Unataka Mafanikio Zaidi? Anza Kulipia Gharama Hizi Tano(5).


Categories :

Ukienda dukani kununua bidhaa, uwingi wa bidhaa utakazozipata itategemea pia na kiasi cha gharamaambazo utakuwa upo tayari kuzilipa. Kadri utakavyolipia kiasi kikubwa ndivyo utakavyoweza kupata bidhaa nyingi. Kama utakuwa unataka bidhaa bora na za ghali, utatakiwa ulipie kiasi kikubwa zaidi ili uweze kupata bidhaa nyingi zaidi.

Ni hamu ya kila binadamu kuwa na mafanikio kwenye kila eneo la maisha; uchumi mahusiano , kazi, afya, kiroho nk. Pia hamu hiyo siyo ya mafanikio yoyote bali mafanikio makubwa. Habari njema ni kuwa duniani ina utele wa kila kitu hivyo kila mtu anaweza kupata mafanikio yoyote yale tena kwa kiwango akitakacho.

Licha ya dunia kuwa na utele huo wa mafanikio, lakini mafanikio hayo hayapatikani bure. Mtu anahitajika kulipia mafanikio hayo kulingana na kiwango anachokitaka. Licha ya utele huo pia watu wengi wameendelea kuwa na mafanikio madogo ambayo hawaridhishwi nayo. Udogo wa mafanikio hayo ni ishara kuwa gharama wanayolipia ni ndogo. Kama unaona mtu anamafanikio makubwa, tambua kuwa amekuwa tayari kulipa gharama kubwa inayolingana na mafanikio hayo makubwa aliyoyapata.

Ndugu! Natambua kuwa umechoshwa na maisha hayo ya kawaida ambayo hayakuridhishi. Lakini umeyapata maisha hayo kwa kulipa gharama kidogo kwa yale ambayo umekuwa unafanya. Kama upo kwenye njia sahihi, unaweza kuyapata mafanikio makubwa zaidi ambayo yatakuridhisha kwa kulipia zaidi mafanikio hayo. Naenda kukushirikisha maeneo matano ambayo unaweza kulipia zaidi ili uweze kupata mafanikio makubwa.

Eneo la kwanza; Muda. Hakuna kitu chochote kinachoweza kutokea kama hakuna muda. Ni muda ndiyo unaokuwezesha kufanya jambo lolote. Kama umepata mafanikio madogo kwenye eneo fulani la maisha yako kwa mfano mahusiano au fedha, ujue hujalipia muda wa kutosha katika eneo hilo. Utahitaji kuwekeza muda zaidi ili kuweza kupata mafanikio zaidi. Hakuna binadamu mwenye muda wa ziada kwenye siku, hivyo ili uweze kuwekeza zaidi huna budi kuweka vipaumbele kwenye matumizi ya masaa 24 ya siku.

Eneo la pili; Umakini.Ili muda ulioulipia hapo juu uwe na tija ya kukupa mafanikio zaidi, utumiaji wa muda huo lazima uambatane na ongezeko la umakini. Utulivu na uwepo wa akili kwenye kufanya kazi lazima uongezeke ili uweze kupata mafanikio makubwa zaidi. Umekuwa ukitumia muda mwingi kufanya jambo na kuishia kupata matokeo madogo kwa sababu ya kutokuwa kwenye kile unachokifanya kwa 100%. Amua kuweka kuwa unaelekeza akili yako kwenye kile unachokifanya mpaka upate matokeo.

Eneo la tatu; Maarifa. Maarifa ndiyo yanayokupa ufahamu wa namna ya kufanya vitu kiusahihi. Kama una uelewa mdogo kwenye jambo unalolifanya ndivyo utakavyoishia kupata matokeo madogo. Tafakari eneo ambalo unataka kuongeza mafanikio kisha anza kupata maarifa zaidi kwa kusoma vitabu, kushiriki semina nk.

Eneo la Nne; Nguvu. Ili uweze kutumia gharama(muda, maarifa na umakini) ulivyoongeza hapo juu lazima uwe na nguvu za kuvitumia. Matokeo hutokea baada ya kuweka kazi ambayo inazaa matunda. Kufanya kazi kunahitaji utimamu wa mwili, hivyo hakikisha unafanya mazoezi, unakula vizuri na kupata muda mzuri na wa kutosha wa kulala ili kuufanya mwili wako kuwa imara. Ongeza kiwango cha kuulinda mwili wako na magonjwa ili uzidi kuimarika na kukuruhusu kufanya kazi zaidi.

Eneo la Tano; Maumivu. Mafanikio yako hayakui na kuendelea kuwa pale pale ulipo kwa sababu ya kuyaogopa maumivu. Pale ulipotamani mafanikio zaidi na kulazimika kufanya zaidi ya ulivyozoea, ulikutana na maumivu na kurudi kwa kiwango ulichozoea ambacho hakina maumivu. Iambie akili na mwili wako kuwa tayari kwa maumivu yanayoweza kujitokeza wakati wakukuza akili yako. Kuna gharama ya uvumilivu ambayo inabidi uilipe ili uweze kukua kutoka hapo ulipo. Lipa gharama kwa kuvumilia kuchelewa kupata matokeo makubwa, maumivu ya kufanya kazi muda mrefu, kukataliwa nk.

Anza kufanyia kazi maeneo haya matano kwa kuweka nguvu zaidi ya vile unavyofanya sasa ili uweze kukua zaidi ya hapo ulipo sasa. Kadri unavyoendelea kulipa gharama zaidi ndipo utatengeneza thamani kubwa zaidi kwa watu wengine na kuwa chanzo cha mafanikio zaidi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *