Sababu Tano(5) Za Kwa Nini Mbegu Ya Uwezo Wako Haizalishi Msitu Wa Mafanikio
Mbegu yoyote ya mti inakuwa imebebea msitu ndani yake. Hii hutokea pale mbegu ile inapozikwa kwenye udongo, kuota na kisha kukua na kuwa mti mkubwa unaoweza kuzalisha mbegu nyingine. Mbegu za mti huo zikioteshwa zaitazalisha mbegu nyingine nyingi na hivyo baadaye kutengeneza msitu.
Lakini mbegu hiyo haitafikia hatua ya kuwa msitu kama haitakubali kuzikwa na kutengenezewa mazingira mazuri ya kumea. Katika mazingira ya kidunia, kuzikwa ni kufa. Ili iweze kuota huzikwa kwenye udongo na kumwagiliwa, ili kutoa vimelea ambavyo baadayae hutengeneza mizizi na matawi na kuwa mti mkubwa. Isipokubali kufa, itaendelea kubakia katika hali yake ile ile na hivyo duniai kukosa mti na msitu ulio ndani yake.
Kama mbegu ya mti ilivyo na uwezo wa kuzalisha msitu, binadamu naye ana mbegu ndani yake ambayo akikubali kuizika ikafa, ataweza kuzalisha msitu wa mafanikio. Mbegu hiyo ya binadamu ni uwezo wake wa kipekee ambao upo ndani yake tangu kuzaliwa. Kupitia mbegu hiyo, binadamu ana uwezo wa kufanya mambo makubwa na kuzalisha msitu wa mafanikio. Lakini dunia imeshindwa kushuhudia misitu ya mafanikio kutoka kwa binadamu kwa sababu mbegu hizo ndani hazifi na hivyo kubakia katika hali yake ile ile.
Kama umekuwa ukiishi na kuona hakuna dalili za msitu wa mafanikio unaoutengeneza basi jua kuna mazingira ambayo umeyatengeneza yanayofanya mbegu ya uweo wako isife na hivyo kuendelea kuishi maisha ya kawaida. Zifuatazo ni sababu tano ambazo zimesababisha kutotengeneza msitu wa mafanikio yako licha ya kuwa na mbegu ya uwezo huo ndani yako kwa muda mrefu. Zijue sababu hizo na anza kuzifanyia kazi mara moja ili uweze kuizika mbegu yako ya uwezo na kuzalisha msitu wa mafanikio yako.
Mtazamo: Vitu vinakuwa kwako namna akili yako inavyoviona. Je unaamini kuwa una uwezo mkubwa ndani yako ambao umelala tu unasubiri kuamshwa ili uweze kufanya mambo makubwa? Umeshindwa kuuamsha uwezo wako kwa kuwa na matazamo hasi juu ya uwezo wako. Kwa kuamini kuwa kuna watu wachache waliopendelewa uwezo wa kipekee, umetengeneza mazingira ya mbegu yako ya uwezo kutoota na kutengeneza msitu wa mafanikio. Kuaniza sasa amini kuwa uwezo ambao unafikiri watu wachahce wamependelewa upo pia kwako, hivyo unaweza na wewe kufanya mambo makubwa.
Mazoea: Mtu anapopanga kuruka mbali zaidi ya alivyoruka awali, hukusanya nguvu nyingi zaidi ili aweze kufika mbali zaidi. Mazoea yamekuwa sumu kubwa sana kwenye kusababisha mbegu ya uwezo wako isife. Huwezi ukaamusha nguvu ambazo bado zipo ndani yako kama hutataka kufanya tofauti na ulivyozoea. Anza kuua mazoea katika maeneno mbalimbali ya maisha yako kwa kufanya zaidi na nje ya ulivyozoea.
Mafanikio yako ya sasa: Kiasi kidogo cha uwezo ulichokitumia kimekupa majibu ambayo umeridhika nayo. Ulipojaribu kujilinganisha na wanaokuzunguka umeona umepiga hatua kubwa sana na kuhisi upo kileleni. Ndugu licha ya hicho ulichokipata, bado umetumia kiasi kidogo sana cha uwezo wako. Shukuru kwa kile ulichokipata na kisha anza kuweka mipango ya kupata mafanikio makubwa zaidi ya hayo uliyonayo sasa. Kuendelea kukumbatia mafanikio ya sasa ni kuifanya mbegu ya nguvu ambazo hujazitumia kutokumea.
Watu wanaokuzunguka: Je wanaokuzunguka wanasaidia kuamsha uwezo wako au ndiyo wanaubembeleza uendelee kulala? Mafanikio yako ni wastani wa mafanikio ya watu watano wanaukuzunguka. Kama wanaokuzunguka hawaamini kuwa wana mbegu za uwezo ndani yao ya kutengeneza msitu, usitarajie watakuwa chachu kwako kuamsha uwezo wako. Hakikisha unachangamana na watu wenye kiu ya kutafuta mafanikio makubwa.
Maigizo: Kila mtu ameumbwa kwa upekee na hivyo kuwa na upekee mkubwa ndani yake. Unapofanikiwa kujua upekee huo ndipo unapotengeneza mazingira mazuri ya mbegu ya uwezo wako kufa na kuzaa msitu wa mafanikio. Kwa sababu ya kutotambua upekee wako, umekuwa unaishi maigizo. Haya ni maisha ya kuangalia mtu mwingine anachokifanya na kisha na wewe kufanya hicho hicho. Kuna vitu vya kipekee unavyoweza kuvifanya kwa viwango vya juu ambavyo watu wengine hawawezi kuvifikia. Usikilize moyo wako utakuambia upekee huo, anza kuvifanya ili kuifanya mbegu yako kuota na kutengeneza msitu.
Ndugu! Hizi ni miongoni mwa sababu zinazokufanya kutotengeneza msitu wa mafanikio kutoka kwenye mbegu ya uwezo iliyopo ndani yako. Zifanyie kazi sababu hizo ili kutengeneza mazingira rafiki kwa uwezo wako kuamka na kufanya mambo makubwa yatakayokupa mafanikio makubwa.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952
Email: alfred@amshauwezo.co.tz