Tengeneza Mtazamo Kisha Weka Viwango
Kuna chujio lipo katikati ya vitu halisi na macho ya binadamu. Chujio hilo ni mtazamo. Vitu vingi unavyoviona si katika uhalisia wake bali kulingana na chujio hilo. Kumbe watu wawili wanaweza wakakutana na jambo moja lakini wakawa wanaona tofauti. Hii ni sababu mojawapo ya watu kutofautiana viwango vya mafanikio hata kama wamekuwa eneo moja kwa muda sawa na nafasi sawa ya kutumia rasilimali zilizopo.
Mtazamo una nafasi kubwa sana katika kufikia hatua kubwa ya mafanikio katika maisha yako. Kumbe ili uweze kufikia ukuu wa maisha yako huna budi kutengeneza mtazamo mzuri juu mambo mbalimbali yanayoathiri mafanikio yako. Una mtazamo gani kuhusu utajiri? Una mtazamo gani kuhusu afya? Una mtazamo gani kuhusu mahusiano? Huna budi kutengeneza mtazamo sahihi kwenye kila eneo la maisha yako. Tengeneza matazamo kuwa una haki ya kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako. Pia ona jukumu la mafanikio ya maisha yako ni lako.
Baada ya kutengeneza mtazamo sahihi ya juu ya mafanikio yako, kuna jambo moja muhimu ambalo huna budi kulifanya ili uweze kuyafikia mafanikio hayo tena kwa viwango unavyostahili. Jambo hilo ni kuweka viwango. Ni kweli una mtazamo sahihi wa kuwa huru kifedha, je ni kwa kiwango gani? Kiasi gani cha fedha kitakuweka huru? Una mtazamo sahihi kuwa ili uweze kufikia mafanikio makubwa lazima uilinde afya yako, je utafanya nini kwa viwango gani ili uweze kuilinda afya yako? Baada ya kuwa na mtazamo sahihi juu ya safari ya maisha yako ya mafanikio anza kuweka viwango sahihi katika maeneo yafuatayo;
Binafsi: Hili ni eneo la maisha ambalo linakuhusu wewe moja kwa moja. Hiki ni chanzo cha mafanikio makubwa ya nje. Huwezi kukua nje zaidi ya ulivyo ndani. Eneo hili linahusisha akili yako, nidhamu, hekima nk. Weka viwango vya juu katika eneo hili ili uweze kufanikiwa kufikia viwango vya nje yako. Weka kiwango cha juu sana kuhakikisha unafanya vitu ambavyo unakuwa umepanga. Katika nidhamu usiruhusu sababu yoyote ya kwa nini usifanye yale muhimu uliyoyapanga.
Fedha: Tumeshindwa kufikia uhuru wa kifedha kwa sababu ya kuishia kuwa na mtazamo wa kuwa na fedha nyingi. Nenda zaidi ya mtazamo huu wa kuwa na fedha nyingi kwa kuweka viwango kwenye kiasi cha fedha ambacho inabidi ukitafute ili ufikie uhuru wa kifedha. Kiasi gani kitakupa uhuru wa kifedha? Kiasi gani utakusanya kila wiki, mwezi, mwaka au miaka kumi? Akiba kiasi gani utaweka kwenye kila kipato chako? Weka bayana haya na hakikisha unaweka nguvu kuvifikia viwango hivyo.
Kazi: Kazi umekuwa msingi wa kufikia mafanikio unayoyatamani. Hata kama utakuwa umeweka mipango mizuri kiasi gani kama hutaweka kazi ni bure tu. Baada ya kutambua kuwa itakubidi kuweka kazi ili ufikie mafanikio unayoyataka, kinachofuata ni kuweka viwango vya juu kabisa katika kazi zako. Kiwango mojawapo cha kuzingatia ni ubora wa kazi. Usifanye kazi mradi umefanya, bali hakikisha kazi yoyote unayokubali kufanya unaifanya kwa ubora wa hali ya juu sana.
Mahusiano: Huwezi kufikia mafanikio makubwa kwa kufanya peke yako. Unahitaji watu ili uweze kufikia ukuu wako. Mafanikio yanapatikana kwa kutoa thamani kubwa kwa watu wengine. Huwezi kuwapa thamani kubwa watu wengine kama hushirikiani nao vizuri. Mahusiano mazuri yanabebwa na upendo. Weka viwango vikubwa vya kuwapenda watu wengine. Viwango vikubwa vya kumpenda mtu mwingine vinahusisha kuupenda utu wa mtu mwingine na si alivyonavyo. Weka viwango vizuri vya mahusiano ya roho yako kwa kuabudu, kutafakari nk.
Afya: Viwango vya kazi ulivyoweka huwezi kuvifikia kama viwango vyako vya afya vitakuwa chini. Kuna afya ya mwili, roho na akili pia. Weka viwango vya juu vya kuulinda mwili wako dhidi ya magonjwa kwa kufanya mazoezi, kula vizuri na kupumzika. Hakikisha unalisha akili yako maarifa sahihi na kuepuka mambo hasi.
Kuwa na mtazamo chanya peke yake haitoshi kukufikisha kwenye mafanikio unayoyatamani. Huna budi kuongeza kipengele kingine cha viwango ambavyo vitakuongoza kasi ya kueleke kwenye uelekeo sahihi uliochagua. Tafakari maeneo mbalimbali ya maisha yako na weka viwango ambavyo utaviishi kila siku.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz