Vigezo Sita(6) Vya Kuzingatia Unapochagua Nini Ufanye Ili Upate Mafanikio Makubwa.
Kila binadamu aliye hai huwa kuna kitu anachofanya kila wakati. Zama hizi kila mtu amekuwa ‘busy’ akifanya kitu. Kutopata mafanikio si kwa sababu ya watu kutofanya vitu bali kuna sababu nyingine ya msingi. Waliofanikiwa na wasiofanikiwa wote huondoka asubuhi wakiwa na nguvu na hurudi nyumbani jioni wakiwa wamechoka, hii ni ishara kuwa kila mtu kuna kitu ambacho amekuwa akikifanya kutwa nzima. Kadhalika kama umeishi hapa duniani kwa muda mrefu, ni ishara kuwa kuna vitu umekuwa ukivifanya ambavyo vimekupa maisha uliyonayo sasa.
Kumbe unachokipata ni matokeo ya kile unachokifanya. Unafanya nini? Kumbe siri ya mafanikio ya maisha yako imejificha kwenye kile unachokifanya. Kufanikiwa au kushindwa kutategemea vile vitu unavyochagua kuvifanya hata kabla ya muda unaoutumia kufanya vitu hivyo. Watu ambao wapo busy ni wengi lakini wanaopata mafanikio na kuishi maisha ya furaha na ridhiko ni wachache sana.
Kumbe kuna mtihani mkubwa ambao watu wengi wanafeli katika kuishi maisha yao hapa duniani. Mtihani huo ni kuchagua na kusimamia kitu cha kufanya. Usifanye chochote bila kuwa na machaguo ya nini ufanye kwa kutumia mtaji wa muda ambao kila mtu anakuwa amepewa.
Vifuatavyo ni vigezo sita(6) vya kuzingatia ili uweze kuchagua vitu vya kufanya vyenye faida na vitakavyokupa mafanikio makubwa maishani mwako;
- Fanya vinavyotoka ndani mwako. Dunia ina vitu vingi sana vya kufanya, kama hujachagua nini cha kufanya utakupa vitu kwa kufanya. Hivyo ndivyo ambavyo watu wengi wapo busy kuvifanya na hivyo kuishia kuwa watu wa kawaida licha ya kuwa busy muda wote. Vitu vinavyotoka ndani yako vinaendana na kusudi lako na hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kutumia uwezo wako wa kipekee na kufanya mambo makubwa. Ni kwa kufanya vitu vinavyotoka ndani yako ndipo unapoweza kuamsha uwezo wako mkubwa uliopo ndani yako. Usifanye chochote, bali sikiliza ndani yako nini ulicholetewa ukifanye na fanya hicho.
- Fanya kinachoongeza kipato. Maisha ya mafanikio ya duniani yanahitaji fedha tena fedha nyingi. Utafanikiwa kuishi maisha yako kwa uhuru kama utakuwa na fedha nyingi. Japo fedha si kila kitu lakini ni vitu vingi. Unapoamua nini ufanye, basi moja ya kitu ambacho inabidi uwe busy nacho ni kutengeneza kipato kikubwa ambacho kitasaidia kuishi maisha mengine kwa mafanikio makubwa. Unachokifanya kinaingiza kipato kiasi gani?
- Fanya kitakacholinda na kuboresha afya yako. Afya yako ni mtaji mkubwa sana wa maisha yako. Ni kitu kimoja wapo ambacho inabidi ukipe muda ili kuweza kuishi maisha yako kwa ufanisi. Unapochagua nini cha kufanya, hakikisha unapanga kufanya vitu vitakavyolinda na kuboresha afya yako ya mwili kupitia, mazoezi, chakula na mapumziko. Lakini afya huhusisha akili na roho pia. Je unachokifanya kinalinda na kuboresha afya ya mwili, akili na roho kwa kiasi gani?
- Fanya vinavyoongeza mahusiano. Hakuna mafanikio ya maana ambayo hayahusishi watu. Ili uweze kufanikiwa unahitaji kuwa na mahusiano mazuri na wengine. Mahusiano mazuri huboreshwa na thamani unayowapa wengine ikiwa pamoja na muda. Je unatenga muda mzuri wa kukaa na watu wako wa karibu kwa mfano familia? Je inaipa thamani gani jamii unayoizunguka? Unapochagua nini cha kufanya kwa muda ulio nao, moja ya kigezo ni kuimarisha mahusiano.
- Fanya kile kinachotoa thamani: Chagua kufanya kitu kitakachokuwa na thamani kwako au kwa watu wengine. Thamani unayoitoa ndiyo inayoamua kiasi cha mafanikio unayokuwa nayo. Ili kufikia mafanikio mkubwa huna budi kuwa busy kutoa thamani kubwa kwako na kwa watu wengine.
- Fanya kinachoongeza maarifa. Tunafanya vitu kutokana na tunavyojua. Tunaviona vitu kutokana na mtazamo tulionao. Kujua na kutazama vitu vinachangiwa kwa asilimia kubwa na maarifa tuliyonayo. Kumbe ili kuboresha utendaji wetu na mitazamo yetu hatuna budi kuendelea kuwekeza kwenye maarifa. Je unachokifanya kinaongeza maarifa?
Ndugu njia pekee ambayo unaweza kunufaika na kuchoka kwako baada ya kuwa busy ni kuwa na vipaumbele kwenye vitu unavyovifanya. Kabla hujafanya chochote kaa chini na tafakari mchango wa kile unachofanya kwenye mafanikio yako na si kufanya chochote kinachokuja mbele yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.
Mawasiliano:
Simu: 0752 206 899/0714 301 952
Email: alfred@amshauwezo.co.tz