Huwezi Kuonyesha Ufundi Wako Wa Kuogelea Kwa Kuogelea Mavumbini Rudi Majini.


Categories :

Ukiongelea ufundi wa kuogelea majini huwezi kuacha kumtaja samaki. Hii ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutembea majini na kuepuka vikwazo vyote vilivyomo. Licha ya uwezo huo mkubwa alionao samaki lakini hawezi kuuonyesha mavumbini.  Ukimchukua samaki na kumweka nchi kazu unaweza kusema sio yeye yule anayeogelea kwa ufundi mkubwa majini. Kumbe ufundi wa samaki kuogelea unategemea maeneo.

Kama ilivyo kwa samaki binadamu naye ana ufundi wake ambao aliumbwa nao. Ufundi huo ndio ungeweza kumpa uhuru wa kufanya chochote katika maisha yake. Ufundi huo ndiyo unaotambulisha upekee wake na kufanya ajulikane kwa watu wengine. Kwa kutumia ufundi huu anaweza kufanya mambo makubwa na ya kushangaza wengine. Ufundi huo ni kipaji/vipaji vya alivyonavyo ndani yake.

Kupitia kipaji chako unaweza kufanya vitu fulani kwa utofauti mkubwa sana, kiasi cha kuwa na thamani kubwa sana kwa watu wengine. Kupitia kipaji chako na kutoa thamani kwa wengine unatarajiwa kupata mafanikio makubwa. Lakini hali imekuwa ni kinyume chake, dunia imepungukiwa sana na matokeo ya ufundi ambao watu wangeweza kuutoa. Licha ya mahangaiko waliyonayo binadamu, lakini wachache sana wameweza kutumia ufundi wao na kupata mafanikio makubwa. Lakini wengi wameishia kuwa wanyonge.  Unyonge huo si kwa sababu hawana ufundi bali unatumika eneo lisilo sahihi.

Uko wapi sasa? samaki anatarajiwa awe kwenye maji ndipo aoneshe ufundi wake, vivo hivyo unatarajiwa na wewe uwepo eneo ulilopangiwa ili uweze kuonyesha ufundi wako. Eneo lako sahihi la kuishi na kuonyesha ufundi ni kusudi lako. Hili ndilo eneo la kujidai na ndiko unakoweza kutumia vizuri kipaji chako.

Kila mtu ana sababu (kusudi) ya kuwepo hapa duniani, sababu hiyo ni maalumu kwa kila mtu. Mafanikio yako ya kuishi hapa duniani yatategemea ni kwa namna gani umeweza kuliishi kusudi lako. Ili uweze kuishi kusudi hilo kwa utimilifu umepewa kipaji/vipaji vya kukuwezesha kulitimiza.  Kutambua kusudi lako ni kutambua uwanja wa kuonyesha ufundi wako na kupata mafanikio makubwa.

Umeshindwa kuonyesha ufundi wako kwa viwango vikubwa na vya kushangaza kwa sababu ya kuwa katika sehemu isiyo sahihi. Kutokutambua kusudi lako ni kuamua kuishi maisha yoyote. Unapoamua kuishi sehemu tofauti na kule ulikotakiwa kuwepo inakuwa ni vigumu kuonyesha ufundi wako kwa viwango vikubwa.

Samaki akisogezwa na maji na kupelekwa  nchi kavu, hujitahidi arudi majini ili aendelee kuishi maisha yake kwa mafanikio makubwa. Vivo hivyo ni wakati wako sasa wa kutambua kusudi lako la kuwepo hapa duniani na kuweza kutumia vipaji vyako kikamilifu. Kujua kusudi la maisha imekuwa ni changamoto kwa watu wengi. Kutambua kusudi lako unaweza kuanza kujiuliza maswali yafuatayo: Ni kitu gani ambacho unasukumwa kukifanya kiasi cha kukumbushwa mara kwa mara hata unaponyamaza? Tatizo gani au pengo gani unaloliona katika jamii na unasukumwa kuliziba? Vitu gani unapenda kuvifanya hata kama unalipwa kidogo au hulipwi kabisa? Anza kutafakari maswali haya na kisha sikiliza moyo wako utakupa majibu.

Ukisha jua kusudi lako, na kuweka mipango ya kuishi ndipo utakapopata uwanja mzuri wa kuonyesha ufundi wa kipaji chako na kupata matokeo makubwa. Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeelezea kwa kina hatua za kuchukua ili kuweza kutambua kusudi lako na kuliishi. Pata nakala yako leo kwa kupiga simu namba 0752 2068 99 ili uweze kutegua kitendawili hiki ambacho kimekuwa kigumu kwa watu wengi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,

Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi.

Mawasiliano:

Simu: 0752 206 899/0714 301 952

Email: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *