Si Ukamilifu…..Bali Upekee.


Categories :



Bahari ni kubwa na nzuri lakini ina chumvi na giza kwenye kina kirefu. Anga huonekana lipo mbali sana lakini kila wakati hufunikwa na mawimgu. Licha ya uzuri wa mwezi lakini huwa na shimo katikati.

Haya yalikuwa ni majibu ya Bobby Marley, mwanamziki nguli alipoulizwa kama kuna mwanamke kamili. Baada ya majibu hayo hapo juu alihitimisha kuwa kila kitu kizuri siyo kamili bali ni maalumu/pekee.

Na kwa sababu alikuwa ameulizwa kuhusu mwanamke akasema kuwa kila mwanamke ni wa kipekee.

Lakini kuna somo kubwa sana la kujifunza hapa. Kwenye kila kitu utakachokutana nacho, ukisema uangalie kama kina udhaifu, bila kujali uzuri wake, utakikuta na udhaifu.

Kuna msemo huwa wanasema ukimchunguza sana nyoka, utamkuta ana miguu. Hivyo ile sifa ya nyoka kuwa na kasi licha ya kutokuwa na miguu inaweza kuharibikia hapo.

Hivyo faida pekee unayoweza kuipata unapokutana na mtu, kitu au hali fulani ni kujitahidi kuwa chanya ili uweze kuuona upekee wake. Kadhalika ili uweze kutoa upekee wako basi hakikisha unaweka jitihada kutoa upekee wako badala ya kutaka kumridhisha kila mtu.

Hii ni misingi unayoweza kuitumia ili kufaidika na vitu vizuri vinavyokuzunguka;

1. Kila mtu unayekutana naye ana kitu maalumu, kitazame na kukipata hicho, achana na udhaifu wake.

2. Kila hali hata zile unazoziona zina maumivu kuna kitu cha kujifunza. Angalia upande chanya

3. Kwenye kila kitu uanchofanya, weka jitihada kutoa upekee wako na siyo kuhangaika kumridhisha kila mtu.

4. Kama kuna mtu unamuona ni wa pekee basi huo ni ushahidi tosha kuwa na wewe ni wa pekee.

5. Ukamilifu, utajiri na ridhiko la maisha yako lipo kwenye kuishi upekee wako. Kutafuta na kuuishi upekee wako kiwe kipaombele cha maisha yako.

Hatua ya kuchukua: Kaa chini kisha tafakari kuhusu upekee wako. Utafanikiwa kutambua upekee wako kwa kujiuliza ni kitu gani unapenda sana kukifanya na unakifanya kwa viwango vya juu mpaka wengine wanakushangaa? Huko ndiko upekee wako uliko.

Kila la kheri.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *