Utafanikiwa Kumla Ng’ombe Mzima Kama Utamkata Vipande


Categories :

Kila mtu aliyepo hapa duniani ana uwezo wa kipekee wa kufanya mambo makubwa ambayo huachwa kama alama ya yeye kuwepo hapa duniani. Anayefanikiwa kufikia mafanikio makubwa ni yule anayetengeneza ndoto kubwa na kufanikiwa kuiishi kikamilifu.

Ndoto kubwa hutimia kwa kuiwekea malengo. Kadri unavyokuwa na ndoto kubwa ndivyo inavyohitaji kuwa na malengo makubwa ili uweze kuitimiza kikamilifu. Hivyo malengo yaliyo sahihi ni yale yanayotokana  na ndoto yako. Kwa kuwa ndoto ni kubwa na zinachukua muda mrefu, vivo hivyo kwenye malengo.

 Malengo makubwa huogopesha na kukatisha tamaa, ni kama unapokuwa na ng’ombe mbele yako na inabidi umle mpaka umalize. Fikra ya kwanza itakayokuja kichwani mwako ni kuwa haiwezekani na kuahirisha kuona hilo litakuwa ni zoezi gumu. Lakini ukiamua kumkata ng’ombe huyo vipande vipande na kuanza kumla kidogo kidogo una nafasi kubwa ya kummaliza ng’ombe mzima tofauti na ulivyokuwa unafikiri mwanzoni.

Hivi ndivyo inavyobidi ufanye kwenye malengo makubwa uliyo nayo. Ligawe lengo kubwa ulilonalo vipande vidogo vidogo. Kama una lengo la kukamilisha kwa miaka kumi unaweza kuligawa kwenye vipande vya mwaka mmoja, miezi mitatu, mwezi , juma na kisha siku. Kwa mfano kama lengo la miaka kumi ni kuwa na kipato cha shilingi milioni mia moja, huna budi kugawa lengo hilo ili kujua ni kiasi gani utatakiwa uzalishe ndani ya mwaka, miezi mitatu, mwezi, juma na kisha kila siku. Kwa kutumia mfano huu itabidi uingize kipato cha shilingi milioni kumi kila mwaka, sh laki nane na elfu thelathini na tatu kila mwezi, sh laki mbili na elfu nane  mia tatu na thelathini na tatu kila juma na sh elfu saba mia nne na arobaini kila siku.

Ulipoitazama sh milioni  mia moja ilionekana kubwa sana na kama kitu ambacho hakiwezekani lakini baada ya kugawa na kuona ili ufikishe kipato hicho kikubwa inabidi uzalishe sh. elfu saba mia nne na arobaini kila siku kinaonekana sasa ni kitu kinachowezekana. Hii ndiyo faida ya kumwangalia ng’ombe kama vipande vipande na sio yeye mzima.

Muda ambao unaweza kuchukua jukumu la kutimiza lengo lako umefichwa kwenye siku. Mafanikio makubwa unayoyashuhudia ambayo mwanadamu ameyapata yalifichwa kwenye matumizi sahihi ya siku. Kipato cha milioni mia moja unachoweza kutarajia baada ya miaka kumi, kitafikiwa baada ya kufanikiwa kupata sh elfu saba mia nne na arobaini kila siku. Ndiyo maana wanasema mafanikio makubwa ni jumla ya jitihada ndogo ndogo zinazokusanywa kila siku. Hakikisha unaiishi siku yako kikamilifu.

Ili uweze kukamilisha malengo makubwa huna budi kujifanyia tathmini kila wakati. Baada ya kuligawa lengo lako mpaka kwenye hatua ya siku, kila mwisho wa siku kaa chini na jiulize ni kwa kiasi gani umefanikiwa kuiishi siku hiyo kikamilifu? Tathmini pia kila baada ya miezi mitatu na mwaka. Tathmini inaonyesha uhai wa utekelezaji wa malengo yako. Pia tathmini zitaainisha changamoto ambazo zinajitokeza kwenye utekelezaji wa malengo yako na kuja na majawabu bora ya kung’atuka kutoka kwenye mkwamo wowote ule.

Ndugu! Angalia malengo uliyonayo, na yale uliyoyaacha kwa kukutatishwa tamaa na ukubwa wake, kisha yagawe vipande vipande ambavyo itakuwa rahisi kuanza utekelezaji wake. Tambua kwa wazi kabisa nini unachotakiwa kukifanya kila siku ili kukamilisha lengo lako kubwa. Fanya tathmini mara kwa mara ili kujua mwenendo wa utekelezaji wa lengo lako. Kwa kufanya hivyo utamla ng’ombe ambaye mwanzoni alikuwa anakutisha mbele yako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *