kufanya lakini hisia zinakuwa kinyume. Kisha unaahirisha kufanya sahihi na kuzitii hisia. Unatakiwa uweke akiba, lakini hisia zinakuvuta kununua kitu ambacho hakikuwepo hata kwenye bajeti. Ili kujua kama unakua, fika hatua ya kufanya kilichosahihi sahihi siyo kile unachojisikia.

Je leo ni bora kuliko jana? Mafanikio yako ni mkusanyiko wa matokeo ya jitihada ndogondogo unazozifanya kila siku. Ili kukua hakikisha leo yako ni bora kuliko jana. Matokeo ya leo lazima yawe mazuri kuliko jana. Kuna nafasi ya kuboresha kwenye kila unachokifanya.

Leo kaa juu ya mizani hizo nne na jipime kuona kama unakua au unakufa. Kama unakufa, fufuka leo.
Usikuli kuumizwa kirahisi, toka nje ya mduara wa mazoea, thibiti hisia zako kisha hakikisha leo ni bora kuliko jana.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *