Mfahamu Leo Adui Namba Moja Anayekwamisha Mafanikio Yako.
Mikwamo mingi ya maisha ambayo umekuwa ukikutana nayo imetokana na adui yako ambaye amekuwa akifanya bidii kuhakikisha hupigi hatua. Kwa kipindi kirefu kuna maisha ambayo umeyatamani uyafikie lakini kila unapoanza adui huyo anakuja na kukupiga vita na umeishia njiani. Mara nyingine umefikiri kuwa jirani yako ndiye anayekupiga vita usipige hatua kwa kutumia njia za kishirikina. Lakini jirani huyo siyo yeye, yupo mwenyewe ambaye ni wa ukweli.
Kumtambua adui yako anayekukwamisha usipige hatua naenda kukushirikisha njia ambayo kuku alitumia kumjua adui yake. Kuku alikuwa na mahindi yake ardhini, kadri alivyoendelea kudonoa alihisi mhindi yale yalikuwa yanaisha kwa kasi kubwa. Ikabidi aanze kumtafuta kuku mwingine ambaye anakula mahindi yake kwa siri. Alivyogeuka kulia, kushoto, mbele na nyuma karibu na alipokuwa hakumuona kuku yoyote, akazidi kuchanganyikiwa ni nani sasa anayekula mahindi yake? Alipoinua kichwa chake na kuangalia kwa mbali kidogo ambako kulikuwa na kioo, akamuona kuku mwingine akimuigilizia kila anachofanya yeye. Hapo ndipo aliposogea karibu zaidi ya kile kioo na kumuona adui yake vizuri.
Na wewe unaweza kutumia mbinu hii kumjua adui namba moja wa mafanikio yako. Nenda peke yako mbele ya kioo cha kujitazamia kisha simama hapo, unamuona nani? Huyo unayemuona mbele yako ndiye adui namba moja wa mafanikio yako. Naamini umejiona mwenyewe. Ndiyo, ni wewe mwenyewe! Kama wapo adui wengine, basi hao watafuata lakini aliyesababisha kwa asilimia kubwa maisha unayoyaishi sasa ni wewe mwenyewe. Lakini unaweza kukataa kuwa wewe umesababishaje maisha haya yanayokuumiza mwenyewe? Hivi ndivyo umekuwa adui namba moja wa maisha yako;
Umeacha watu wengine wakutambulishe wewe ni nani. Licha ya upekee uliowekwa ndani yako tangu kuzaliwa kwako lakini umewaachia watu wengine wakutambulishe wewe ni nani. Jamii imekutambulisha kuwa wewe ni mdhaifu ukakubali, ilipokuambia wewe ni wa kawaida ukakubali na ilivyokuambia wewe huna maajabu yoyote ukasema ndiyo. Kwa kuwaachia watu wakutambulishe na wewe kukubali utambulisho huo, umekuwa adui namba moja wa mafanikio yako. Tambua, utambulishe na kuuishi upekee wako sasa badala ya kuachia watu wengine wakutambulishe.
Umeacha kuishi ndoto yako na kuishi ndoto za watu wengine. Ndoto kubwa ndiyo inayokuwa dira ya maisha yako hapa duniani. Kwani utaamka kila siku asubuhi ukijua unaenda kutimiza nini. Ndoto yako ndiyo itakula muda wako mwingi. Pia ndoto yako kubwa ndiyo itakayokufanya uache alama kubwa hapa duniani na kufanya uendelee kukumbuka hata baada ya kufa. Ndoto gani unaiishi sasa? Kwa sababu maisha yanaendelea, kama huna ndoto unayoiishi basi ujue unawasaidia watu wengine kukamilisha ndoto zao. Tengeneza ndoto yako kubwa na anza kuiishi sasa.
Umeacha watu wengine wakupangie kipato chako. Je kipato unachokipata kinatosha? Je umeridhika na mshahara unaoupata? Kama hapana, umechukua uamuzi gani? Kama umeendelea kulalamikia watu au serikali kwa kipato chako kuwa kidogo, jua wewe ndiye adui wa kwanza wa mafanikio yako. Jukumu la kuongeza na kuthibiti matumizi ya kipato chako ni jukumu lako. Panga kiasi cha kipato unachotamani uwe nacho kisha toa thamani kwa watu wengine ambayo itaendana na kipato unachokitaka.
Umekubali kutumia kiasi kidogo tu cha uwezo wako. Mafanikio madogo uliyoyapata hayaendani kabisa na uwezo wako ulionao. Hata wale unaowashangaa kwa mafanikio makubwa waliyoyapata, wametumia kiasi takribani 10% ya uwezo wao. Je wewe utakuwa umetumia asilimia ngapi? Kama hujafanya jitihada za kuamsha uwezo wako, kwa mfano kwa kujipa malengo makubwa na kujisukuma kuyatimiza ujue wewe ni adui namba moja wa mafanikio yako.
Umeacha mazingira yakutawale. Je unahofia kushindwa kwenye mambo uliyopanga kufanya? Je umeshindwa kuishi kwa raha kwa sababu kuna watu wabaya wanakuzunguka? Je hasira na wivu vimekuwa mwiba kwako? Kama mambo haya yamekuwa yanatawala maisha yako ujue wewe ni adui namba moja wa maisha yako. Mawazo hasi yamekuwa ni kikwazo kikubwa katika kupiga hatua za mafanikio yako. Anza leo kujisukuma kutawala mazingira yako badala ya kuacha yenyewe yakutawale
Ndugu umeona ni kwa namna gani umekuwa adui wa mafanikio yako. Kama kuna mtu mmoja na wa kwanza wa kupigana naye ili kupiga hatua katika maisha yako, basi ni wewe mwenyewe. Anza kubadilika kwa kuutambua upekee na uwezo wako wa kipekee kisha kuchukua jukumu la kuishi ndoto yako kikamilifu. Ukifanikiwa kumushinda adui wewe, itakuwa rahisi kuwashinda na wengine.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz