Kutokuchukua Hatari Ni hatari Zaidi……


Categories :

“Kama mgonjwa atafanikiwa kuzuia kutochomwa sindano kwa sababu ya kuogopa maumivu anayoweza kuyapata basi ana hatari kubwa ya kupoteza maisha yake”

Kuchukua hatari kuna maumivu. Maumivu makuu yamejengwa kwenye misingi miwili mikuu. Kwanza ni kulazimishwa kutoka nje ya mazoea. Pili ni kutokuwa na uhakika wa matokeo.

Kuchukua hatari ni kufanya kitu ambacho hujazoea. Hivyo inakuhitaji wewe ujivute au kujitanua zaidi kwenye fikra zako, imani yako lakini na nguvu ya mwili. Hii huleta maumivu na watu wengi hawataki maumivu.

Kuchukua hatari ni kitendo cha imani kwani utafanya kitu ambacho huna uhakika wa matokeo yake. Kwa mfano kuanza kufanya biashara ambayo hujawahi kuifanya. Unahitaji imani mpya na wengi huamua kutochukua hatari hiyo na kuendelea kufanya ambavyo wana uhakika wa matokeo.

Njia rahisi ambayo watu wamekuwa wakikwepa maumivu ya kuchukua hatari ni kutokuchukua hatari. Wamebaki kwenye mazoea bila kujishughulisha kufanya vitu vipya.

Hakuna kukua kwenye mazoea. Kufanya kitu kile kile ni kukubali kusimama palepale kila siku. Asili haihitaji mtu asimame, kama hukui basi unakufa.

Hivyo usijione mjanja kutokuchukua hatari, kwani kwa kutokufanya hivyo umekaribisha kifo; Anza kuchukua hatari zilizopimwa sasa;

  1. Chukua hatari ya kuanzisha biashara ili kukuza kipato chako, ajira pekee haitoshi.
  2. Chukua hatari ya kuwafikia wadau wakubwa wa biashara yako, hao watakupa faida kubwa.
  3. Chukua hatari ya kuachana na baadhi ya watu ambao hawaungani na ndoto yako kubwa uliyonayo.
  4. Chukua hatari ya kuanza kuishi maisha yako ya kipekee. Usiogope huko ndiko kwenye ukuu wako.
  5. Chukua hatari ya kuweka malengo makubwa zaidi ya yale uliyokwisha yafikia. Hii ni njia pekee ya wewe kukua.

Kumbuka kutokuchukua hatari ni hatari tayari kwani utakufa kwa mazoea.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *