Jinsi Ya Kujenga Siku Yenye Shauku Na Mafanikio Makubwa.
Kuna siku ulitamani usiku uishe mapema ili uamke. Kuna siku ulikuwa usingizini lakini ulikuwa unaiona asubuhi ungali bado umelala. Hii ni siku uliyoamka hata kabla ya alamu haijalia. Je unaukumbuka usiku huo?
Huu ulikiwa ni usiku ambao ulikuwa unausubiri uishe ili ukutane na jambo kubwa na zuri. Je ilikuwa ndiyo siku ya kuoa ambayo uliisubiri kwa siku nyingi? Je ilikuwa ni siku ya kusafiri kwenda sehemu ambayo umeitamani kwa siku nyingi? Je ilikuwa ni siku ambayo ulikuwa unakwenda kupanda ndege kwa mara ya kwanza? Je ilikuwa ni siku ambayo ulikuwa unaenda kupokea ulilomdai mtu kwa muda mrefu?
Ndugu! Hamu uliyokuwa nayo juu ya siku ile ndiyo unayotakiwa kuwa nayo kila siku. Inapoisha siku moja na kisha kuamua kwenda kupumzika lazima uwe na hamu kubwa ya siku inayofuata.
Unaweza ukatulia kidogo kisha kujiuliza, kunapokucha huwa unajisikaje? Je huwa unakuwa na shauku kubwa ya kukiacha kitanda na kuianza siku hiyo kwa shauku kubwa? Au huwa unachukia kwa nini kumekucha? Jibu utakuwa nalo mwenyewe.
Leo nataka nikuambie jinsi unavyoweza kuianza siku yako kwa shauku kubwa. Jinsi ambavyo utatamani asubuhi ifike na uianze mpya. Hii ndiyo siri kuu ya mafanikio makubwa maishani mwako.
Kumbuka kitu kilichokufanya uisubiri asubuhi kwa hamu kubwa kwenye maswali niliyouliza hapo huu. Unachotakiwa kufanya hapa ni kutafuta kitu kimoja ambacho unafikiri ukikipata maishani mwako utakuwa umeyaishi maisha yako kikamilifu.
Hiki ni kitu ambacho upo tayari kuvipoteza vitu vingine vyote na kukipata hicho. Hiki ni kitu ambacho upo tayari kuweka nguvu, muda na umakini wako. Hiki ni kitu ambacho ukikipata unakuwa umepata vyote. Ni kipi hicho?
Je ni kuwa na utajiri utakaokupa uhuru wa kifedha?
Je ni kujenga biashara kubwa yenye mafanikio makubwa?
Je ni kujijenga na kuwa kiongozi mkubwa utakayeongoza na kuleta mageuzi makubwa chanya?
Je ni kujenga uwezo fulani utakaokuwezesha kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii?
Kaa chini kisha jenga picha kamili ya kile unachokitaka. Hakikisha umejenga picha iliyowazi kabisa yaani akili yako ione waziwazi kabisa kitu unachokitaka.
Baada ya kujenga picha ya wazi kabisa. Piga picha ya matokeo utakayoyapata baada ya kukipata kile unachokitaka. Ona kama tayari unamiliki kitu hicho.
Kifahamu kitu hicho leo tena sasa. Kijengee taswira hiyo kisha kesho na kila siku itakuwa ya shauku na mafanikio makubwa.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz