Sifa Tano(5) Za Malengo Bora Yatakayokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa


Categories :

Licha ya ndege kuwa angani kwa kimo kirefu kutoka ardhini lakini rubani wake hufanikiwa kusafiri maili nyingi na kuifikisha ndege hiyo bila ya kupotea. Hii ni kwa sababu hutumia dira iliyopo kwenye chombo hicho kukiongoza kwa usahihi. Kadhalika treni huhitaji reli ambayo itaiongoza kwa kupita juu yake na kufika inakotarajiwa salama.

Kuna hatua unazotamani kupiga mwaka huu na miaka inayofuata ya maisha yako. Mafanikio ya matarajio hayo utayapata kama utakuwa na dira kama ilivyo kwa rubani au kama yatatengenezewa reli kama treni. Dira na reli kwa mafanikio yako unayoyataraji ni malengo. Huwezi kupiga hatua kubwa bila kuwa malengo. Huu ndiyo mwongozo wako sahihi wa kukuwezesha kuchukua hatua sahihi kwa kile unachotaka kitokee maishani mwako.

Kuwa na malengo si jambo geni kwenye masikio ya watu wengi. Watu wengi wamekuwa wakisikika kuwa wana malengo au wakiweka malengo. Lakini shida imekuwa namna ya kuweka malengo hayo. Malengo mengi yamekosa ubora na hivyo kusababisha kupata matokeo yasiyo bora kwenye yale waliyoyapanga. Naenda kukushirikisha sifa tano za malengo bora ambazo ukizizingatia katika kuweka au kurekebisha malengo yako utafanikiwa kupiga hatua kubwa mwaka huu na miaka ijayo.

Sifa tano za malengo bora zinaainisha na neno SMART likiwa ni kifupisho cha maneno matano ambayo ni Specific, Measurable, Attainable, Realistic na Time;

1. Specific (Malengo yawe maalumu):  Lengo lolote unalolipanga lazima liwe wazi kabisa likielezea ni nini hasa unataka kukikamilisha. Usiliweke lengo kwa ujumla wake. Kwa mfano kama una lengo la kuongeza kipato mwaka huu, usiishie kusema nataka kuongeza kipato mwaka huu. Badala yake sema kabisa nataka kuongeza kipato mwaka huu kwa sh…… au kwa asilimia…. Lengo ambalo ni maalumu linakuwa rahisi kutathminiwa.

2. Measurable (Malengo yapimike): Kwenye kila lengo unaloliweka hakikisha kunakuwa na kitu unachoweza kukipima. Utazalisha nini kwenye yale unayotaka kuyafanya? Kama ni kuongeza kipato unaweza kupima kwa kiasi cha fedha kinachoongezeka. Kama lengo ni kuikuza biashara unaweza kupima kwa idadi ya wateja au mauzo. Weka wazi ni nini utakipima kwenye lengo unaloliweka.

3. Attainable (Malengo yafikike): Je unachokipanga unaweza kukifikia. Weka lengo ambalo wewe mwenyewe unaamini unaweza kulifikia. Usiweke lengo kwa kumkomoa mtu mwingine au ionekane na wewe una malengo makubwa. Malengo ambayo wewe mwenyewe huamini kuwa unaweza kuyafikia, yataishia kukukatisha tamaa.

4. Realistic (Malengo yawe halisi): Je unachokipanga kukipata kipo? Je asili ina kitu kama hicho? Lengo lako liwe na kitu ambacho kinaakisi uhalisia na sio kinachoenda kinyume na asili. Kuna vitu huwezi kuvipata ndani ya muda mfupi, hivyo ili kuwa halisi lazima uupe muda nafasi yake. Weka lengo ambalo unaona unaweza kuliweka kwenye vitendo na likatokea.

5. Time (Malengo yawe na muda maalumu):  Lengo lenye sifa bora hupewa muda maalumu kufikiwa. Usiweke lengo ambalo halina ukomo kwani itakuwa ngumu sana kulifikia. Baada ya kujua ni kiasi gani cha kipato unataka kukiongeza, jipangie muda wa kuhakikisha utakuwa umeshakiongeza kipato hicho. Bila kuweka muda maalumu wa kukamilisha utakosa msukumo. Malengo ambayo yanakosa muda maalumu huishia kupotelea njiani au kupata matokeo madogo sana.

Hizi ndiyo sifa tano za malengo bora. Tumia sifa hizi kuweka malengo yako bora ya mwaka huu mpya na malengo ya muda mrefu pia. Kama ulishaweka malengo, chunguza malengo yako kama yana sifa zilizoainishwa hapo juu na kisha yarekebishe. Malengo bora ndiyo dira kuu ya hatua utakazokuwa unapiga, hivyo kupata mafanikio makubwa hakikisha unakuwa na malengo bora.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *