Nguvu ya Maono Katika Kujenga Nidhamu Kali.
“Dreva akishajikumbusha akilini mwake safari ndefu iliyopo mbele hujikuta akiongeza mwendokasi na kutamani sehemu nyingine magurudumu ya yasikanyage”
Kama umeshawahi kupanda mabasi yanayokwenda masafa marefu kwa mfano Dar – Tunduma au Mwanza Dar utaelewa kauli hiyo hapo juu. Madreva wa mabasi kama hayo huwa na nidhamu kali sana.
Nidhamu hiyo kwanza huanzia katika maandalizi ya safari zao. Huhakikisha kila kitu kipo sawa kabla kesho ya safari haijafika. Hivyo kama kuna kitu kina kasoro huhakikisha kimerekebisha ili kisilete shida wakati wa safari ya kesho.
Siku ya safari huhakikisha wanakuwa wa kwanza kwenye foleni ili muda wa kuondoka ukifika wasiwe nyuma ya mabasi mengine na yasiwazuie uharaka wao.
Safari ikianza ndipo huhakikisha kila wakati wanaendesha kwa kasi kubwa inayoruhusiwa ili kuhakikisha wanaendelea kupunguza umbali mrefu uliopo.
Nidhamu hiyo haiishii hapo, bali huendelea hata pale wanapotakiwa wasimame sehemu kupata chai au chakula na ‘kushimba dawa’. Ndipo muda maalumu (dakika tano) hutolewa ili abiria kupata huduma hiyo. Hapo ndipo abiria huweza kuachwa kama asipozingatia muda huo.
Nidhamu hii kali ya dreva huyu hutokana na maono ya safari aliyonayo. Kwani huamini akipoteza muda atashindwa kufika kwa wakati. Kutofika kwa wakati huathiri ratiba za abiria na pia gari lenyewe kwa siku inayofuata.
Hapa kuna somo kubwa sana la kujifunza katika kujenga nidhamu kali maishani mwako. Ukitaka kufanikiwa kujenga nidhamu kali ya kukusukuma kuchukua hatua za kukupa mafanikio makubwa, hakikisha una maono ya wazi kabisa.
Nini kikubwa unataka kukipata maishani mwako? Wapi unataka kufika maishani mwako? Gharama gani unazotakiwa ulipe ili uweze kupata mafanikio unayoyataka?
Maswali haya ukiyajibu utakuwa unatambua safari yako ndefu uliyonayo na jinsi unavyotakiwa ujitoe kulipa gharama za kutimiza ndoto uliyonayo.
Nidhamu ndiyo kiungo kikuu cha kukuwezesha kutumia uwezo ulionao ili kuishi ndoto yako. Lakini kujenga nidhamu kali imekuwa changamoto kwa watu wengine kwa sababu ya maumivu unayotakiwa kuyavumilia ili kuchukua hatua ngumu.
Lakini kwa kujua umbali wa safari ya ndoto yako uyotakiwa kuifikia na kuuona uzuri wa mwisho wa safari yako utapata nguvu ya kuhakikisha unajitoa na kupata matokeo. Umekuwa huweki nidhamu kubwa kwenye yale unayoyafanya kwa sababu hujawa na maono ya wazi na shauku ya kile unachotaka kupata.
[ ] Je ndoto yako ni kufikia uhuru wa kifedha ili kuondokana na utumwa wa fedha ulionao sasa?
[ ] Je ndoto yako ni kuwa na biashara kubwa itakayoajiri watu wengi ambao hawana ajira sasa?
[ ] Je ndoto yako ni kuwa kiongozi ambaye utaongoza kutatua changamoto nyingi zinazowakabili watu?
[ ] Je ndoto yako ni nini?
Kuwa na maono au ndoto iliyowazi ni ni kuuona mzigo mkubwa uliombele yako. Ukifanikiwa kuuona mzigo huo au urefu wa safari ndefu uliyonayo itakupa hamasa ya kujenga nidhamu kali ili kupata matokeo. Ukiiona safari ndefu uliyonayo
[ ] Hutapoteza muda ovyo kwa sababu utajiona unajichelewesha tu
[ ] Kila utakachokipanga utajisukuma utoe matokeo na sio sababu ili uweze kupata matokeo unayoyasubiri kwa hamu
[ ] Utajiona ni wewe ndiye mbeba maono na unawajibika kwa 100% kuifikia safari hiyo.
[ ] Hutaairisha jambo kwani muda utakaokuwa unauona utakuwa haitoshi.
Chukua hatua .
Ndugu unahitaji kutengeneza maono/ndoto ya maisha yako ili yakusaidie kuishi kwa nidhamu kubwa kisha kutimiza ndoto ambayo ndiyo njia kuu kwenda kwenye mafanikio makubwa.
Tafakari ni kitu gani kikubwa ambacho kama kusingekuwa na kikwazo chochote ungetamani uwe nacho . Huko ndiko kwa kutengenezea ndoto yako. Kila wakati angalia wapi unataka kufika kisha jitoe mzima mzima kupata kilichobora katika maisha yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz