Je Umekuwa Ukisubiri Muda Au Ukipoteza Muda?


Categories :

Kusubiri au kupoteza muda ni jambo ambalo limekuwa linafanywa na watu kwa kujua au kutokujua. Mara nyingine mtu amefikiria anasubiri wakati kumbe  kiuhalisia anapoteza muda. Kusubiri muda ni pale unapongoja kupata mrejesho baada ya kuweka nguvu kwenye jambo fulani. Hii ni sawa na kutanguliza thamani  huku ukitarajia majibu ya thamani hiyo uliyoweka. Kupoteza muda ni kitendo kile cha kusubiria matokeo wakati hujaweka nguvu yoyote au kusubiria matokeo makubwa wakati umeweka thamani ndogo.

Kusubiri na kupoteza muda ndivyo vinavyoamua nini unapata katika safari ya maisha yako. Kusubiri na kupoteza muda vyote vinatumia muda.  Wale wanaofanikiwa katika maisha yao ni wale wanaokuwa wanasubiri badala ya kupoteza muda. Wanaosubiri wanapata mafanikio kwa sababu kabla hawajatarajia matokeo wanawekeza thamani kwanza. Wanaamini kuwa hakuna chochote unachoweza kupata maishani bila ya kuweka thamani wakati wanaopoteza muda wanaamini vitu huja kwa bahati na kuna watu fulani wanaweza kuishi maisha kwa niaba yao na hivyo wao wakabaki wamekaa.

Kwa sababu kuna muda umekuwa ukifanya vitu bila kujua unasubiri muda au kupoteza muda; au umefikiri unasubiri muda wakati unapoteza muda, naenda kukushirikisha namna ambavyo umekuwa ukipoteza muda, ili uache mara moja na kuanza kusubiri muda.

Kuma huna malengo unatengeneza mazingira ya kupoteza muda. Unapokuwa na malengo yanakuwa ni dira ya nini ufanye au utafanya na hivyo unasubiri muda kufika wa kupata matokeo kulingana na malengo unayofanyia kazi. Kama unafanya chochote kinachokuja mbele yako ujue unapoteza muda kwani kuna nafasi kubwa ya kutopata chochote.

Kama huwekezi mali unapoteza muda. Uwekezaji mwingi wenye tija unachukua muda mrefu.  Ili uweze kufikia uhuru wa kifedha huwezi kuepuka uwekezaji kama kwenye hisa, ardhi, biashara kubwa nk. Kama huanzi kuwekeza mapema na unatarajia kuwa tajiri ujue husubiri muda bali unapoteza muda.

Kama unaigiza watu wengine husubiri muda bali unaupoteza. Mafanikio makubwa huja kwa mtu kufanya kwa upekee, yaani kufanya vitu ambavyo yeye anaweza kuvifanya kwa viwango vikubwa. Anapofanya kwa viwango vikubwa anakuwa yupo kwenye nafasi ya kutoa thamani kubwa kuliko wengine. Kama unaiga watu wengine wanachokifanya na unatarajia miujiza , tambua kuwa unapoteza muda na sio kusubiri muda. Anza mara moja kuishi upekee wako kwa kutambua kwanza nini cha pekee kilichopo ndani yako.

Kama unawalalamikia watu wengine kwa matokeo ya maisha yako ujue unapoteza muda. Je unafikiri kushindwa kwako kumesababishwa na wazazi wako kwa kutokukupeleka shule? Je unailaumu serikali yako kwa maisha yako magumu kwamba imeshindwa kutengeneza mazingira mazuri ya wewe kufanikiwa? Kama umekaa na kuridhika na hali yako kwa kuamini kuna watu wa kuwatwisha mzigo wa lawama kwa kushindwa kwako, ujue unapoteza muda na sio kusubiri muda. Anza mara moja kuchukua jukumu la kutengeneza maisha yako.

Kama hutekelezi uliyoyapanga ujue unapoteza muda. Umekuwa na mipango mingi ya muda mfupi na mrefu, je unaitekeleza? Au imeshindwa kuwa na nidhamu ya kuhakikisha unafanya kile ulichokipanga?  Au ulipokutana na changamoto wakati unatekeleza yale uliyoyapanga ukaacha baada ya kukosa uvumilivu? Huwezi kupata matokeo yoyote kama hutachukua hatua za kutekeleza yale unayopanga. Panga na chukua hatua.

Chukua muda kutafakari katika mengi ambayo umekuwa ukifanya. Je umekuwa ukisubiri muda au kupoteza muda? Kama umekuwa ukipoteza muda, ni wakati sasa wa kubadili uelekeo. Kuishi maisha ya mafanikio huna budi kila wakati kutoa thamani na kisha kusubiri matokeo. Anza kutoa thamani ya pekee kuanzia leo huku ukisubiri muda ukupatie matokeo mazuri.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *