Zuia Kazi Isitanuke; Kamilisha Kazi Nyingi Kwa Muda Mfupi.
Zuia kazi isitanuke, unaweza ukawa umeshituka au kujiuliza kuwa inawezekanaje kazi ikatanuka! Ni kweli kazi huwa zinatanuka. Hapa utajifunza namna ambavyo umekuwa ukiruhusu kazi zitanuke na kuchelewesha mafanikio yako.
Sheria ya Parkinson inasema “It is a commonplace observation that work expands so as to fill the time available for its completion” ikiwa na tafairi kuwa ni kitu cha kawaida kuona ukubwa wa kazi ukiongezeka ili kujaza muda uliopo.
Hiki ndicho kinachotokea kwenye maisha yako ya kila siku. Inawezekana pia ndiyo sababu iliyosababisha ushindwe kukamilisha mambo mengi uliyotamani uyafanye.
Pale unapokuwa na jukumu la kulifanya hata kama ni dogo la lutumia muda mfupi lakini kama hujalipangia muda, kuna uwezekano mkubwa sana wa jambo hilo kuchukua muda mwingi uliopo.
Hii ni sheria inayoweza kuelezewa katika mazingira na matukio mbalimbali ya asili.
[ ] Fikiri pafyumu iliyogandamizwa kwenye kichupa kidogo itasambaa chumba kizima baada ya kuipulizia kwenye pembe moja tu ya chumba.
[ ] Maji yaliyopo kwenye bomba jembamba yatasambaa eneo kubwa baada ya kuyatoa kwenye bomba hilo.
Hivyo usipoiwekea kazi muda maalum unayoifanya itasambaa kwenye muda wako mwingi ambao unaonekana uko wazi tu.
[ ] Kama umekuwa ukishangaa mbona siku imeisha lakini matokeo na madogo kuliko muda uliotumia, basi tambua kazi zako zilikuwa zinatanuka.
[ ] Kama unaona ufanisi wa kazi ni mdogo. Ubora unapungua, basi tambua kuwa umeachia muda wako utanuke.
[ ] Kama kuna kazi umeifanya kwa muda mrefu sana kiasi cha kukuanza kukuchosha, basi tambua kuwa umeuacha kazi zako ziwe zinatanuka.
Maji yakielekezwa kwenye bomba hasa dogo huwa na kasi na mgandamizo mkubwa kuliko yakiwa kwenye bomba kubwa au yakiachiwa yatembee tu ardhini.
Miale ya jua ikikusanywa na kuelekezwa sehemu moja ina nguvu kubwa ya kuunguza kuliko ikiachwa isambae tu eneo kubwa.
Hii ni mifano ambayo inadhihirisha ni kwa namna gani unaweza kuwa na ufanisi mkubwa pale utakapoamua kuzielekeza kazi zako kwenye muda maalumu. Unaweza kutekeleza hilo kwa kuzingatia yafuatayo
[ ] Hakikisha kila kazi unayoifanya unaipa muda maalumu. Kamwe usiseme utafanya tu kwa muda utakaokuwepo.
[ ] Uheshimu muda ulioipa hiyo kazi. Weka umakini wako wote kwenye kazi ya muda huo.
[ ] Jiepushe na usumbufu wowote unaotegemea kujitokeza wakati unafanya kazi uliyoitengea muda.
[ ] Kamilisha jambo hilo kwanza kabla ya kwenda jambo jingine.
Ndugu! Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya kazi, muda na mfanikio. Kadri unavyofanya kazi nzuri yenye thamani kubwa kwa muda mfupi ndiyo unayojihakikishia kupata mafanikio makubwa kwa haraka zaidi.
Unahitaji kujenga nidhamu kali ya kutoitanua kazi yako. Iwekee kazi yako muda maalumu, iwekee kazi yako muda wa mwisho.
[ ] Kuanzia sasa anza kuziwekea kazi zako muda maalumu kisha jisukume kukamilisha ndani ya muda huo maalumu.
[ ] Hakikisha hakuna muda unaobakia wazi kiasi cha kazi moja kutamani kutanukia huko
Anza kwa kutafuta jambo moja ambalo unaona ukilikamilisha litakupa matokeo makubwa sana. Lipe muda maalumu wa kulikamikisha. Kisha weka umakini wako wote kwenye jambo hilo. Hakika utapata matokeo yenye thamani kubwa sana.
Asante.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz