Hizi Ni Ishara Za Kuwa Umetabiri Mafanikio Katika Maisha Yako…
Umekuwa ukisikia kuhusu utabiri wa hali ya hewa; mwaka huu kutakuwa na mvua nyingi au chache, kuna kimbunga kitatokea maeneo fulani au mwezi utapatwa siku fulani. Kwa asilimia kubwa tabiri hizo zimekuwa zikitimia.
Wanaotabiri ni wa taalamu wa mambo hayo wanayotabiri. Ukiacha hali ya hewa, upo utabiri ambao na wewe unaweza kuufanya. Huu ni utabiri kuhusu maisha yako.
Kwa sababu matamanio makuu ya maisha yako ni kufanikiwa, ni lazima utabiri kuhusu mafanikio yako ndipo uyapate mafanikio hayo. Wewe ndiye mtabiri mkuu wa maisha yako; yawe ya mafanikio au kushindwa.
Haya ni maeneo ambayo unapaswa kuyawekea utabiri ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio makubwa;
1. Kuwa na ndoto kubwa. Kujenga ndoto kubwa maishani mwako na kuiishi ni kujitabiria kuwa na mafanikio makubwa. Kuwa na malengo madogo ambayo hayakusukumi kuchukua hatua kubwa ni kujitabiria kushindwa au kuwa na mafanikio madogo.
2. Kuwa na malengo na mipango. Malengo ni mwongozo wa kitu sahihi cha kufanya na mipango ni njia za kupatia matokeo. Kuishi kwa malengo na mipango kila wakati ni utabiri wa kuwa utapata matokeo sahihi.
3. Kuweka kazi. Kuweka kazi kwenye mipango yako ni utabiri wa kupata matokeo kwenye malengo yako. Kama unaweka kazi sahihi, tabiri kabisa kuwa utapata matokeo sahihi.
4. Uvumilivu. Mgonga mawe hutabiri kuwa mwisho wa jitihada zake atapata kokoto kutoka kwenye jiwe analoliponda kwa sababu ya uvumilivu wa kuendelea kushusha nyundo. Tabiri kuwa magumu unayopitia sasa yatakupa matokeo kwa kuendelea kuweka jitihada sahihi hata kama hupati matokeo sasa.
5. Ishi upekee wako. Utakapoamua kuwa wewe kwa kuacha kuiga maisha ya watu wengine, au kusikiliza maoni hasi ya watu wengine utakuwa unajitabiria kupata mafanikio makubwa maishani mwako. Kwa sababu ya kufanya kwa upekee, matokeo haya yatakupa ridhiko ndani ya moyo wako.
Ndugu! Kama hujitabirii mafanikio, moja kwa moja unajitabiria kushindwa. Ni bora sasa uanze kutabiri kwa kuchukua hatua hizo hapo juu na mafanikio kwako yatakuwa uhakika.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz